WAKATI CCM, ikihaha kujaza watu kwenye mkutano wake, Katibu Mkuu wa
CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa, amekidhihaki chama hicho kuwa hakiwezi
kuendelea kutawala nchi kwa kuwalipia nauli, kuwabeba na kuwapa posho
watu wanaokwenda kwenye mikutano.
Slaa, alisema ilani ya chama chochote makini inapaswa kuonekana
machoni mwa wananchi na siyo kusemwa kama ambavyo Rais Jakaya Kikwete na
timu yake ndani ya CCM wanavyofanya.
Kauli hiyo aliitoa jana katika Uwanja wa Likangala wilayani Ruangwa
mkoani Lindi wakati akihutubia mkutano wa hadhara, huku akitanabaisha
kuwa wafuasi wanaokipenda chama chao hawawezi kubebwa na magari kwenda
kwenye mikutano kwa kulipiwa nauli.
Dk. Slaa alikuwa akijibu matamshi mbalimbali yaliyokuwa yakitolewa na
viongozi wa CCM katika mkutano wao wa hadhara uliofanyika katika viwanja
vya Jangwani jijini Dar es Salaam na kurushwa moja kwa moja na vituo
vya redio na runinga.
Alisema mawaziri wa CCM wamekuwa makasuku kwa kushindwa kutathmini
kauli zao za awali, ambazo hazijatekelezwa na kwamba sasa wanakuja na
hoja nyingine zisizotekelezeka.
Akiwachambua baadhi ya mawaziri na kuanza na Jumanne Maghembe, alisema
kuwa anapaswa akumbuke miaka zaidi ya kumi iliyopita serikali ilikuja
na mkakati wa kilimo cha umwagiliaji na kusema imeshapata kiasi cha dola
milioni 12 za Marekani kwa ajili ya shughuli hiyo.
“Tunataka watuambie hizi fedha zimeenda wapi mpaka sasa wanakuja na
kauli nyingine, hivi hakumbuki tulikaa katika ukumbi wa mikutano wa Pius
Msekwa wakatuambia hizi fedha zipo, sasa zimeenda wapi?” alihoji Dk.
Slaa.
Kuhusu ujenzi wa barabara kilomita 11,000 zilizoelezwa na Waziri wa
Ujenzi, Dk. John Magufuli, Slaa alisema huo ni upuuzi kwa kufananisha
hali hiyo na mahitaji mazima ya nchi.
Alisema fedha zilizoibwa na watumishi wa serikali ya CCM ni nyingi
kuliko hivyo wanavyojinadi kuwa wamefanya, na kuitaka serikali ieleze
dola milioni 1.5 zilizokutwa katika akaunti ya mbunge wa Bariadi
Magharibi, Andrew Chenge (CCM) zimefanyiwa nini.
Alibainisha kuwa, Serikali ya CCM inapaswa kutolea maelezo fedha za
chenji ya rada zimefanya nini wakati katika mahesabu ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hazionekani kutumika.
Kuhusu kauli ya Steven Wassira kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA,
Freeman Mbowe atalaaniwa kwa kuwa baba yake aligombea uhuru na Mwalimu
Nyerere, Dk. Slaa alisema viongozi hao walisimama kwa ajili ya kuwatetea
Watanzania na kama watasimama leo kuna hatari ya kuwachapa viboko
viongozi wa CCM kwa kushindwa kuendeleza malengo waliyofikia.
Naye Mbowe alisema anamsikitikia Wassira kwa kile alichoeleza kuwa,
anashindwa kusimamia hata utendaji wa nafasi yake na badala yake
anahangaika kuropoka kila wakati mambo yasiyo na tija kwa taifa.
Alibainisha kuwa, Wassira si saizi yake kwenye majukwaa ya kisiasa kwa
sababu hana hadhi ya kupigania ukombozi wa kweli, hivyo akamtaka
awatafute watu wenye hadhi yake.
Alisema katika hali ya sasa, CCM haioni mahaba ya wananchi, hivyo
wanajitahidi kukusanya watu katika maeneo mbali mbali ya nchi ikiwa ni
pamoja na kununua kadi za CHADEMA kwa ajili ya kujiaminisha mbele ya
wananchi.
“Hawa watu vipi, wana nini sijui kwa kuwa wanatunga uongo
wanauaminisha umma na mwisho wa siku wanauamini huo uongo walioutunga
kama ambavyo wamefanya leo kule Jangwani,” alisema Mbowe
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz
Post a Comment