Ufisadi huu sasa kiama

Dodoma. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amewasilisha ripoti tano za ukaguzi wa fedha kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2014 akibainisha ufisadi wa zaidi ya Sh600 bilioni katika maeneo mbalimbali na matumizi ya fedha ambayo hayana maelezo ya kutosha.
Ukaguzi huo ulifanywa katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, mashirika ya umma, miradi ya maendeleo na ufanisi wa maeneo mbalimbali.
Ripoti hizo zinaonyesha jinsi watumishi hewa wa umma wanavyoendelea kulipwa mishahara, wakiwamo wa balozi za Tanzania waliostaafu, misamaha ya kodi na ukiukwaji wa ununuzi na matumizi yasiyoeleweka ya fedha katika Wizara ya Ujenzi na Kitengo cha Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Amina Mwidau na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Rajab Mbaruk Mohamed walizichambua ripoti hizo na kueleza jinsi watumishi wa Serikali wanavyotafuna mabilioni ya fedha.
Akizungumzia ripoti hiyo katika mkutano wa pamoja na CAG, Mwidau alisema imeonyesha jinsi Sh285 bilioni za Kitengo cha Maafa zilivyotafunwa licha ya kuwa zilitengwa kwa ajili ya kufanya shughuli maalumu.
Kuhusu Wizara ya Ujenzi, alisema ililidanganya Bunge baada ya kueleza kuwa Sh262 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara, kitu ambacho kimebainika kuwa siyo kweli.
“Ukaguzi unaonyesha kuwa fedha hizo zimetumika katika mambo mengine kabisa, yaani zimetumika tofauti na hakuna maelezo ya kuridhisha,” alisema Mwidau huku akifafanua kuwa wizara hiyo inadaiwa na makandarasi Sh800 bilioni.
Misamaha ya kodi
Profesa Assad alisema ofisi yake ilibaini kasoro katika mfumo wa ufuatiliaji wa misamaha ya kodi na kusababisha ukiukaji wa matumizi iliyotolewa kwa mafuta yanayotumika migodini.
Alisema mafuta yenye kodi ya Sh22.33 bilioni yaliyotakiwa kutumiwa na kampuni zilizosamehewa kodi, Geita Gold Mine na Resolute TZ Ltd, yalipelekwa kwa makandarasi wasiostahili msamaha na kusababisha hasara ya Sh22.33 bilioni,” alisema.
Alisema pia misamaha ya kodi kwa malengo tofauti na yaliyokusudiwa, ilitolewa na kusababisha upotevu wa Sh392.7 milioni katika Kampuni ya Kiliwarrior Expeditions Ltd ya Arusha iliyokuwa imesamehewa kodi Sh465.2 ili kuingiza magari 28.
Hata hivyo, alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kati ya hizo kukusanya Sh72.5 milioni.(Mwananchi)

Post a Comment

Previous Post Next Post