Mkapa atoa siri ya mafanikio, Lema amvaa

 Mkapa atoa siri ya mafanikio, Lema amvaa
 .
RAIS Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ameeleza siri ya mafanikio ya uchumi na siasa ya Serikali yake, miaka kumi aliyokaa madarakani kuwa ni uwazi na ukweli katika mambo yote hata magumu yaliyoikabili Serikali.

Akizungumza kwenye mjadala maalumu kuhusu uwekezaji barani Afrika, ulioandaliwa na Taasisi ya Uwezeshaji na Uwekezaji (ICF), Mkapa aliyetambulika enzi zake kama Mzee wa uwazi na ukweli, alisema sera hiyo ilimsaidia kupata uungwaji mkono kutoka kwa umma ambao ulipewa fursa ya kujua mazuri na mabaya yaliyokuwa yakitokea na njia ya kukabiliana nayo.

“Uwazi na ukweli ulisaidia kuwapa wananchi taarifa sahihi kuhusu hali ya uchumi, fedha na changamoto zote zilizoikabili Serikali na wao kupata fursa ya kushiriki kuzitafutia ufumbuzi,” alisema Mkapa.
Alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni kuwawezesha kiuchumi wanawake na vijana ambao ndiyo idadi kubwa ya wananchi sehemu nyingi duniani.

Hata hivyo, wakati Mkapa akitamba kwa mafanikio hayo,  Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Goodless Lema, ‘amemvaa’  na kumtupia lawama kutokana na umaskini uliotopea Mtwara licha ya mkoa huo kuwa na utajiri wa kutisha.

Akihutubia mkutano wa hadhara Kijiji cha Mangamba, Kata ya Likonde, Wilaya ya Mtwara jana, Lema alisema Mkapa licha ya kuongoza taifa kwa miaka 10, alishindwa kuwawezesha wakazi wa mkoa huo kuondokana na umaskini. 

“Mkapa amekaa madarakani kwa miaka 10 lakini Mkoa wa Mtwara umeendelea kuongoza kwa umaskini nchini,” alisema Lema na kuongeza:

 “Leo nimepata jibu kwa nini Mkapa ameukimbia mkoa huu, hataki kuishi hapa, nimetembelea Kijiji cha Namayanga na kujionea umaskini unaotisha.”

Alisema wananchi wa Mtwara hawapaswi kuvitazama viashiria vya maendeleo kama majengo ya ghorofa yaliyopo Dar es Salaam, bali kuitazama hali yao ndani ya mkoa alikozaliwa Mkapa.Lema ambaye alikuwa Mbunge wa Arusha Mjini kabla ya ushindi wake kutenguliwa na mahakama, alisema kushindwa kwa Mkapa kufikia matarajio ya umma, kunaweza kutumika kama kigezo cha kumuombea dua mbaya.“Mkapa ameiongoza nchi hii kwa miaka 10 akiwa Rais, leo hii Mtwara ni aibu tupu watu wa hapa wanaishi katika nyumba za nyasi na udongo zinazotaka kudondoka, bila elimu wakitembea pekupeku na kushindwa hata kumudu kununua malapa ya Sh700,” alisema.

Alisema Mtwara ina rasilimali za asili kama bahari, gesi, ardhi yenye rutuba kwa kilimo cha korosho, mafuta na bandari yenye kina kirefu, lakini bado inakabiliwa na `umasikini wa kutupwa.’
Lema alisema kutokana na umaskini huo, Mkapa ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Lupaso, wilayani Masasi, ameamua kukimbia mkoa kwenda kuishi Lushoto, mkoani Tanga.

 Alisema hata wa watoto wao wameishia mitaani kufanyabiashara ndogo za korosho, maji, mitumba na nyinginezo zinazodhalilisha utu wa binadamu kutokana na kukimbia maisha magumu mkoani humo.
“Leo hii Machinga kila mahali, hili ni zao la wanaMtwara kutokana na kupumbazwa kielimu hawataki watoto wenu wasome waweze kufunguka akili zao na kudai haki,” alisema.

Alisema badala yake watawala wanawanyonya haki zao ikiwamo kuwakopa wakulima wa korosho, hivyo kusababisha mzunguko mdogo wa fedha.

Alisema kama mzunguko huo ungekuwapo, wakulima wangeweza kuwalipia watoto mahitaji yao kama ada za shule, lakini kwa vile hilo halifanyiki, wamebaki kuwa mbumbumbu na kutawalika kwa rahisi.
Aliwataka wakazi hao kuachana na CCM kutokana na kuendelea kuwapumbaza kwa zaidi ya miaka 50 na kujiunga  na Chadema kupigania mabadiliko ya nchi.

Katika hatua nyingine, Lema alisema ataandaa maandamano makubwa mjini Arusha kutaka watu wote waliomo magerezani mkoani humo wanaokabiliwa na kesi mbalimbali za wizi wa kuku, sigara, ubakaji, ujambazi na wahalifu wote kuachiwa huru iwapo Serikali ya CCM haitawafikisha mahakamani mawaziri waliojiuzulu wanaodaiwa kutafuna zaidi ya Sh9 bilioni za umma.

 “Haiwezekani hawa wezi wa mabilioni ya shilingi waishie kujiuzulu, huku maskini ambao wengi wamefungwa kwa kesi za wizi wa kuku na wengine kufungwa kwa kusingiziwa... nao waachiwe huru kama walivyoachiwa mawaziri

Post a Comment

Previous Post Next Post