TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod
Slaa amehitimisha ziara ya siku 10 ya kujenga chama na kukagua uhai wa
chama katika mikoa mitano, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Geita na Mwanza,
ambako katika maeneo mbalimbali alikopita amesimamia vikao vya
kiutendaji ambavyo vimelazimika kuchukua maamuzi mazito na muhimu dhidi
ya watu waliobainika kuhujumu maendeleo ya wananchi, kukihujumu chama,
kuvunja katiba, kanuni na taratibu za CHADEMA.
Moja
ya maamuzi hayo mazito ni kuvuliwa kwa uanachama kwa aliyekuwa Diwani
wa Kata ya Katoro, Gervas Daudi, kufutwa uongozi wa BAVICHA Geita,
kuvuliwa uanachama baadhi ya viongozi na wanachama ambao baada ya
kuhojiwa na vikao walibainika pasi na shaka kuwa wamekuwa wakihujumu
chama hivyo kukwaza matumaini ya wananchi kwa CHADEMA, kuwa chama
mbadala nchini. Watu hao waliovuliwa uanachama watalazimika kusubiri
maamuzi zaidi ya Kamati Kuu inayotarajiwa kuketi hivi karibuni, ili
kujua hatma yao ndani ya CHADEMA.
Akiwa
katika vikao hivyo vilivyofanya maamuzi hayo mazito, Katibu Mkuu Dkt.
Slaa alilazimika kutoa kauli kali akisema kuwa chama hakitakubali kulea
viongozi wasiowajibika kwa watu, akisisitiza kuwa kama kuna kiongozi
yeyote hawezi kuendana na kasi ya mahitaji ya chama hicho katika
kuwatumikia watu, anapaswa kupisha mara moja badala ya kukwaza juhudi
hizo.
“Viongozi
wangu naomba mtambue, chama hiki si mali ya mtu, wala si chama cha
viongozi, ni chama cha wananchi, ni chama cha watu, ni chama cha
Watanzania. Hiki si chama cha kukaa siku nzima kutatua migogoro, ni
chama cha kutafakari suluhisho la matatizo mbalimbali yanayowakabili
Watanzania. Chadema ni tumaini pekee la Watanzania kwa sasa.
“Hatutavumilia
ufisadi, hatutavumilia uzembe, hatutakubali viongozi wanaojali maslahi
yao badala ya wananchi, katika hili CHADEMA tutakuwa wakali kwa yeyote
hata kama angekuwa ni katibu mkuu, hatuwezi kujifungia kuzungumzia
migogoro inayosababishwa na ubinafsi wa watu badala ya kutumia muda huu
kuzungumzia kero na maendeleo ya watu,” amesisitiza Dkt. Slaa katika
ziara hiyo.
Katika
ziara hiyo iliyoanzia Nzega, mkoani Tabora, Aprili 13 na kumalizikia
Jijini Mwanza Aprili 22, 2012, Katibu Mkuu Dkt. Slaa kupitia vikao hivyo
vya kimaamuzi amelazimika pia kutoa kauli kali dhidi ya viongozi na
wanachama wanaoonekana kukwaza jitihada za CHADEMA katika kuwatumikia
watu, akisema kuwa chama hiki ndiyo tumaini pekee lililobaki kwa
Watanzania katika harakati za ukombozi wa awamu ya pili, kutafuta
mabadiliko ya kimfumo na kiutawala nchini kwa ajili ya maendeleo ya
watu.
Wilayani
Nzega, kikao cha kiutendaji kiliwavua uongozi aliyekuwa Mwenyekiti wa
Jimbo, Tito Onesmo kutokana na kupata nafasi hiyo kinyume cha utaratibu
na Katibu Mwenezi, Shaaban Mohamed kwa kosa la kughushi barua. Wote
walipewa karipio kali na kutakiwa kuandika barua ya maelezo kwa nini
wasichukuliwe hatua kali zaidi. Mohamed baada ya kubanwa na kukosa
utetezi wa makosa yake, aliamua kurejesha kadi ya uanachama mbele ya
kikao hicho.
Katika
Wilaya ya Bariadi, Katibu Mkuu alifutilia mbali kile kilichoitwa
uongozi wa Mkoa wa Simiyu kwani kwa taratibu za chama mkoa huo bado
haupo, hivyo uchaguzi ulikuwa batili tangu mwanzo.
Viongozi
wa Wilaya ya Bariadi waliohusika katika kuitisha uchaguzi huo, akiwemo
Mwenyekiti Mwenyekiti wa Wilaya Limbu Ntalima, Katibu wake Elias Maduka
Kaselabantu na Mwenyekiti wa Vijana wa Wilaya, Khamis Rajab, na Bwana
Kube Kube aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mkoa, walipewa onyo kali,
kuwekwa chini ya uangalizi maalum kwa kipindi cha miezi 12, kuangalia
mwenendo wao ndani ya chama, huku pia Kube akitakiwa kuandika barua
ndani ya siku 30 kueleza kwa nini alikuwa nyuma ya suala hilo.
Mbali
ya kufutilia mbali uongozi huo, kikao hicho kiliwaondoa madarakani
viongozi wa wilaya waliochukua madaraka isivyohalali aliyekuwa
Mwenyekiti wa Wilaya Limbu Ntalima, Katibu wake Elias Maduka Kaselabantu
na Mwenyekiti wa Vijana wa Wilaya, Khamis Rajab kwa kukiuka katiba ya
chama na kukihujumu katika uchaguzi mdogo wa kutafuta Diwani wa Kata ya
Legangabilili, ambapo CHADEMA ilikuwa ikipewa asilimia kubwa ya kuibuka
mshindi.
Viongozi
hao waliomba radhi na kuahidi mbele ya kikao kuwa mara moja watakwenda
kufuta kesi waliyofungua mahakamani kuhoji uhalali wa Kamati Maalum
(task force) iliyoundwa kwa ajili ya kuongoza chama wilayani Bariadi kwa
muda.
Katika
Wilaya ya Kahama, Baraza la Mashauriano lilikubaliana kwa kauli moja
Charles Dotto Lubala, Anastazia Kanyanda na Justine Mganga wavuliwe
uanachama, huku wenzao 12 wakiwekwa chini ya uangalizi maalum kwa kosa
la kusababisha mgogoro ndani ya chama wilayani humo, hali iliyosababisha
chama kushindwa kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi katika maeneo
mbalimbali kama vile ngazi ya vitongoji, vijiji na kata ambako wananchi
waliichagua CHADEMA kuwatumikia.
Katika
Jimbo la Busanda, Mkutano Mkuu wa Jimbo uliamua kwa sauti moja, baada
ya kupiga kura, kumuachisha uanachama aliyekuwa Diwani wa Kata ya
Katoro, Gervas Daudi, akikabiliwa na tuhuma kadhaa ikiwemo kukihujumu
chama hicho. Ngazi husika za chama zitawasilisha taarifa ya maamuzi
husika kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kwa mujibu wa katiba na kanuni za
chama.
Mbele
ya kikao hicho, Daudi alituhumiwa kukihujumu chama hicho kwa kuzuia
uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Katoro ambayo inaongozwa na Chadema
kutekeleza ilani ya chama hicho katika kuwaletea maendeleo wananchi wa
eneo hilo, hasa katika kusimamia rasilimali za wanakijiji, huku
akishiriki vikao vya kuizushia tuhuma za kutengeneza.
Alituhumiwa
kuzuia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa
sekondari, kituo cha magari na urekebishaji wa mikataba mibovu ya
upangaji wa vibanda vya biashara mali ya kijiji hicho ambayo iliingiwa
wakati wa uongozi wa CCM katika Serikali ya Kijiji cha Katoro kabla ya
uchaguzi uliokiondoa madarakani chama hicho katika eneo hilo.
Tuhuma
zingine ni kuwachangisha fedha wananchi 9 kiasi cha shilingi laki 5
kinyume na taratibu, akiwaahidi kuwatoa waume zao ambao wanashikiliwa
mahabusu wakituhumiwa kwa kosa la mauaji, pia alituhumiwa kushiriki
vikao na wafanyabiashara, viongozi na wanachama wa CCM wakipanga
kuipindua serikali ya kijiji hicho na pia kuwapindua viongozi wengine wa
vitongoji wanaotokana na CHADEMA.
Daudi
pia amesimamishwa nafasi zake zingine ndani ya chama hicho, ikiwemo
Uenezi Jimbo la Busanda, Uenyekiti Wilaya ya Geita, ambapo Kamati
Tendaji ya Wilaya ya Geita imeagizwa kukaa haraka kuteua mtu atakayeziba
nafasi ya Daudi kisha jina hilo litumwe na kujadiliwa Kamati Kuu ya
chama hicho inayotarajiwa kuketi hivi karibuni.
Halikadhalika
katika Wilaya ya Geita, Baraza la Mashauriano kwa kauli moja, baada ya
kupiga kura lilifikia uamuzi wa kuvuliwa uanachama kwa viongozi wa
Baraza la Vijana (BAVICHA); aliyekuwa Mwenyekiti wa BAVICHA Jimbo la
Geita, Emmanuel Otto, Katibu wake, Vincent Paul na Mratibu wa
Uhamasishaji Philibert Msiba. Pia uongozi mzima wa baraza hilo ngazi ya
jimbo uliondolewa. Diwani wa Marceline Simbasana aliandikiwa barua ya
karipio kali kwa mwenendo wake kinyume na taratibu za chama.
Baraza
la Mashauriano katika Wilaya ya Sengerema liliamua kwa kauli moja
kuvunja Baraza la Uongozi la Wilaya, pia uongozi wa Mabaraza yote, yaani
BAVICHA, BAWACHA na Baraza la Wazee katika majimbo mawili ya Buchosa na
Sengerema ulivunjwa baada ya kuonekana haukidhi mahitaji ya kikatiba,
kanuni na taratibu za chama.
Halikadhalika
uongozi wa CHADEMA Jimbo la Sengerema wote ulivunjwa, ambapo
ilikubaliwa kuwa viongozi wote waliohusika katika kuvunja katiba, kanuni
na taratibu katika kusimamia shughuli za chama ikiwemo kuwafukuza
wenzao uanachama wasihusike katika mchakato wa kujaza nafasi za uongozi
wakati uchaguzi wa kukaimisha na pia katika uchaguzi wa ndani
unaotarajiwa kuanza hivi karibuni na kukamilika mwaka 2013.
Katibu
Mkuu, Dkt. Slaa amesema kuwa hatarudi nyuma katika kuendesha ‘safisha
safisha’ hiyo kwani akiwa Mtendaji Mkuu wa chama anatekeleza azimio la
Kamati Kuu iliyoazimia kuwa ofisi yake ifanye uhakiki wa uongozi na
utendaji wa chama ili kujenga chama na kukagua uhai wa chama kuanzia
ngazi ya chini, Msingi mpaka juu.
Imetolewa leo Aprili 26, 2012, Dar es Salaam na;
Tumaini Makene
Afisa Habari wa CHADEMA

Post a Comment