TAMKO LA CHADEMA-MAREKANI KUHUSU KUUAWA KWA WANA-CHADEMA


TAMKO LA WANACHAMA WA CHADEMA MAREKANI KUHUSU MATUKIO YA KUUAWA KWA WANACHAMA NA WAPENZI WA CHADEMA.
Kumekuwa na mfululizo wa matukio ya kinyama ya kuuawa kwa Wanachama, Viongozi na wapenzi wa CHADEMA hasa katika vipindi vya chaguzi.
Matukio yote haya hutokea kwenye vipindi vua chaguzi ndogo au baada ya chaguzi hizo. Kuna taarifa kwamba katika baadhi ya Matukio jeshi la Polisi hutaarifiwa lakini hawachukui hatua zozote stahiki kulinda Usalama wa Raia hosusani wanachama wa CHADEMA kama Raia wengine.
Kutokana na mfululizo wa matukio haya ni dhahiri kabisa kuna mpango wa kutaka kuwatisha Raia wapenda haki wasifanye maamuzi ya Kidemokrasia kwa kushirki katika chaguzi hizo kwa kujazwa hofu kutokana na Matukio haya yanayojili.
Kila mara kunapotokea matukio haya Jeshi la Polisi huishia kusema kuwa wanafanya Uchunguzi kujua nani wanahusika na kufanya Matukio haya ya kinyama pasipo kutoa taarifa zozote kwa wananchi wala kuonyesha jitihada zozote za kuwakamata wahusika; Matokeo yake uchunguzi wa matukio hayo ukiwa hauna mafanikio yeyote ya kuwakamata na kuwafungulia mashtaka wahusika.
Kutokana na hali hiyo wananchi wengi wamekuwa hawana Imani na jeshi la polisi kwani hakuna hata tukio moja kati ya matukio ya mauaji ya kinyama  yaliyokuwa na mafanikio ya kuwakamata wahusika.
Kuna sababu nyingi za kuhusisha matukio haya na masuala ya kisiasa kwa sababu ya Mazingira ya matukio haya jinsi yanavyotokea. Kwanza yanalenga kwa wanachama, Viongozi na wapenzi wa CHADEMA tu. Naweza kutoa ushahidi kwa tukio lililotokea kwenye Uchaguzi Mdogo wa Igunga kwa kuuwawa kinyama kwa msimamizi wa kura wa CHADEMA aliyetekwa nyara na watu wasiojulikana hatimaye kukutwa porini akiwa ameuawa kinyama kwa kupigwa na vitu kama mawe na kumwagiwa tindikali.
Ushahidi wa pili ni wa lile tukio la kupigwa Mapanga kwa Wabunge wawili wa CHADEMA Mheshimiwa Silvestre Machemli na Mheshimiwa Hayness Kiwia kwenye Uchaguzi mdogo wa diwani wa Kirumba Mwanza. Siku ya tukio waheshimiwa hawa walipogundua kuwa wanafuatiliwa na watu waliowatilia mashaka walipiga simu Polisi kuomba msaada lakini kilichotokea Polisi walichelewa kufika sehemu ya tukio na hata walipofika waliwashuhudia waheshimiwa hawa wakiwa wamezungukwa na watu wasiojulikana na kupigwa mapanga bila hata Polisi kuchukua hatua zozote. Je, hili linaashiria nini? Kitendo cha Polisi kushuhudia Raia mwema tena Mbunge akiwa anapigwa mapanga mbele ya macho yao wasichukue hatua zozote?
Ushahidi wa tatu ni wa lile tukio lililotokea Arumeru la kupatikana miili ya watu wanne wanaosemekana kuuawa kwa kunyongwa na kutupwa karibu na shule moja ya Msingi huko Arumeru. Bila kusahau tukio la Mwanachama mmoja wa chadema aliyekamatwa na kutekwana watu wasiofahamika na kuteswa na kuachwa na majeruhi makubwa na kutupwa kando ya mto hatimaye kuokotwa na mpita njia.
Mfululizo wa matukio haya na mengne ya kupotea kwa kutekwa Wanachama na wapenzi wa CHADEMA ni ishara tosha kwamba kuna mpango ulioandaliwa wa kufanya uhalifu huu kwa Wanachama wa CHADEMA na Jeshi la Polisi linafahamu hilo.
Je, Watanzania Siasa ndio inatupeleka huko? Tuna vyombo mbalimbali vya ulinzi ikiwemo Idara ya Kijasusi (Usalama wa Taifa). Je, wanatoa mchango gani kuhusiana na matukio haya yanayoendelea?
Vyombo vya Usalama likiwemo jeshi la Polisi kumbukeni matukio haya yanawapata Watanzania wasio na hatia ambao ni Kaka zenu, wajomba zenu, dada zenu na Shangazi zenu. Kuyafumbia macho matukio haya itapelekea siku moja Wananchi watachukua Sheria mkononi na kusababisha machafuko makubwa ambayo yatasababisha umwagaji mkubwa wa damu wa kulipiza kisasi.
Watanzania hatuna utamaduni huo wala hatupendi yaliyotokea kwa jirani zetu wa Rwanda na Burundi yatokee hapa. Huko yalikuwa na masuala ya ukabila hapa yanaweza kuwa  masuala ya itikadi za Kisiasa.
Masuala ya kisiasa yamesababisha machafuko makubwa katika nchi za Kiarabu kama Tunisia, Misri, Yemen na sasa Syria.  Kwa kweli hatupendi hayo yatokee kwetu.
Kufumbia macho matukio hayo ni kujenga chuki kwa Wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi. Pia wananchi kuchukiana wenyewe kwa wenyewe kwa sababu za itikadi za kisiasa. Vyombo vya Ulinzi hususani Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama lazima wachukue hatua stahiki kukabiliana na matukio haya ya kinyama, vinginevyo tutarajie umwagaji mkubwa wa damu wa kulipiza kisasi.
WANACHAMA WA CHADEMA MAREKANI.

Post a Comment

Previous Post Next Post