Marekani imekiri kuwa
mwanaharakati wa kijamii mwenye ulemavu wa kuona, raia wa Uchina , Chen
Guangcheng, anataka kuondoka nchini humo, suala ambalo limetishia
kusambaratisha mazungumzo kati ya nchi hizo mbili, yanayoendelea mjini
Beijing.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani
amesema ni dhahiri kuwa Bwana Chen na mkewe walikuwa wamebadili msimamo
wao, tangu walipoondoka kutoka ubalozi wa Marekani siku ya Jumatano.
Chen
aliiambia BBC kua alitaka kushauriana na maafisa wa kidiplomasia wa
Marekani, kuhusu mipango yake, lakini anaamini kuwa wanazuiliwa na
maafisa wa serikali ya Uchina kumuona hospitalini, ambako anaishi kwa
sasa.
Baada ya kutoroka kifungo cha nyumbani wiki
iliyopita, Bwana Chen alipewa hifadhi katika ubalozi wa Marekani hadi
siku ya Jumatano.
Suala hilo lingali linaangaziwa pakubwa na
vyombo vya habari kuliko mazungumzo kati ya maafisa wakuu wa serikali ya
Marekani na China.
Clinton azungumzia haki za kibinadam
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Bi Hillary
Clinton, yuko mjini Beijing kwa mazungumzo yanayoangazia Korea Kaskazini
na Syria.
Wakati mazungumzo hayo yalipoanza, Bi Clinton hakumtaja bwana Chen kwa jina, lakini aliangazia suala la haki za kibinadam.
Katika muda wa siku mbili zilizopita, kumekuwa
na habari za kuhitilafiana, hasa kuhusu sababu zilizomfanya Chen
kuondoka kutoka ubalozi wa Marekani na habari ambazo alikuwa amepewa.
Mapema hii leo Balozi wa Marekani nchini China,
Gary Locke, alipinga madai kuwa Bwana Chen alishurutishwa kuondoka
kutoka ubalozi wa wake.
Chanzo:- BBC Swahili
Post a Comment