SERIKALI YAKABIDHI TSH. MIL 10 ZA RAMBI RAMBI KWA MAMA MZAZI WA MAREHEMU STEVEN KANUMA
SERIKALI imekabidhi sh. milioni 10 kwa
mama mzazi wa aliyekuwa nguli wa filamu nchini, Steven Kanumba, Frola
Mtegoa kama rambi rambi ya msiba huo.
Akizungumza wakati akikabidhi fedha hizo
nyumbani kwa marehemu, Kanumba, Naibu Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Amos Makalla alisema Serikali inatambua mchango wa
Kanumba katika tasnia ya sanaa ya filamu na maigizo hapa nchini.
Alisema kifo chake kimeipa Serikali
changamoto kubwa ya kuhakikisha inalinda na kusimamia vyema kazi za
wasanii, hivyo mchakato huo utaenda kwa kasi sana.
"Kifo chake ni changamoto kubwa kwetu
hivyo kutokana na cheo changu nitahakikisha naipeleka kasi mchakato wa
kulinda kazi za wasanii ili ifike mahala kila msanii aridhike na
anachokipata, kwani marehemu Kanumba aliigiza filamu nyingi lakini
hakupata mafanikio kama ilivyotakiwa" alisema Makala.
Alisema Serikali kwa kushirikiana vema na
Kamati ya mazishi iliyokuwa ikiongozwa na Gabriel Mtitu, wametoa fedha
hizo ambazo Serikali iliahidi kutoa kwa ajili ya rambi rambi ya marehemu
Kanumba aliyeweza kuinua na kuitangaza tasnia ya filamu nchini.
"Nakumbuka nilienda nchini Uingereza
kufungua tawi la Chama Cha Mapinduzi (CCM) nilishangaa sana kumkuta
Kanumba huko akiwa na Mkrugenzi wa Bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka
wakiwa wanahamasisha Watanzania waishio huko kuhusiana na chama, hivyo
wanaosema Kanumba ni alikuwa si mwanachama wa CCM naomba niwaeleze kuwa
si kweli" alisema Makalla.
Naye mama mzazi wa Kanumba, Frola alitoa
shukrani kwa Serikali kwani amefarijika na kuona kwamba Serikali
inamjali licha ua kumpoteza mwanae kipenzi.
"Kwa kweli naishukuru sana Serikali kwani
wamenifariji sana, Japo Kanumba hatorudi tena lakini nimefarijika kwa
ushirikiano mlionipa" alisema mama mzazi wa Kanumba.
Wakati huohuo Mtitu alitoa shukrani kwa
Serikali kwani mchango waliotoa unaonyesha kwamba wanatambua kazi za
wasanii hapa nchini.
"Kwa jina alilokuwa nalo Kanumba pamoja na
filamu alizoigiza, hakupaswa kuwa vile ndio mana hata kwenye msiba
nilisema marehemu aliondoka akiwa masikini, hivyo tunashukuru kwamba
Serikali imetambua na imetuhakikishia kulinda kazi zetu ili na sisi tule
kutokana na jasho letu" alisema Mtitu.

Post a Comment