Boniface Meena
SAKATA la ufisadi ulioanikwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), limeingia sura mpya baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuanza kuwachunguza watendaji wote waliohusika, wakiwamo mawaziri.
SAKATA la ufisadi ulioanikwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), limeingia sura mpya baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuanza kuwachunguza watendaji wote waliohusika, wakiwamo mawaziri.
Hatua hiyo ya Takukuru imekuja wakati tayari Kamati Kuu (CC) ya CCM
imebariki uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kulisuka upya Baraza la Mawaziri
kama hatua mojawapo katika kutekeleza maazimio ya Bunge kutaka mawaziri
wanane na watendaji waliotajwa katika ripoti ya CAG wawajibishwe.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema jana kuwa
pamoja na hatua ya Rais ya kufanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri,
taasisi hiyo imeanza uchunguzi wake dhidi ya wahusika.
Dk Hoseah alisema ofisi yake imeshaanza kushughulikia tuhuma zote za
rushwa zilizotolewa na CAG na baadaye kupigiwa kelele na wabunge ili
watakaobainika wafikishwe kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), kwa
ajili ya hatua zaidi za kisheria.
“Sheria inatutaka tufanye uchunguzi wa tuhuma zozote na katika hili,
CAG alitakiwa atupe taarifa. Lakini sisi baada ya kusikia bungeni
tulimwandikia barua (CAG) kumwomba atupatie ripoti ya mambo yanayotuhusu
tuanze kuyashughulikia haraka,” alisema Dk Hoseah.
Hata hivyo, Dk Hoseah alisema asingeweza kuwataja watu
wanaowachunguza kwa majina, kwa kuwa sheria (Kifungu cha 37 cha Sheria
ya Takukuru ya mwaka 2007, kinazuia kuzungumzia mchakato wa uchunguzi).
Lakini, mawaziri waliotajwa katika ripoti hiyo ya CAG na hivyo
kushinikizwa kujiuzulu ni William Ngeleja wa Nishati na Madini na Waziri
wa Uchukuzi, Omari Nundu.
Wengine ni Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo; Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Tamisemi), George Mkuchika; Waziri wa Maliasili na Utalii,
Ezekiel Maige; Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami.
“Siwezi kusema tunamchunguza nani kwani sheria hairuhusu ila elewa tu
kwamba tuko serious (makini) na tunafanyia kazi tuhuma zote na wote
tutahakikisha tunawafikia,” alisema Dk Hoseah.
CAG akiri
Kwa upande wake CAG, Ludovick Utouh alikiri kuwasiliana na Takukuru kuhusu kuwachunguza wote waliotajwa katika ripoti yake.
“Kimsingi ofisi yangu inafanya kazi kwa karibu na Takukuru na barua
waliyotuandikia tunaendelea kuifanyia kazi. Sheria inatueleza kwamba
katika ukaguzi wetu, tunapokutana na suala lolote la rushwa
tuliwasilishe Takukuru na tumekuwa tukifanya hivyo,” alisema Utouh.
Awali, wakati sakata hilo likiwa bungeni, kuliibuka malumbano ya hapa
na pale miongoni mwa mawaziri na wasaidizi wao huku watendaji hao wa
wizara, wakitupiana mpira kuhusu kashfa mbalimbali zinazoelekezwa kwenye
ofisi zao.
Kashfa za mawaziri
Waziri Nundu na Naibu wake, Athuman Mfutakamba kwa upande mmoja na Waziri Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu walianza kutupiana mpira huku kila mmoja akijisafisha kiaina.
Waziri Nundu na Naibu wake, Athuman Mfutakamba kwa upande mmoja na Waziri Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu walianza kutupiana mpira huku kila mmoja akijisafisha kiaina.
Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu katika utetezi wake alisema Naibu
wake huyo amekuwa akishinikiza Kampuni ya China Communication
Construction Company (CCCC), ipewe kazi ya kujenga gati namba 13 na 14
katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa ilimgharamia safari kadhaa
kwenda nje.
Waziri Nundu pia alishangazwa na shinikizo la Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Miundombinu chini ya Mwenyekiti wake, Peter Serukamba kuingia
na kushinikiza CCCC ipewe kazi hiyo huku akihoji kuna nini?
Hata hivyo, Mfutakamba alipoulizwa kuhusu safari zake hizo za nje
kugharamiwa na CCCC na baadaye kuandika ripoti akishinikiza ipewe kazi
ya kujenga gati hizo, alikiri kusafirishwa na kampuni hiyo, lakini
akasema alifuata taratibu zote za kiserikali.
Nyalandu kwa upande wake, alionekana kutua mzigo wa kashfa
ulioigubika wizara hiyo ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango
Tanzania (TBS), Charles Ekelege kudaiwa kuiingizia Serikali hasara ya
karibu Sh30 milioni kwa ukaguzi hewa wa magari nje ya nchi akisema
alimshauri Waziri wake, Dk Chami kumsimamisha kazi mkurugenzi huyo
mapema.
Lakini Dk Chami alisema hadi Bunge linamalizika mjini Dodoma, alikuwa
hajaiona ripoti ya Kamati ndogo ya Bunge iliyomchunguza Ekelege ambayo
alisema ingemsaidia kupata tuhuma zinazomkabili mkurugenzi huyo ili
kuchukua hatua.
Mkulo ambaye alikuwa waziri wa kwanza kutakiwa ajiuzulu, anatuhumiwa
kuvunja Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) ili kuficha
tuhuma zake ikiwemo uuzaji wa kiwanja Na.10 kwa Kampuni ya Mohamed
Enterprises (MeTL).
Mkuchika alitakiwa aachie ngazi baada ya ripoti ya Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC) kubaini mtandao mkubwa wa wezi wa
mali za umma. Ripoti hiyo ilibainisha kuwa kwa mwaka wa fedha ulioishia
Juni 30, 2010, Sh583.2 milioni zililipwa kama mishahara hewa, kiasi
ambacho kingetosha kujenga madarasa 194.
Ripoti ya CAG ilibaini kuwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa
mwaka mmoja wa fedha linafanya ununuzi wenye thamani ya Sh300 bilioni
hadi Sh600bilioni, hivyo kumtaka Waziri Ngeleja awajibike.
Katika mwaka wa fedha 2009/2010, Tanesco ililitumia Sh1.8bilioni
ukilinganisha na Sh65 milioni zilizokuwa zimepangwa katika bajeti ya
ukarabati wa gati mojawapo katika Kituo cha Bwawa la Mtera na kuingia
mikataba isiyo na tija kwa taifa.
Waziri Maige anakabiliwa na tuhuma za kutengeneza mazingira ya rushwa
katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji, ambao inadaiwa ulitawaliwa na
dosari nyingi ikiwa ni pamoja na kutangaza majina ya waliopata vitalu
bila kuonyesha maeneo waliyopewa.
Pia, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi na Maliasili ilieleza kuwa
kampuni 16 zilizopewa vitalu hivyo hazikuomba na kwamba vitalu hivyo
vilikuwa vya daraja la kwanza na la pili.
Mbali na tuhuma hizo, Maige pia anakabiliwa na kashfa ya kununua
nyumba kwa Dola za Marekani 700,000 iliyopo Mbezi Beach, Dar es Salaam,
tuhuma ambazo alizipinga na kusema kuwa nyumba hiyo ameinunua kwa Dola
410,000, (wastani wa Sh600 milioni).
Waziri Mponda ametakiwa kuwajika baada ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD),
ambako ukaguzi maalumu wa MSD uliofanyika kubaini kuwapo tofauti ya
Sh658.9 milioni ikiwa ni pungufu ya kiasi ambacho kilipokewa na
kuripotiwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwenda MSD na ushahidi
wa kupokewa haukutolewa.
Pia kulikuwa na kiasi cha Sh100 milioni kilichopelekwa na MSD kutoka
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kikatumiwa na MSD bila kuwapo na
mchanganuo wa matumizi.
Ukaguzi maalumu ulibaini pia kuwapo kiasi cha Sh4.5 bilioni
zilizotoka Hazina kwenda Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya
kununulia dawa na vifaa vya hospitali, lakini ni kiasi cha Sh4.344
bilioni tu kilichopokewa na MSD ikiacha Sh196 milioni bila kuwepo na
ushahidi wa kupokewa na MSD kutoka wizarani.
Chanzo: Mwananchi
Post a Comment