Zitto awavaa TRA, akerwa na Misamaha ya kodi

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema misamaha ya kodi imepanda kutoka Sh1.4 trilioni mwaka 2012/13 hadi Sh1.8 trilioni mwaka 2013/14, kueleza kuwa chanzo ni misamaha ya kodi katika miradi mikubwa.
Imesema kati ya misamaha hiyo, Sh 676 bilioni zinatokana na misamaha ya kodi inayotokana na Ongezeko la Thamani (VAT) na kufafanua kuwa hali hiyo itapungua iwapo nchi itaanza kutumia Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Pia, imefafanua kuwa mpaka sasa wafanyabiashara na kampuni kubwa zimefungua kesi katika mahakama ya rufaa wakipinga  kulipa kodi ambayo inafikia Sh1.7 trilioni.
Akizungumza katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa Mapato, Richard Bade alisema, “Kuna ongezeko la Sh400 bilioni. Kuongezeka kwa misamaha hii kunatuathiri kwa kiasi kikubwa.”
Alisema chanzo cha kuongezeka kwa kiwango hicho kunachangiwa na misamaha ya kodi katika miradi mikubwa kama ujenzi wa barabara, miradi ya gesi na mafuta na ujenzi wa daraja la Kigamboni.
“Katika miradi hiyo kuna misamaha ya zaidi ya Sh300 bilioni. Pia katika Sh1.8 trilioni kuna misamaha ya VAT ya Sh 676 bilioni na suala hili limefanyiwa kazi katika sheria mpya ya VAT,” alisema.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe alishangazwa na kitendo cha sheria hiyo kutotumika licha ya kuwa ilipitishwa na Bunge, jambo ambalo linasababisha Serikali kukosa mapato.
“Kamati ya PAC italiwasilisha suala hili kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa ajili ya hatua zaidi. Nadhani kutotumika kwa sheria hii kuna watu nyuma yake ambao wananufaika na misamaha hii,” alisema Zitto.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post