WANANCHI
wa kitongoji cha Tazara kilichopo katika kijiji cha Mbalizi mkoani
Mbeya wamemtaka askari wa jeshi la wananchi (JWTZ) kikosi cha 44 Karume
Camp, Chacha Mwita, ahame makazi yake na kurudi kambini kwa madai kuwa
askari huyo amekuwa akitishia usalama wa wao kila kuchwapo.
Hayo
waliyasema bayana katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya
Tazara wiki iliyopita baada ya uongozi kuitisha mkutano huo ili
kujadili mahusiano mabaya yaliyokuwepo baina ya askari huyo na raia
anaoishi nao mtaani hapo.
Mkutano
huo uliokuwa chini ya Mkuu wa upelelezi mkoa wa Mbeya Elias Mwita
(RCO) ambaye alihudhuria baada ya kupokea malalamiko ofisini kwake
kwamba hali ya usalama katika eneo hilo si shwari kutokana na msigano
uliopo.
Mkuu
huyo aliwaambia wananchi kuwa mapema mwezi huu alipokea ugeni ofisini
kwake ulioongozwa na Mwanajeshi Chacha ukiimtuhumu Benson Mwakilembe
(Tall) kwamba anawanyanyasa wananchi wa eneo hilo na kwamba wananchi
waliowengi hawamtaki mwananchi huyo.
Alisema
Chacha aliongozana na wenzake ambao aliwataja kwa majina kuwa ni
Cosmas Maluli na Mchungaji wa kanisa la EAGT usharika wa Galilaya Ayub
Mwasiposya ambao wote walikuwa wakimtuhumu Mwakilembe kuwa hana
mahusiano mazuri na wananchi wa eneo hilo.
Mwita
alisema baada ya kuelezwa hivyo aliona ni vema afike kuwasikiliza
wakazi wote wa mtaa huo badala ya kuwasikiliza watu wachache waliofika
ofisini kwake.
Mchungaji
Mwasiposya alisimamishwa na kuwa wa kwanza kujieleza katika mkutano
huo ambapo alikiri kufika ofisini kwa Mwita lakini kwa shinikizo la
Chacha aliyemdanganya kwamba wakapatane na Mwakilembe kufuatia tofauti
zao hapo awali.
Mchungaji
huyo alikanywa katika mkutano huo kutumia vizuri mahubiri yake ambayo
baadhi ya wakazi wamekuwa wakiyalalamikia kwa madai kwamba amekuwa
akiipotosha jamii kutokana na kuongelea habari za kishirikina ambazo
aliwahi kuzielekeza kwa Mwakilembe na akakamatwa kwa kushindwa
kuthibitisha kasha akasamehewa
Sababu
zilizopelekea wananchi kumtaka mkuu wa upelelezi amhamishe Chacha
kwenye mtaa huo mbali ya vitisho pia walidai kwamba ni mchochezi na
anatumia vibaya kazi yake kwa raia kitendo ambacho walikifafanua kuwa
analichafua jeshi hilo lenye heshima kubwa barani Afrika na dunia kwa
ujumla.
Walisema
amekuwa na tabia ya kuwapeleka watu katika kituo kidogo cha polisi cha
Mbalizi bila makosa na kuzuia sungusungu kufanya kazi yake pia amewahi
kuomba rushwa ya sh.100,000 ili kumwachia kijana mmoja ambaye
alimtuhumu kumwibia kuku wawili madai ambayo walisema hayakuwa ya
kweli.
Hata
hivyo mkuu huyo wa upelelezi alisema kuwa mtanzania anahaki ya kuishi
mahali popote kwa mujibu wa taratibu za serikali lakini pia alifafanua
kuwa kwa kuwa Chacha ni mtumishi wa serikali atafanya mawasiliano na
viongozi wake ili kuliweka sawa suala la kumtaka Chacha arudi kambini na
akasema kuwa Chacha aache kutumia jina lake kutafuta umaarufu.
Tuhuma
hizo zilitolewa katika mkutano huo ambao pia Chacha alipewa fursa ya
kujieleza mbele ya mkuu wa upelelezi na alikiri kupeleka malalamiko
hayo kwa mkuu huyo wa upelelezi kitendo ambacho kiliibua hasira kwa
wananchi na kumtaka asiendelee kujieleza.
Awali
Chacha ndiye aliyeuthibitishia mkutano kwa kumtuhumu kijana mmoja
ambaye hakumtaja jina kwamba alimkamata akiwa na kuku wawili wa wizi
lakini kauli hiyo ilimgeuka baada ya mama mmoja kusimama na kuueleza
umma kuwa, malalamiko ya Chacha kuibiwa kuku hayakuwa ya kweli kwani
aliliunda tukio na kutumia vitisho vya uaskari ili kujipatia kiasi hicho
cha pesa.
Kwa hisani ya Gordon Kalulunga wa Mbeya Yetu blog
|
Post a Comment