Dar es Salaam. Wanafunzi 150 kati ya 1,000
waliojiunga na masomo katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es
Salaam (Duce) mwaka jana wamebainika kuwa na ujauzito waliopewa na
wenzao chuoni hapo.
Utafiti wa usawa na jinsia uliofanywa na chuo
hicho kati ya Juni na Novemba mwaka jana umebaini kuwa wanafunzi
wanaopata ujauzito ni wale wa mwaka wa kwanza.
Hayo yamebainishwa jana na Mratibu wa Masuala ya
Jinsia wa chuo hicho, Dk Dativa Shilla katika warsha ya uchaguzi na
uhusiano wa kijinsia iliyofanyika chuoni hapo.
Alisema hali hiyo inatokana na kuwapo kwa vitendo
vya ukatili, manyanyaso na ubabe unaofanywa na wanachuo wa kiume dhidi
ya wale wa kike na hivyo kuwalaz imisha kufanya mapenzi bila hiyari yao.
“Kupitia utafiti huu tumeona hakuna usawa wa
kijinsia wa kupata elimu baina ya mwanamke na mwanamume kwa sababu
mwenye ujauzito hawezi kufanya vizuri katika masomo yake ukilinganisha
na mhusika wa kiume,” alisema.
Awali, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo cha
Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Amon Katunzi alisema ni wakati sasa kwa
Serikali kutoa mikopo kwa wanafunzi wote kwa sababu hatua hiyo
itapunguza wanafunzi wa kike kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi kwa
sababu watakuwa na fedha za kujikimu. “Lengo la warsha hii ni kutoa
elimu na ushauri kwa wanafunzi wa jinsi zote ili waweze kusoma vizuri na
kuacha ushawishi wa kujihusisha na uhusiano wa kimapenzi. Pia,
tunawashauri hata wale ambao wapo katika ndoa wavumilie na kuepuka
kupata ujauzito ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao,” alisema
Katunzi.
Mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo hicho
Gosbeth Kihanga ambaye alikiri kuwapo kwa vishawishi chuoni hapo na
kudai kuwa inachangiwa na ugumu wa maisha hasa kwa wanafunzi wa kike.
Alisema kupitia kongamano hilo wamejifunza na
kuelewa mengi hususani katika suala la kupanga na kugawana majukumu,
kubadilisha mtazamo na kuacha kutumia ubabe katika uhusiano wa mapenzi.
Post a Comment