CHADEMA yazidi kumkaba Mkuchika

CHADEMA yazidi kumkaba Mkuchika

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika kuhakikisha sh bilioni 40 zilizochotwa kwa ufisadi na Kampuni ya Kagoda zirudishwa na kuwanufaisha wakulima, wakiwamo wa k
orosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Pamoja na hilo, chama hicho kimemtaka Mkuchika kumwajibisha Diwani wa Mkwedu, Juma Dadi, anayedaiwa na wanakijiji wa Tengulengu wilayani Newala, mkoani Mtwara kutofika katika ofisi yake kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na kuwafanya wananchi washindwe kujua sehemu ya kupeleka kero zao.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika alipokuwa akifanya mikutano katika Kata ya Makukwe na Mkwedu wilayani hapa na wananchi kumueleza kero mbalimbali, ikiwamo kupeleka barua ya kumlalamikia diwani huyo kwa Mkurugenzi wa mji wa Newala na mbunge wa jimbo hilo, Mkuchika na kwamba hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa hadi sasa.
Alisema udhaifu wa Mkuchika kusimamia majukumu yake haukuishia katika jimbo analoliongoza, kwani alipokuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zilionyesha ufisadi alioshindwa kuusimamia na kusababaisha nchi kuingia katika hasara.
“Hivi kuna nini baina yao (Mkuchika na Rais Jakaya Kikwete)? Ripoti zinaonyesha udhaifu mkubwa alionao juu ya usimamizi wa mali ya umma, lakini rais anamsogeza karibu yake, tena kwenye wizara nyeti ambayo TAKUKURU inakuwa chini yake. Mnadhani mali zetu zitaendelea kuwa salama?” alihoji Mnyika.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema Rais Kikwete aliahidi bungeni kuwa fedha hizo zitarudi na kuingizwa katika Benki ya Rasilimali (TIB), hivyo ni wakati muafaka kwa Mkuchika kuhakikisha fedha hizo zipo na kwamba kinyume cha hapo itaaminika kuwa amekwenda kuwalinda mafisadi.
Aliongeza kuwa, ni wakati wa Mkuchika kuhakikisha ufisadi wa Newala na maeneo mengine ambayo ripoti ya CAG imeainisha, unashughulikiwa na kuwahakikishia wananchi kuwa uwepo wake hauhusiani na mafisadi.
Kuhusu diwani wa Mkwedu kutohudhuria katika mipango ya maendeleo ya kata, Mnyika alisema ni aibu kwa Mkuchika kuzunguka maeneo mengine na kuwakemea madiwani wasiofanya mikutano na wannchi huku akiwa na barua ya wananchi wa Newala wanaomlalamikia kuhusu jambo hilo hilo.
Alisema ni wakati wa kuacha kulindana kwa maslahi ya kisiasa na badala yake aonyeshe mfano kwa kumwajibisha Mkurugenzi wa Mji wa Newala pamoja na diwani huyo anayelalamikiwa kwa kushindwa kusimamia majukumu yao.
Aidha, Mnyika alilisisitiza kuwa, Mkuchika anapaswa kujipima katika nafasi yake hiyo kama inamfaa kwa kuwa wananchi wake wanamlalamikia kwa kuonyesha mfano mbaya wa uongozi, kwa kuamua kuhamisha kituo cha afya na makao ya tarafa kwenda kwenye maeneo yasiyopimwa bila kuwashirikisha wananchi.
Chanzo:- Tanzania daima

Post a Comment

Previous Post Next Post