Dodoma. Waziri wa Fedha, Saada Mkuya amesema, Serikali itabadilisha kanuni kwa malengo mahususi ya kudhibiti misamaha ya kodi.
Waziri Mkuya alisema hayo bungeni jana alipokuwa
akijibu hoja zilizowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC), Zitto Kabwe kuhusu Ripoti ya Ukaguzi Maalumu wa
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Alisema Serikali itapitia misamaha ili kuhakikisha ile isiyokuwa na tija inaondolewa.
Akizungumzia suala la wafanyakazi wa Mamlaka
Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kujilipa posho za safari kiasi
kikubwa, Mkuya alisema walikuwa wakijilipa tangu Septemba mwaka 2009
bila kupata kibali cha Msajili wa Hazina kitu ambacho ni kinyume na
utaratibu.
“Hivi sasa tunaidhinisha sisi wenyewe na mashirika yote ya umma yanatakiwa kupata kibali cha Msajili wa Hazina,” alisema.
Waziri Mkuya alisema ili kuhakikisha kunakuwapo na
ufanisi katika hilo, watendaji wote wa Msajili Hazina wataondolewa
kwenye bodi za mashirika ambako ni wajumbe ili kusiwe na mwingiliano wa
kimasilahi.
Kuhusu tatizo la mtaji katika Benki ya Taifa ya
Biashara (NBC), alisema Serikali inalishughulikia na kwamba italipa deni
la Sh22.5 bilioni zilizoelezwa na kamati.
Kuhusu deni la mashirika ya hifadhi za jamii
ambalo Serikali inadaiwa, Waziri Mkuya alisema Serikali ina mpango wa
kuuza bondi zake ili iweze kulipa deni hilo lakini akasema hiyo itakuwa
baada ya kupeleka waraka wa kusudio hilo kwenye Baraza la Mawaziri.
Serikali za Mitaa
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia akijibu hoja za Kamati ya Hesabu za
Serikali za Mitaa (LAAC) alisema hatua mbalimbali zimechukuliwa katika
mikataba ambayo haina masilahi kwa halmashauri.
Pia, alisema ili kudhibiti ununuzi usiozingatia
sheria katika halmashauri, Serikali imeandaa mafunzo kwa wanunuzi wote
ili wajue Sheria za Ununuzi na wale wasiozingatia watachukuliwa hatua.
Alisema kutokana na matatizo katika halmashauri
mbalimbali nchini, Serikali imewavua madaraka wakurugenzi 21,
wakurugenzi watano wamefikishwa mahakamani, 27 wamepewa onyo, pia
watumishi 233 wamefukuzwa kazi na 277 wamefikishwa mahakamani, huku 10
kesi zao zimekwisha na wengine wamefungwa na wengine kulipa faini.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment