KATIBA: Kura ya Maoni hakuna-Lissu

Dodoma. Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema Kura ya Maoni kwa ajili ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa haitaendeshwa bila kuifanyia marekebisho sheria inayoongoza mchakato huo.
Lissu, ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki, alisema hayo jana wakati akiwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) mjini hapa.
Kura ya Maoni ilipangwa kufanyika Aprili 30 lakini ikaahirishwa kwa muda usiojulikana kutokana na kasi ndogo ya uandikishaji wapigakura, lakini Lissu aliliambia Bunge jana baada ya kuahirishwa kuwa hakuna uwezekano wa kura hiyo kupigwa bila ya kufanyia marekebisho Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013.
Vikao vinavyoendelea mjini Dodoma ni vya mwisho kwa Bunge la 10 lililochaguliwa mwaka 2010 na iwapo Serikali haitawasilisha muswada wa marekebisho ya sheria hiyo, Kura ya Maoni haitafanyika mwaka huu, kwa mujibu wa Lissu.
“Kwa kifupi Mheshimiwa Spika, hakuna uwezekano kisheria wa kurudia tena hatua zozote muhimu ambazo zilikwishachukuliwa kwa ajili ya kufanyika kwa Kura ya Maoni iliyokuwa imepangwa Aprili 30, 2015,” alisema Lissu. 
“Mpaka sasa Serikali hii ya CCM haijawasilisha muswada wowote wa marekebisho ya sheria hiyo ili kuwezesha kufanyika kwa kura ya maoni siku za usoni.
“Kama ilivyokuwa kwa ahadi ya Kura ya Maoni ya Aprili 30,  Serikali hii ya CCM inadanganya Watanzania kuwa kutakuwa na Kura ya Maoni wakati kila mwenye akili timamu anajua hilo haliwezekani bila kwanza kuwa na mazingira wezeshi ya kisheria.”
Akiwasilisha hotuba ya upinzani, Lissu alisema kila hatua inayotakiwa kuchukuliwa, haiwezekani kuahirishwa wala kuongezewa muda kama ilivyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Serikali.
Lissu alisema kitendo cha kutofuata muda uliowekwa katika sheria hiyo, kinaiondolea sheria hiyo uhalali wa kuendelea kutumika.
Lissu, ambaye ni wakili wa kujitegemea, alisema ndani ya siku 14 tangu tarehe ya kupokea Katiba Inayopendekezwa, Rais alitakiwa kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar, kuielekeza Tume ya Uchaguzi kwa amri iliyotangazwa katika Gazeti la Serikali kuendesha Kura ya Maoni.
Alisema amri ya Kura ya Maoni inatakiwa kufafanua kipindi cha kampeni na kipindi ambacho kura hiyo inatakiwa kufanyika.
“Rais Kikwete alikwishatoa amri kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Kura ya Maoni, lakini hana mamlaka yoyote, kwa mujibu wa sheria hii, ya kutengua amri yake au kutoa amri mpya ili kuwezesha kura ya maoni kufanyika kwa tarehe nyingine tofauti na tarehe iliyotangazwa kwenye amri ya  kwanza,” alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post