Bibi kizee aanguka akiwa anasafiri angani


Na Kadama Malunde, Shinyanga
KATIKA hali ya kushangaza, bibi kizee anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (70), asiyejulikana jina wala makazi yake, ameanguka akiwa uchi wa mnyama nyumbani kwa Suzana Mwandu, mkazi wa Mtaa wa Mageuzi mkoani Shinyanga.
Tukio hilo lilitokea juzi ambapo bibi huyo baada ya kuanguka alianza kutembelea makalio bila kuzungumza chochote jambo ambalo limedaiwa ni ushirikina.
Akielezea tukio hilo jana, Mwandu alisema lilitokea nje ya nyumba ambapo alishangazwa kumkuta kikongwe huyo akiwa amelala huku akiwa uchi wa mnyama.
Mwandu alisema baada ya kikongwe huyo kuanguka, alijivuta hadi kwenye jiko lake lililoko nje ya nyumba ambalo lipo wazina baada ya kuanza kumsemesha ndipo akazinduka na kuanza kuongea maneno yasiyoeleweka, hali ambayo ilimtia wasiwasi na kutoa taarifa kwa uongozi wa Serikali ya Mtaa.
“Nyumba yangu nimeizindika vilivyo, hivyo kikongwe huyu alipokuwa katika safari zake na kupita maeneo ya nyumbani kwangu ndipo akakutana na balaa hilo na hatimaye akajikuta ameanguka na kuingia jikoni kwa ajili ya kujificha.

“Unajua siku zote mchawi anapoanguka na ukimwacha kwa muda mrefu bila ya kumsemesha, anaweza kupoteza maisha, hivyo kutokana na mimi kutokuwa na ubaya naye, nikaona bora nimsemeshe ili kumwokoa na baada ya hapo nikampa nguo za kujistiri na aibu ya kuwa mtupu,” alisema Mwandu.
Kwa upande wao mashuhuda wa tukio hilo, walidai kuwa bibi huyo huenda akawa ni mchawi kutokana na kauli zake tatanishi alizokuwa akizitoa huku mikono yake ikionekana kukatwa kwa mapanga na kuota sugu.

“Huyu bibi atakuwa mchawi, angalia hata mikono yake imekatwa katwa na imekomaa kweli, huenda huwa anajigeuza fisi na kutembelea mikono, halafu macho yake siyo ya kawaida, ana kiburi kupita kiasi na ndiyo tabia za wachawi wengi,”alieleza Halima Juma.
Hata hivyo, bibi huyo alifanya kituko kwa kuanza kutoa frdha za noti na sarafu alizokuwa amezihifadhi kiunoni kwa kutumia kitambaa cheusi huku akizirusha juu na katika hali ya kushangaza alipata nguvu na kuinuka.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mageuzi, Waziri Mussa (Chadema), alikiri kuwepo kwa tukio hilo ambalo lilijaza umati wa watu, huku wakishindwa kumtambua kikongwe huyo alikotokea na alikokuwa akielekea.
Alisema wakati wakiendelea kumuhoji na kumpa uji, alipata fahamu na wakati huo huo polisi walikuwa wamekwishafika na hivyo kumnusuru bibi huyo kushambuliwa na wananchi waliokuwa na hasira.
Hata hivyo, askari hao walishindwa kwenda naye kituoni kwa kile walichodai kwamba Serikali haiamini uchawi na kumruhusu bibi huyo kuendelea na safari yake.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Longunus Tibishubwamu, alithibitisha kutokea tukio hilo

Post a Comment

Previous Post Next Post