Wafungwa watishia tena kugomea chakula
Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Godbless Lema
Mgomo
wa wafungwa unanukia kwa mara nyingine, baada ya kuwepo kwa taarifa za
wafungwa wa kifo waliopo gereza la Ilungu lililopo mkoani Mtwara,
kutangaza kugoma kula kuanzia leo. Nia
ya mgomo huo ni madai ya chakula, kupinga manyanyaso ya kipigo kutoka
kwa askari magereza pamoja na rufaa zao kuchelewa kusikilizwa na hali ya
gereza kuwa mbaya.
Wakizungumza
na NIPASHE mwishoni mwa wiki iliyopita, baadhi ya wafungwa walimshutumu
mkuu wa gereza hilo kwamba amekuwa akisimamia ukatili dhidi yao.
Walisema tangu Desemba mwaka jana, wafungwa hawapewi matunda, hawapikiwi
nyama wala hawawekewi sukari kwenye uji badala yake wanakunywa uji wa
chumvi. Wafungwa
waliozungumza na NIPASHE na namba zao kwenye mabano ni Abdul Ali Sunna
(303/2008), Salehe Ramadhani Juma (151/2005), Said Ali Majeje (93/2011),
Hussein Said Ntanda (95/2011) na Omary Mussa (104/2011); wote
wamehukumiwa kifo. Kadhalika, walisema wamefutiwa huduma ya matibabu na
badala yake wamekuwa wakielekezwa kujitibu wenyewe au kujinunulia dawa,
jambo ambalo sio sahihi.
Kuhusu
unyanyasaji, walisema tukio la kusikitisha zaidi lilitokea Desemba
mwaka jana baada ya mfungwa mwenzao waliyemtaja kwa jila moja la
Selemani mwenye namba 205/2010 ambaye amekaa gerezani kwa miaka 30
alitoroka, lakini akadakwa na askari. Walisema
askari sita walimfunga kwenye mti na kumpiga kuanzia saa moja asubuhi
hadi saa tisa alasiri; bila kuwepo kwa Ofisa Usalama wa gereza, kinyume
cha taratibu. Walisema baada ya kutoa malalamiko yao, wamegeuziwa kibao
kwa kunyanyaswa na kupigwa.
Mfungwa
mwingine Salehe Ramadhani Juma mwenye namba 151/2005, alikaa gerezani
tangu mwaka 1995 na hukumu ya kesi yake ilitolewa mwaka 2005 na alikata
rufaa, lakini hadi leo haijasikilizwa. Msemaji
wa Jeshi la Magereza, Omary Mtiga, alipotafutwa na NIPASHE kuzungumzia
azma hiyo na namna jeshi linavyoshughulikia kero hizo za wafungwa,
alisema bado hawajapata taarifa hizo hivyo hawezi kusema chochote.
“Taarifa
za mgomo hatujazipata, lakini pengine nianze kufuatilia ili tujue
tatizo nini, hadi kesho tunawezakuwa tumepata taarifa ambayo tunaweza
kukueleza,” alisema Mtiga. Kwa mara ya mwisho wafungwa waligoma Juni mwaka jana katika gereza la Maweni, mkoani Tanga kwa madai ya kupewa chakula kibovu.
Kufuatia
mgomo huo, aliyekuwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani,
Godbless Lema, alitoa ahadi ya Kambi ya Upinzani bungeni kufuatilia hali
za magereza kwa kuwa haiwezekani wafungwa wakagoma tu kula kwa kuwa
wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo rufaa zao kuchelewa
kusikilizwa na pindi wanaposhinikiza ili zisikilizwe wanahamishwa
gereza.
Lema
alisema asilimia 50 ya mahabusu wanakaa hadi miaka minane bila kesi zao
kusikilizwa kwa kisingizio cha upelelezi kutokamilika, jambo
linalochangia migomo magerezani.
HABARI NA - RESTUTA JAMES
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment