Wanafunzi Chuo Kikuu wabakwa, walawitiwa

Wanafunzi Chuo Kikuu wabakwa, walawitiwa




Image

Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma
 
WANACHUO wa Chuo Kikuu cha St John mjini Dodoma, leo wamegoma kuingia
madarasani hadi wawasilishe malalamiko yao kwa Kamanda wa Polisi wa
Mkoa, Zelothe Stephen kutokana na kukithiri kwa vitendo vya kupigwa
nondo, kuibiwa kadi za benki, kompyuta za mkononi, kulawitiwa na
kubakwa.

Hali hiyo ilisababisha wanafunzi kukusanyika huku wakiwa wamebeba
mabango mbalimbali ambayo yalikuwa yakisomeka, ‘Tunaomba ulinzi ili
kubaka na kulawitiwa kukomeshwe’, ‘Ulinzi ni haki yetu ya msingi polisi
Mko wapi? Tumechoka kuwa wajinga katika jamii yetu na Ulinzi Shirikishi
stop crime.’

Baadhi ya wanafunzi hao walilaani vitendo vya wenzao kubakwa na
kulawitiwa na kudai kuwa katika siku za hivi karibuni, mwanafunzi wa
kiume ambaye anasoma mwaka mwaka wa pili aliibiwa na kisha kulawitiwa
hali iliyolazimu alazwe hospitali.

“Kesi kadhaa zimepelekwa polisi lakini hakuna chochote kinachofanyika,” alisikika mwanachuo moja akizungumza kwa jazba.

Walisema kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na wakati mgumu
kutokana na kuibiwa vifaa muhimu zikiwemo kompyuta za mkononi hali
ambayo hulazimika kuishi kwa hofu.

“Juzi wenzetu wamevamiwa usiku na kuporwa simu tano na laptop tatu
sasa tunaona maisha yanakuwa magumu sana kwetu kwani usalama wetu sasa
ni mdogo,” alisema mmoja wa wanafunzi hao.

Walisema hali ni mbaya zaidi kwa wanafunzi ambao wanaishi nje ya
chuo kwani hata kujisomea nyakati za jioni kumekuwa kwa mashaka
kutokana na kuogopa kuvamiwa na vibaka.
Walisema baadhi ya wenzao wanaanza mitihani Juni, hali ambayo
inawatia hofu kama wimbi hilo la kuvamiwa na vibaka linaweza hata
kupunguza ufaulu mioungoni mwao.

Pia walitaja sababu kadhaa ambazo zinadhaniwa kuwa zinasababisha
matukio hayo ni chuo hicho kukosa uzio na hivyo kufanya mwingiliano wa
watu na wanachuo kuingia chuoni bila kuwa na utaratibu.

Walisema kundi lisilojulikana limekuwa na kawaida ya kuvamia sehemu
ambazo wanachuo wanakaa na baada ya kuiba vitu mbalimbali humalizia kwa
kubaka wasichana au kwa kulawiti kama ni mvulana.

Hata hivyo, juhudi za wanafunzi wao kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Dodoma hazikufanikiwa baada ya kuelezwa kuwa alikuwa na majukumu
mengine ya kikazi, na kutuma mwakilishi wake ambaye ni Mkuu wa Polisi
Wilaya, Dominic Mlei na Mkuu Mpya wa Polisi wa Wilaya atakayeanza kazi
hivi karibuni, Thadeus Malingumu.

Kwa upande wake, OCD Mlei alisema ulinzi unaanza rasmi leo, kufanya
doria maeneo yanayozunguka chuo hicho na maeneo jirani, pia chuo
kijenge hosteli za kutosha na kwa kila hosteli za nje na nyumba
walizopanga wanafunzi zitakaguliwa kesho na mapungufu ya kiusalama
kwenye makazi hayo yataainishwa na wamiliki wataitwa na hosteli zote
zitatakiwa kuwa na mageti na ulinzi wa makazi hayo kuboreshwa.

Pia alitaka kuundwa kwa mara moja kwa vikundi vya ulinzi shirikishi.

Hata hivyo, mtumishi wa Chuo hicho, Mzee Muganda alishauri Kituo Kidogo cha Polisi kijengwe Kikuyu na bidii ya doria iongezwe
Source: Habari Leo Mtandaoni

Post a Comment

Previous Post Next Post