KONGAMANO LA MICHEZO KWA MAENDELEO NA AMANI KUANZA KESHO.

KONGAMANO LA MICHEZO KWA MAENDELEO NA AMANI KUANZA KESHO.


Na Mwandishi wetu
  Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na taasisi za Right To Play na British Council zimeandaa Kongamano la Michezo kwa Maendeleo na Amani linalotarajia kuanza kesho  katika Hoteli ya Blue Pearl kuanzia 3: 00 asubuhi.
 
Akiongea na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Bw. Leonard Thadeo amesema lengo kubwa la Kongamano hilo ni kutoa fursa kwa wadau mbalimbali kubadilishana mawazo, kupeana uzoefu na kuangalia kwa pamoja changamoto zinazoikabili sekta ya michezo nchini.
 
Bw. Thadeo amesema, katika Kongamano hilo washiriki wataangalia Sera ya Michezo inazungumziaje matumizi ya michezo kama nyenzo ya kukuza maendeleo na kuhamasisha amani.
 
Aidha, amesema  kutakuwa na mjadala wa kuangalia ni jinsi gani michezo inaweza  kusaidia utekelezaji wa Mikakati mbalimbali ya kitaifa kama vile MKUKUTA na Mpango wa Taifa wa Maendeleo.
 
Naye Mkurugenzi wa Right To Play nchini, Bibi Josephine Mukakalisa amesema  michezo inatumika si tu kuburudisha bali pia kuelimisha, kuhamasisha watoto wa jinsia zote kushiriki katika uongozi na kutoa maamuzi yanayolenga kuendeleza jamii husika.
 
Kwa upande wake Meneja Mradi, British Council, Bw. George Agango ameeleza kuwa Kongamano hilo ni fursa  kwa wadau kujadili kwa pamoja namna ya kuendeleza vijana katika michezo na kuhamasisha watoto wa kike na walemavu kushiriki  katika michezo kwa ajili ya Maendeleo.
 
Kongamano hilo la siku mbili litashirikisha Vyama vya Michezo, Wawakilishi wa Mikoa, Ofisi za Kibalozi nchini, Ofisi za Serikali na Wanahabari.

Post a Comment

Previous Post Next Post