Dar/mikoani. Nchi imesimama. Hii ndiyo sentensi inayofaa
kuelezea tukio la jana la mgomo wa madereva nchini kote ambao kwa mara
ya kwanza ulisababisha mabasi yote kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani
na nchi jirani kushindwa kuondoka.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT), kushindwa kutoa huduma kwa sababu yoyote ile.
Tangu asubuhi hadi jioni, hakuna basi hata moja
lililotoka wala kuingia katika kituo hicho hadi abiria walipoanza kukata
tamaa na baadhi yao kuondoka na wengine kuanza kushinikiza kurejeshewa
nauli.
Mgomo huo ambao ni mwendelezo wa ule uliofanyika
Aprili 9, mwaka huu ulipewa uzito na madereva hao baada ya ahadi
walizopewa na Serikali kutofanyiwa kazi kama ilivyoahidiwa na Waziri wa
Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka.
Tofauti na wa awali, safari hii mpaka inatimu saa
11.00 jioni hakuna kiongozi yeyote aliyejitokeza katika kituo hicho
kusikiliza kilio cha madereva hao.
Hata hivyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameunda
kamati ya iliyotangazwa na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta ya kusimamia
usafiri barabarani itakayowakutanisha wadau wote ili kutatua matatizo
katika sekta hiyo kila yanapotokea.
Polisi wachemsha Dar
Tangu saa 2.30 asubuhi, polisi walijaribu
kuyasindikiza mabasi waliyodhani madereva wake wako tayari kuondoka
Ubungo lakini walishindwa baada ya kutoungwa mkono.
Mkuu wa Trafiki Ubungo, Inspekta Yussuf Kamotta
akiwa na Inspekta Solomon Nkindwa ambaye pia ni mkaguzi wa magari,
waliingia katika basi la Kampuni ya Master City na kuliondoa kituoni
hapo wakiwa na mmiliki wa kampuni hiyo, Abdallah Mohammed huku
wakimtafuta dereva bila mafanikio na kulazimika kulitafutia sehemu
salama ya kuliegesha baada ya madereva kulizingira.
Kitendo cha askari hao kilisababisha kuzomewa kwa
Inspekta Nkindwa wakisema mkaguzi huyo arudi shule akasome...
“Solomoooon… rudi shuuuule… gia nane… zimekushinda,” walisikika madereva
hao wakiimba huku wakikimbia mchakamchaka kurudi zilipo ofisi zao.
Kutokana na vurugu zilizotokea nje ya kituo hicho,
polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu
waliokuwa katika makundi.
Nje ya UBT, magari sita ya polisi yaliegeshwa
katika makutano ya barabara za Sam Nujoma, Nelson Mandela na Morogoro
wakati mengine yakielekea Mwenge na Buguruni kwenda kukabiliana na
tishio lolote ambalo lingeweza kutokea.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment