Maaskari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakimzika mwenzao aliyeuawa na maiti yake kutupwa katika eneo la jeshi.
Na Shomari Binda, Musoma/UwaziAskari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kikosi cha 27 Makoko kilichopo Musoma, MT 78227, Wirfred Koko, ameuawa kisha maiti yake kutupwa katika eneo la jeshi ikiwa imenyofolewa viganja na mguu mmoja, huku ikiwa katika sare za jeshi.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi mkoani Mara, juu ya kifo hicho ilisema askari huyo aliokotwa katika eneo la JWTZ Januari 30 mchana huku mwili wake ukiwa hauna baadhi ya viungo ukiwemo mguu wa kulia pamoja na viganja.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ernest Kimola, aliliambia gazeti hili kuwa, upande wa mguu wa kushoto wa marehemu ulikutwa na jeraha lililokatwa na kitu chenye ncha kali hali inayoashiria kuwa aliuawa na kutupwa kwenye eneo hilo.
“Baada ya kupata taarifa hizo askari polisi walifika eneo la tukio na kuchukua mwili wa askari huyo kwa ajili ya taratibu nyingine. Natoa wito kwa wananchi watakaokuwa na taarifa juu ya tukio hili kutoa taarifa kwa jeshi la polisi ili zifuatiliwe, sisi tunachunguza tukio hili,” alisema kamanda huyo.
Mwili wa marehemu Wirfred Koko ukiwa kwenye jeneza.
Kufuatia kifo hicho ambacho hakijulikani kilitokea lini, familia ya
mwanajeshi huyo imeviomba vyombo vya dola kufuatilia kwa kina na kuwapa
taarifa sahihi juu ya mauaji hayo ya ndugu yao.Wakizungumza na Uwazi katika Kijiji cha Kiabakari wilayani Butiama, mkoani Mara nyumbani kwao askari huyo, mmoja wa ndugu wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Bakari Koko, alisema baada kupata taarifa za kifo cha utata cha ndugu yao na kumaliza taratibu za mazishi, hawajapewa taarifa sahihi za kuwajulisha nini na nani aliyemuua askari huyo na wanashindwa kupewa ushirikiano na vyombo vya dola vinavyochunguza kifo hicho.
Aliongeza kuwa mara ya mwisho ndugu yao aliondoka nyumbani kwenda kazini jeshini na hakuweza kuonekana tena hadi alipokutwa amefariki dunia karibu na kituo chake cha kazi. “Mimi ni mdogo wake marehemu, nimesikitishwa na mauaji haya ya ndugu yangu aliyekuwa mlinzi wa nchi tena basi maiti yake ikiwa haina viganja wala mguu,” alisema Bakari.
Alisema ndugu yao ambaye ameacha mjane na watoto wawili, alikuwa akitoa msaada wa hali na mali na mawazo ndani ya familia na kifo chake kimekuwa ni pigo ambalo haliwezi kuzibika.
Post a Comment