Bunge la Sudan limepiga kura na kuitangaza Sudan Kusini kuwa adui wa nchi hiyo


Bunge la Sudan limepiga kura na kuitangaza Sudan Kusini kuwa adui wa nchi hiyo, ni baada ya majeshi ya Sudan Kusini wiki iliyopita kutwaa eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Shambulio la Jumanne wiki iliyopita katika eneo la mafuta la Heglig, lenye umuhimu mkubwa kwa uchumi wa Sudan Khartoum, limesababisha kufungwa kwa shughuli za uzalishaji wa mafuta.
Spika wa bunge la Sudan, amesema nchi yake itatumia kila raslimali iliyonayo kupambana na Sudan Kusini.
Afisa wa Sudan katika ubalozi wa Sudan mjini London, Dr Kalid Mubarak, alisema kuwa sio nchi yake pekee inayolaani vitendo vya Sudan Kusini.
Afisa huyo anasema jamii yote ya kimataifa inailaumu Sudan Kusini kwa uchokozi wake.
Sudan kusini imekuwa ikiilaumu Sudan kwa kushambulia maeneo yake.
Mwandishi wa BBC aliye Khartoum James Copnall anasema kuwa kufuatia tangazo hilo kuna hatari ya nchi hizo mbili kuingia katika vita.
Hatua ya bunge la Sudan ya kupiga kura ya kuitangaza Sudan Kusini kama adui inakuja wakati msemaji wa umoja wa mataifa akithibitisha kuwa ndege za Sudan zimekuwa zikishambulia kambi za maaskari wa kulinda amani zilizoko maeno ya Sudan Kusini.

Post a Comment

Previous Post Next Post