KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willbroad Slaa, amesema harakati za kuendesha mchakato mzima wa ‘Vua
gamba, Vaa gwanda’ ni lazima zikiguse pia Chama cha Wananchi (CUF) kwa
vile kimeungana na CCM na kushindwa kutetea masilahi ya wananchi hususan
wakazi wa mikoa ya Mtwara na Lindi.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika Kata ya Mkanaledi mkoani Mtwara
jana, Dk. Slaa alisema tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka
1992, Chama cha CUF kilipata uungwaji mkono kwa kiasi kikubwa na wakazi
wa kusini hivyo kushindwa kutetea masilahi yao na kuungana na CCM ni
sawa na kuwaambia wananchi wajitafutie ukombozi mwingine.
“CUF tulikubaliana nao, kwakuwa wote ni wapinzani na wao wana nguvu
huku na maeneo ya pwani ni vema tukawaachia ili waendeleze jukumu la
kuwakomboa Watanzania,” alisema Dk. Slaa na kuongeza:
“Ndio sababu hatujawahi kuweka mgombea urais katika uchaguzi wowote
kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, lakini kitendo cha CUF kuungana na
CCM kimeonyesha dhahiri hawana nia ya kuwakomboa Watanzania,” alisema.
Dk. Slaa alisema wakati wa wakazi wa Mtwara, Lindi na maeneo mengine
kuendelea kunung’unika umepita na kinachotakiwa ni kuchukua maamuzi
magumu kwa kuikataa CCM na kujiunga na CHADEMA.
Akizungumzia rasilimali za mikoa ya kusini, Dk. Slaa alisema mikoa ya
Lindi na Mtwara inaongoza kwa kuzalisha zao la mihogo na korosho na
kama mazao hayo yangetumika vema yangesaidia kuleta maendeleo.
“Ninyi mna rasilimali za kutosha sasa kama gesi, mihogo na bandari hizi
zikitumika ipasavyo hakuna kati yenu atakayelalamikia huduma mbovu za serikali lakini hamna kinachofanyika,” alisema Dk. Slaa.
Alisema serikali haikuwa na nia ya kweli ya kuwasaidia wananchi ndiyo
maana ikaamua kuuza kiwanda cha kubangulia korosho kwa Mama Anna Mkapa
kwa shilingi milioni 50 huku wananchi wakiendelea kutaabika.
Chanzo:- Tanzania daima
Post a Comment