MAONI
YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YAMAENDELEO YA JAMII KUHUSU MUSWADA WA
MAREKEBISHO YA SHERIA ZA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII, 2012 (THE SOCIAL
SECURITY LAWS (AMENDMENTS) ACT), 2012
UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika, Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007, Kanuni
ya 86 (5), naomba kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu, maoni ya
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kuhusu Muswada wa
Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, 2012 (The Social
Security Laws (Amendments) Act), 2012.
Mheshimiwa
Spika, Kamati ilipata nafasi ya kujadili Muswada huu katika vikao
vilivyofanyika katika Ofisi ndogo ya Bunge Dar es Salaam. Katika kikao
cha kwanza kilichofanyika tarehe 27/03/2012, Naibu Waziri wa Wizara ya
Kazi na Ajira Mheshimiwa Dkt. Milton M. Mahanga, Mb alitoa maelezo ya
jumla yanayohusu madhumuni ya Muswada. Kikao hiki pia kiliwashirikisha
wadau mbalimbali miongoni mwao wakiwemo:-
1. Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi -TUCTA
2. Chama cha Waajiri Tanzania -ATE
3. Chuo Kikuu Mzumbe
4. Tanzania Higher Learning Instution Trade Union - THTU
5. Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa- LAPF
6. Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma- PSPF
7. Mfuka wa Taifa wa Bima ya Afya- NHIF
8. Mfuko wa Pensheni kwa Mashirika ya Umma- PPF
9. Mfuko wa Akiba kwa Watumishi wa Serikali- GEPF
10. Mfuko wa Hifadhi za Jamii – NSSF
11. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu- LHRC
Mheshimiwa
Spika, kwa namna ya pekee Kamati inawashukuru wadau wote walioshiriki
na kutoa maoni ambayo yamezingatiwa na Kamati katika kuishauri Serikali
ili iyazingatie katika Jedwali la marekebisho.
Mheshimiwa
Spika, vikao vingine vilifanyika terehe 03/04/2012, tarehe 04/04/2012,
tarehe 11/04/2012 na tarehe 12/04/2012 ambapo Waziri Kazi na Ajira
pamoja na Mwakilishi kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu walifafanua na
kutoa majibu ya baadhi ya hoja zilizokuwa zimejitokeza.
Mheshimiwa
Spika, Muswada huu unakusudia kufanya marekebisho katika Sheria za
Hifadhi za Jamii kwa madhumuni ya kuiwezesha Mamlaka ya Usimamizi na
Udhibiti wa Hifadhi za Jamii kufanya kazi yake ya kusimamia na kudhibiti
Sekta ya Hifadhi ya Jamii kikamilifu.
Mheshimiwa
Spika, Muswada huu umegawanyika katika Sehemu Kuu Nane ambazo Kamati
imezifanyia kazi na kutoa mapendekezo ya kuziboresha na hatimae kuwa na
Sheria inayofaa kwa mazingira ya nchi yetu.
SEHEMU YA KWANZA
Mheshimiwa
Spika, Sehemu hii inaelezea jina la Muswada na maudhui yanayofanya
kupendekeza kutungwa kwa Sheria hii. Kamati haikuwa na tatizo lolote
katika sehemu hii na imekubali mapendekezo ya Sheria hii kuanza kutumika
tarehe 1 Juni 2012, kama yalivyoletwa mbele ya Kamati katika jedwali la
marekebisho.
SEHEMU YA PILI
Mheshimiwa
Spika, Sehemu hii inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya
Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa, Sura 407 (The Local Authorities
Pensions Fund, Act, Cap.407).
Mheshimiwa
Spika, Baada ya kupitia sehemu hii kwa makini, Kamati inashauri
marekebisho yafuatayo yafanyike ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa
Sheria hii.
(i)
Kifungu cha 2 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa
Serikali za Mitaa ambacho hakikuletwa kwenye marekebisho haya,
kirekebishwe ili kuruhusu mfuko kusajili wanachama kutoka katika sekta
rasmi na isiyo rasmi kama ilivyofanyika katika Muswada huu kifungu cha
79 cha Sheria ya Mfuko wa Mashirika ya Umma na kifungu cha 120 cha
Sheria ya Mafao ya Hitimisho la Utumishi wa Umma.
(ii)
Kifungu cha 4 cha Muswada kinachofanya marekebisho
kwenye kifungu cha 3 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za
Mitaa, tafsiri ya neno “employee” haijitoshelezi hivyo, iongezwe tafsiri
iliyopo katika kifungu cha 61 cha Sheria ya Taasisi za Kazi (Labour
Institutions Act, 2004) ili kupanua tafsiri ya nani ni mfanyakazi na
hivyo kupanua wigo wa wafanyakazi wengi zaidi kujiunga na mifuko ya
hifadhi ya jamii. Aidha, marekebisho haya yafanyike sehemu zote ambapo
neno ‘employee’ limetafsiriwa katika Muswada huu.
Aidha,
Kamati inashauri tafsiri ya neno actuarial valuation iwe moja katika
mifuko yote kuliko ilivyo sasa ambapo kila mfuko una tafsiri yake.
(iii)
Kifungu cha 7 cha Muswada kinakusudia kufanya
marekebisho katika kifungu cha 8 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa
Serikali za Mitaa kwa kuongeza kifungu kipya cha (3) ambacho kinaelezea
muda wa Mkurugenzi Mtendaji kushika ofisi kwamba ni kipindi cha miaka
mitano na anaweza kuongezewa miaka mingine mitano kama itaonekana
inafaa. Kamati inashauri neno ‘shall’ lililopo kwenye mstari wa pili
lifutwe na badala yake liandikwe neno ‘may’ ili uteuzi wake kwa mara ya
pili utegemee utendaji wake wa kazi kwa kuzingatia Sheria zilizopo sasa
na Mkataba wa ajira.
Marekebisho
haya yafanyike pia kwenye vifungu vya Muswada vya 32, 42, 85, 129 na
144 ambavyo vinahusu uteuzi wa wakurugenzi wa Mifuko yote ya Hifadhi za
Jamii.
(iv)
Kifungu cha 13 cha Muswada kinachofanya marekebisho katika
kifungu cha 27 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa kwa
kuongeza kifungu kipya cha 27A kinachoongelea kuhusu kutoa ‘bonus’ kwa
mtumishi ambaye amefikisha umri wa miaka sitini na anaendelea kuchangia
kwenye Mfuko, Kamati imeona kifungu hiki ni kizuri na ni vema
ikaangaliwa namna ya kuingizwa katika mifuko yote ya hifadhi ya jamii.
Aidha,
Kifungu cha 28 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa
ambacho katika Muswada huu hakijafanyiwa marekebisho kifanyiwe
marekebisho kwa kufuta maneno “commuted pension” yaliyopo kwenye kifungu
1; na kuongeza maneno “subject to subsection (1)” mwanzoni mwa kifungu
cha 2 na kuacha neno ‘gratuity’ ambayo ndiyo anayotakiwa kupewa
mwanachama anayekufa akiwa kazini lakini amechangia kwa kipindi chini ya
miezi 180.
(v)
Kifungu cha 18 cha Muswada ambacho kinafanya marekebisho
katika kifungu cha 38 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za
Mitaa, kuwezesha mfuko kurudisha fedha ambazo mwanachama atakuwa
amezidishiwa (overpaid). Kamati inashauri kifungu hiki pia kizungumzie
suala la mwanachama kupunjwa (underpaid) iwapo litajitokeza. Aidha,
kutokana na mwanachama kupunjwa, Kamati inapendekeza Mfuko kulipa mafao
yote ya mwanachama pamoja na penult ya asilimia mbili (2%) ya mafao yote
ya mwanachama.
(vi)
Kifungu cha 19 cha Muswada kimefanya marekebisho machache
ya kifungu cha 39 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa,
Kamati inakubaliana na Kifungu hiki kwakuwa kinamruhusu mwanachama
aliyeacha kuchangia kwa kipindi fulani kurejea. Vilevile, kitamsaidia
mwanachama kupata mafao yake kana kwamba hakuwa ameacha kuchangia.
(vii)
Kifungu cha 21 cha Muswada kinachofanya marekebisho kwenye
kifungu cha 49 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa,
ambacho kinaongelea kuhusu mfuko kuwekeza fedha za wanachama, Kamati
inashauri kwamba ni vema sasa mfuko kuanza kuwafaidisha wanachama
kutokana na uwekezaji huo kuliko hivi sasa mfuko kuwekeza katika
biashara mbalimbali hasa za ujenzi lakini faida kwa mwanachama
haionekani.
(viii)
Kifungu cha 28 cha Muswada kinachofanya marekebisho kwenye
jedwali la kwanza, ambacho kinaongelea kuhusu muundo wa Bodi, Kamati
hairidhishwi na Bodi kuwa na uwakilishi wa wajumbe saba tu. Kwa mujibu
wa maelezo ya Serikali kuwa idadi hiyo imetokana na suala zima la kutaka
kupunguza gharama za uendeshaji. Kamati inashauri badala ya kupunguza
idadi ni vema suala la malipo ya wajumbe liangaliwe upya.
Aidha,
Kamati inashauri idadi ya Wajumbe iwe ni kuanzia wajumbe saba hadi tisa
kulingana na ukubwa wa mifuko ili kuwa na uwakilishi mzuri wa waajiri,
wafanyakazi na wataalam. Aidha, marekebisho haya yafanyike kwenye muundo
wa bodi zote za mifuko ya hifadhi za jamii.
Vilevile
katika kifungu kidogo cha (e) yaongezwe maneno “members representing
the most representative employers association” ili uwakilishi utoke kwa
chama chenye wanachama wengi kwa mujibu wa Mkataba wa Shirika la Kazi
Duniani (ILO). Marekebisho haya pia yafanyike katika Kifungu cha 76(1)
(b), Kifungu cha 118 (1) (c) na 136 (1) (f).
(ix)
Kifungu cha 31 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali
za Mitaa, kinachozungumzia kuhusu maslahi ya mwanachama kujitoa kwenye
mfuko kwa sababu ya ndoa au uzazi, hakijafanyiwa marekebisho, Kamati
inapendekeza kifanyiwe marekebisho ili kutoruhusu wanachama wanawake
kujitoa kwenye uanachama kwa sababu ya ndoa au uzazi ili kwenda sambamba
na dhana nzima ya hifadhi ya jamii.
(x)
Kifungu cha 37 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa
Serikali za Mitaa hakijafanyiwa marekebisho, Kamati inapendekeza kufanya
marekebisho ili kuwezesha wastaafu kuwa na uhuru wa kuchagua kulipwa
kwa mkupuo (lump sum) iwapo haitazidi asilimia 50 (50%) ya akiba na riba
yake na asilimia 50 (50%) inayosalia alipwe kwenye malipo ya kila
mwezi.
SEHEMU YA TATU
Mheshimiwa
Spika, Sehemu hii inakusudia kufanya marekebisho katika Sheria ya Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya, Sura 395 (The National Health Insurance Fund,
Cap.395). Katika kuchambua na kupitia sehemu hii, Kamati inashauri,
Kifungu cha 38 cha Muswada kinachokusudia kufanya marekebisho ya kifungu
cha 43 cha Sheria ya Mfuko wa Taifa Bima ya Afya kwa kuongeza kifungu
kipya cha (3), maneno yafuatayo yanamakosa ya kiuchapaji, neno ‘instate’
lifutwe badala yake liandikwe ‘instituted’ na neno ‘concert’ lifutwe
badala yake liandikwe ‘consent’.
Mheshimiwa Spika, katika mabadiliko ya Sheria hii, Kamati haikuona kama kunahitajika marekebisho makubwa zaidi.
SEHEMU YA NNE
Mheshimiwa
Spika, Sehemu hii inakusudia kufanya marekebisho katika Sheria ya Mfuko
wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, Sura ya 50 (The National Security Fund,
Cap.50). Kamati inapendekeza yafuatayo:-
(i)
Kifungu cha 48 cha Muswada kinaandika
upya kifungu cha 18 cha Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii,
kwanza, Kamati inapendekeza kifungu cha 18 (1) kisitaje (Order Number
XXXV), kwa vile (Order Number XXXV) inaweza kubadilika wakati wowote na
hivyo kulazimu kurudi tena Bungeni kufanya marekebisho. Aidha,
marekebisho haya yafanyike popote ilipotajwa (Order Number XXXV).
Pili,
kifungu cha 18 (2) ambacho kinalazimisha Mfuko kupata idhini ya
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) kabla ya kufungua mashtaka ya jinai,
Kamati inashauri ili kuharakisha usikilizaji wa kesi za aina hii, DPP
apewe mamlaka ya kuteua mtu atakayesimamia mashtaka haya kwa niaba yake.
(ii)
Kifungu cha 68 cha Muswada kinachoandika
upya kifungu cha 74 cha Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii,
Kamati inapendekeza kifungu kidogo cha (1) na (2) neno ‘may’ lisomeke
‘shall’ ili kuweka uzito katika jambo hili.
(iii)
Kifungu cha 72 cha Muswada kinachorekebisha kifungu cha
82(3) cha Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii inapendekeza
maneno ‘a’ au ‘any’ yaongezwe baada ya neno ‘where’ ili kuondoa utata.
SEHEMU YA TANO
Mheshimiwa
Spika, Sehemu hii inakusudia kufanya marekebisho katika Sheria ya Mfuko
wa Mashirika ya Umma, Sura 372 (The Parastatal Organisations Pensions
Scheme, Cap.372). Kamati inapendekeza yafuatayo:-
(i)
Kifungu cha 80 cha Muswada ambacho kinatoa tafsiri ya
maneno mbalimbali yaliyotumika katika Sheria hii, Kamati inashauri
maneno ‘actuarial valuation’ na ‘actuary’ yaliyopo mwishoni mwa ukurasa
44 wa Muswada yafutwe kwakuwa yameshatolewa tafsriri katika kifungu cha
80 (a).
Vilevile neno ‘member’ lililopo katika ukurasa wa 45 lifutwe kwakuwa limetolewa tafsiri katika ukurasa wa 46.
(ii)
Kifungu cha 86 cha Muswada ambacho kinakusudia kufanya
marekebisho katika kifungu cha 8 cha Sheria ya Mfuko wa Mashirika ya
Umma, pamoja na marekebisho yaliyopendekezwa katika Muswada, Kamati
inapendekeza kuongezwe marekebisho mengine ya kumlazimisha mwajiri
yeyote atakayekuwa amemwajiri raia wa kigeni kupeleka michango yake
kwenye mifuko ya hifadhi za jamii. Marekebisho haya yafanyike pia kwenye
mifuko yote ya hifadhi jamii.
(iii)
Kifungu cha 5 cha Sheria ya Mfuko wa Mashirika ya Umma
ambacho kwenye Muswada huu hakijafanyiwa marekebisho, Kamati inashauri
kifungu hiki pia kifanyiwe marekebisho ili kuruhusu wanachama ambao
watakoma kuwa wanachama kwa sababu yoyote ile wakiwa hawajatimiza umri
wa kustaafu, endapo wataajiriwa tena waruhusiwe kuwa wanachama.
(iv)
Kifungu cha 21(4) cha Sheria ya Mfuko wa Mashirika ya Umma
ambacho kwenye Muswada huu hakijafanyiwa marekebisho, Kamati
inapendekeza kifanyiwe marekebisho kwa kukifuta kwakuwa marekebisho
yaliyofanyika mwaka 2001 kwa Sheria Na.25 yaliondoa neno ‘National
Insurance Corporation’ na kuweka neno ‘Fund’ kwakuwa kwa sasa hakutoweza
kuwa na mgogoro kwani bodi na mfuko ni kitu kimoja.
SEHEMU YA SITA
Mheshimiwa
Spika, Sehemu hii inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya
Mafao ya Hitimisho la Utumishi wa Umma, Sura 317 (The Public Service
Retirement Benefit Act, Cap.371. Kamati inashauri, Kifungu cha 123 cha
Muswada kinachofanya marekebisho kwenye kifungu cha 6 cha Sheria ya
Mafao ya Hitimisho la Utumishi wa Umma kwa kukiandika upya, Kamati
inashauri kuwa kifungu hiki kirekebishwe kwakuwa kimekwenda kinyume na
kifungu cha 25 cha Sheria Na.8 ya mwaka 2008, ambacho kimeipa Mamlaka
jukumu la kuweka viwango vya kuchangia na sio Bodi kama ilivyoandikwa
kwenye Muswada.
SEHEMU YA SABA
Mheshimiwa
Spika, Sehemu hii inakusudia kufanya marekebisho katika Sheria ya
Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Sura 135 (The Social
Security (Regulatory Authority) Cap.135. Kamati inashauri yafuatayo
yafanyiwe marekebisho;-
(i)
Kifungu cha 142 (b) cha Muswasda
kinachokusudia kufanya marekebisho katika kifungu 7 cha Sheria ya
Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kufuta kifungu
kidogo cha (f) ambacho kinamwondoa mtaalamu wa masuala ya hifadhi ya
jamii kuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi. Kamati inashauri kifungu hiki
kisiondolewe kwani mjumbe huyu ni mwakilishi muhimu sana katika Bodi
hii, ili kuisaidia masuala ya kitaalam yatakayokuwa yanaamuliwa na Bodi.
Vilevile,
kifungu cha 142 (c) cha Muswada kinachokusudia kuongeza kifungu kipya
cha 3 kwa kumfanya Mkurugenzi Mkuu kuwa Katibu wa Bodi, Kamati
imekubaliana na maelezo ya Wizara kwamba huo ndio utaratibu kwa
mashirika yote lakini ili kutenganisha jukumu la usimamizi na utendaji,
Kamati inashauri kifungu hiki kitamke wazi kabisa kuwa Mkurugenzi huyu
hatakuwa na haki ya kupiga kura kama ilivyowekwa kwenye kifungu cha
118(b) cha Muswada huu ambacho kinafanya marekebisho katika kifungu cha 6
cha Sheria ya Mfuko wa Mashirika ya Umma.
(ii)
Kifungu cha 147 cha Muswada kinachofanya
marekebisho katika kifungu cha 38 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kwa kuongeza Kifungu cha 38A (2) a, Kamati
inashauri Mwenyekiti wa Kamati hii awe ni afisa wa Serikali aliyestaafu
au mtu yeyote ambaye hafungamani na upande wowote.
Vilevile
katika Kifungu cha 38A.-(2) (d) neno ‘Commissioner for Labour’ lifutwe
kwa kuwa kwa mujibu wa Sheria za Kazi hakuna cheo hicho badala yake
liandikwe ‘Labour Commissioner’.
Aidha,
Kifungu cha 38A.-(2) (e), Kamati inashauri kuwa idadi ya wawakilishi
kutoka uwakilishi wa vyama vya wafanyakazi iongezwe kutoka mtu mmoja na
kuwa watu wawili.
Vilevile
Kamati inashauri kiongezwe kifungu (f) ili kuweka uwakilishi wa waajiri
kwani dhana ya msingi ya utekelezaji wa Sheria hii inazingatia zaidi
masuala ya utatu.
(iii)
Kifungu cha 148 cha Muswada kinachokusudia kufanya
marekebisho katika kifungu cha 47 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti
wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kukifuta na kukiandika upya, Kamati
inashauri ni vema kifungu cha zamani kikabaki kama kilivyo kwavile
kinaendana na kifungu cha 48 ambacho kinaipa Benki mamlaka ya udhibiti
na sio ushauri kama inavyofanywa na mabadiliko haya.
(iv)
Kifungu cha 150 ambacho kinafanya marekebisho katika
kifungu cha 49 cha Sheria Na.8 ya mwaka 2008 kwa kuongeza kifungu kipya
cha 49A ili mamlaka iweze kutoza tozo kwa mifuko ya hifadhi ya jamii na
pia kuwekeza kwenye hisa (share) na dhamana (securities).
Mheshimiwa
Spika, Kifungu cha 49A.-(1)na (2), kwanza, Muswada haukueleza tozo
kusudiwa litatoka wapi. Baada ya maelezo ya Serikali kuwa tozo
inayopendekezwa litatokana na punguzo la fungu la fedha za matumizi ya
kiutawala (administrative costs) kwenye mifuko husika na bila kuathiri
michango ya wananchama, Kamati inakubaliana na marekebisho haya ya
Serikali kuhusiana na dhana nzima ya tozo ili kuiwezesha mamlaka kuweza
kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Pili,
Muswada unapendekeza Waziri akishirikiana na Waziri wa Fedha na Benki
ya Tanzania kuamua kiwango cha tozo kwa kutangaza kwenye Gazeti la
Serikali bila kuwashirikisha wadau. Kamati inashauri kifungu hiki
kifanyiwe marekebisho ili kumlazimisha Waziri kisheria kushirikisha
wadau.
Tatu,
kifungu cha 49A.-(5) kinachohusiana na suala la Mamlaka kupewa uwezo wa
kuwekeza kwenye hisa na dhamana. Kamati inapendekeza kuwa kifungu hiki
kifutwe kwa vile kinakwenda kinyume na lengo kuu la kuanzishwa kwa
mamlaka na majukumu yake kama yalivyoorodheshwa kwenye kifungu cha 5 cha
Sheria ya Na. 8 ya mwaka 2008 ambapo jukumu hili halipo kwa Mamlaka ya
Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Pia kuiruhusu Mamlaka kuingia
kwenye uwekezaji, itakuwa inaingilia shughuli zinazofanywa na Mifuko
ambayo Mamlaka ndiye mdhibiti.
SEHEMU YA NANE
Sehemu
hii inakusudia kufanya marekebisho katika Sheria ya Bima, Sura ya 394
(The Insurance Act, Cap.394). Kamati imepitia sehemu hii na haikuwa na
tatizo hivyo inakubaliana na mapendekezo yaliyoletwa na Serikali.
MAONI YA JUMLA
Pamoja
na kutoa mapendekezo ya jumla ya Muswada, Kamati ina maoni mengine ya
ziada kwa ajili ya utekelezaji bora wa Sheria za Hifadhi ya Jamii kwa
manufaa ya wanachama wake.
(i)
Kwakuwa mchakato wa kuiweka mifuko ya
Hifadhi za Jamii chini ya Wizara moja ni wa muda mrefu na inasisitizwa
pia na Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii, Kamati haikuona sababu kwa
nini marekebisho ya Muswada huu hayakuja na pendekezo la kisheria la
kuiwajibisha mifuko kuwa chini ya Wizara moja. Kamati inashauri ili kuwa
na uendeshaji bora wa mifuko ya Hifadhi za Jamii, ni wakati muafaka
sasa Mifuko hii ikawajibika chini ya Wizara Kazi na Ajira, tofauti na
sasa ambapo mifuko iko katika Wizara mbalimbali.
Aidha,
kwakuwa Kamati inapendekeza mifuko yote ya hifadhi ya jamii kuwajibika
chini ya Wizara yenye dhamana ya Hifadhi ya Jamii ambayo kwa sasa ni
Wizara ya Kazi na Ajira, ni vema ikaanzishwa Idara maalum ndani ya
Wizara itakayoshughulika na Hifadhi ya Jamii ili kuweza kusimamia
utekelezaji wa shughuli hizi katika ngazi ya Wizara kwa vile kwa sasa
Idara hiyo haipo.
Vilevile
inapendekezwa kifungu cha 5(1)(e), (f) na (i) cha Sheria Na.8 ya mwaka
2008 kinachoelezea majukumu ya Mamlaka kifanyiwe marekebisho ili
majukumu haya yafanywe na Wizara ya Kazi na Ajira chini ya Idara
inayopendekezwa ya Hifadhi ya Jamii kwa sababu ni ya kisera zaidi na sio
la kiutendaji. Hii ni kutokana na ukweli kwamba jukumu kuu la mamlaka
ni kudhibiti mifuko ya hifadhi ya jamii, masuala ya kisera ya jinsi ya
kuiboresha sekta hii ni ya Wizara.
(ii)
Kwakuwa fomula ya ukokotoaji wa mafao ya
mwezi ni tatizo kwani kila mfuko una utaratibu wake hivyo kusababisha
viwango vya pensheni kutofautiana kwa kiwango kikubwa. Kamati inashauri
Mamlaka (SSRA) iliangalie suala fomula kwa kina na kwakuzingatia
yafuatayo:-
kiasi cha juu cha miaka ambayo mtumishi ametumikia,
muda wa kuishi baada ya kustaafu (commuting factor),
mshahara wa mwisho aliostaafu nao,
pensheni irekebishwe kutokana na mporomoko wa thamani ya fedha na mfumuko wa bei
uzingatie kipindi mtumishi alichokuwa kazini katika sehemu mbalimbali.
kiwango cha pensheni kisipungue asilimia 70 ya pato la mtu kutokana na ngazi yake.
(iii)
Kwakuwa Kifungu cha 30 cha Sheria Na.8 ya mwaka 2008
kinatoa uhuru wa watumishi wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza au ambao
hawajaandikishwa katika mifuko ya Hifadhi ya Jamii kujiunga na mfuko
wowote wa hifadhi ya jamii, Kamati inashauri waajiri wote nchini kuwapa
nafasi watumishi wao kuchagua mifuko wanayotaka kujiunga nayo kuliko
ilivyo sasa ambapo mbali na kuwepo kwa kifungu hiki bado watumishi wengi
hawana uelewa na hawaeleweshwi kama kuna uhuru huo.
Aidha,
kwa vile sasa mifuko imeruhusiwa kupata wanachama kutoka sekta
isiyorasmi basi ni vema Mifuko ikajiandaa vyema kwa kuwawekea mazingira
mazuri ambayo yatawanufaisha.
(iv)
Vilevile, suala la mwanachama kuruhusiwa kuhamia mfuko
mwingine liruhusiwe na lisiathiri mafao yake, jumla ya vipindi
alivyochangia ndiyo vitumike.
(v)
Pamoja na kwamba mifuko imeruhusiwa kuwekeza lakini mpaka sasa
Kamati haijaona faida inayokwenda kwa wanachama kutokana na uwekezaji
mkubwa unaofanywa na mifuko hii. Hivyo basi, Kamati inashauri ni wakati
muafaka sasa mifuko kujielekeza zaidi katika kuboresha maslahi ya
wanachama wake kutokana na uwekezaji huo.
(vi)
Iwapo Muswada huu utapita na kuwa Sheria, Kamati inapendekeza ni
vema marekebisho yote haya yakachapishwa na kuingizwa kwenye Sheria
husika na kutolewa upya ili kuondoa usumbufu wa kusoma sheria Mama na
mabadiliko haya. Hii itasaidia uelewa wa wanachama na wadau.
(vii)
Kwa vile ripoti za tathmini ya afya ya kifedha ya mifuko
(actuarial reports) hupelekwa kwenye Bodi za Mifuko husika, Kamati
inashauri Wajumbe wa Bodi waone wajibu wa kuwajulisha wanachama wao juu
ya ripoti hizo ili wajue hali halisi ya mifuko yao.
(viii)
Mafao ya kifo yanayotolewa kwa sasa kwa wategemezi, Kamati
inashauri yaendelee mpaka mjane au mgane afariki na mpaka wategemezi
watakapofikisha umri wa kujitegemea.
(ix)
Kwa kuwa mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na.102,
umeorodhesha mafao tisa ambayo mwanachama anapaswa kupewa, Kamati
inashauri kuwa ni vyema mifuko kujielekeza kwenye kutekeleza mkataba huo
na vigezo vya ushindani viwe ni mafao ya ziada.
Aidha,
fao la tiba ambalo lipo kwenye mkataba huo wa kazi, inashauriwa
litolewe kwa wastaafu wote ambao walikuwa wanachama wa mifuko ya hifadhi
ya jamii.
(x)
Utaratibu wa sasa ambapo watumishi waliopo kwenye
mkataba mara wamalizapo muda wao kulipwa pensheni na wakati huo huo
kuongezewa mkataba mwingine. Kamati inaona utaratibu huu unaliingizia
Taifa hasara na inapendekeza mtumishi akiongezewa Mkataba asilipwe
kiinua mgongo mpaka pale atakapomaliza muda alioongezewa.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaishukuru Serikali kwani mapendekezo mengi ya Kamati yamezingatiwa katika Jedwali la Marekebisho.
MWISHO
Mheshimiwa
Spika, Kamati inaamini kuwa, Muswada huu umebeba maoni mengi ya wadau,
na bila shaka utakapokuwa Sheria kamili, Kamati inaishauri Serikali,
Kanuni zitakazotungwa zizingatie maoni ya Wadau na endapo kuna maeneo
yanayohitaji marekebisho, Serikali isisite kuleta mabadiliko mbele ya
Bunge hili.
Mheshimiwa
Spika, Kwa niaba ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii naomba
kukushukuru wewe binafsi kwa kunipatia nafasi ya kuwasilisha maoni ya
Kamati yangu, pia namshukuru Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge.
Aidha ninapenda kumshukuru Mheshimiwa Gaudentia Mugosi Kabaka, (Mb)
Waziri wa Kazi na Ajira, Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Milton Makongoro
Mahanga, (Mb) na wataalam wa Wizara wakiongozwa na Katibu Mkuu Ndugu
Eric Francis Shitindi kwa ushirikiano walioipatia Kamati.
Mheshimiwa
Spika, Kwa namna ya pekee naomba niwashukuru wajumbe wa Kamati ya
Maendeleo ya Jamii kwa michango na mapendekezo yaliyoboresha muswada
huu. Ninapenda kuwatambua Wajumbe wa Kamati hii kwa majina:-
1. Mhe. Jenista Joakim Mhagama, Mb, Mwenyekiti
2. Mhe. Juma Selemani Nkamia, Mb M/Mwenyekiti
3. Mhe. John Damian Komba, Mb Mjumbe
4. Mhe. Mch. Dkt. Getrude P. Rwakatare, Mb “
5. Mhe. Agnes Elias Hokororo, Mb, “
6. Mhe. Fatuma Abdallah Mikidadi, Mb “
7. Mhe. Mary Pius Chatanda, Mb “
8. Mhe. Moza Abedi Saidy, Mb “
9. Mhe. Donald Kevin Max, Mb “
10.Mhe. Joseph Osmund Mbilinyi, Mb “
11.Mhe. Hamad Ali Hamadi, Mb “
12. Mhe. Abdallah Sharia Ameir, Mb “
13. Mhe. Salum Khalfan Barwany, Mb “
14. Mhe. Mariam Salum Msabaha, Mb “
15. Mhe. Assumpter Nshunju Mshama, Mb “
16. Mhe. Asha Mohamed Omari, Mb “
17. Mhe. Ramadhani Haji Salehe, Mb “
18. Mhe. Rebecca Michael Mngodo, Mb “
19. Mhe. Said Mohamed Mtanda, Mb “
20. Mhe. Abdallah Haji Ally, Mb “
21. Mhe. Hussein Mussa Mzee, Mb “
22. Mhe. Livingstone Joseph Lusinde, Mb, “
Mheshimiwa
Spika, namshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilillah na Ofisi yake
kwa kuiwezesha Kamati wakati wote ilipokuwa inatekeleza majukumu yake.
Vilevile makatibu wa Kamati Ndugu Hosiana John na Ndugu Asia Minja kwa
kuratibu kazi za Kamati.
Mheshimiwa Spika, Naunga mkono Muswada na naomba kuwasilisha
Jenista Joakim Mhagama, Mb
MWENYEKITI
KAMATI YA MAENDELEO YA JAMII
13 Aprili, 2012

Post a Comment