Madaktari watishia kugoma tena
Waitisha mkutano wao kesho Dar
MADAKTARI nchini wametishia kuitisha tena mgomo nchi nzima
kushinikiza utekelezaji wa madai waliyoahidiwa na serikali Machi mwaka
huu, Tanzania Daima limebaini.
Ili kutekeleza azma hiyo ambayo
inaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii kuliko ilivyokuwa wakati wa
mgomo wa awali, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kimeitisha mkutano
wa wanachama wake kesho, pamoja na mambo mengine kutoa taarifa ya
utekelezaji ya maazimio ya serikali.
Kwa mujibu wa habari hizo, mkutano huo unatarajiwa kutoa maazimio ya
nini kifanyike ambapo baadhi ya madaktari kutoka chama hicho walidokeza
kuwa wanatarajia kuitisha mgomo mwingine nchi nzima.
Vyanzo vya habari kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge na Huduma za Jamii
ambazo gazeti hili imezipata, zilisema kuwa tayari madaktari hao
wamewasilisha dhamira yao ya kutaka kugoma kwenye Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Huduma za Jamii.
Ikumbukwe kwamba kamati hiyo iliacha shughuli zake bungeni kuja
kuchunguza chanzo cha mgomo wa awali wa madaktari ambao ulisababisha
vifo vya mamia ya Watanzania.
Hadi sasa serikali imeshindwa kutoa idadi kamili ya wananchi waliopoteza maisha kutokana na mgomo huo.
Habari zaidi zilidai kuwa hadi sasa serikali imetekeleza agizo moja tu
la madaktari hao nalo ni kumsimamisha kazi Katibu Mkuu Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii Blandina Nyoni na Mkuu Mkuu, Dk. Deo Mtasiwa.
Baadaye Rais Jakaya Kikwete aliamua kumtema Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii, Dk. Haji Mponda, na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya, wakati
alipofanya madailiko ya Baraza lake la Mawaziri hivi karibuni.
“Hadi leo serikali imeshughulikia madai ya uwajibishwaji na watendaji
wa wizara. Waziri Mkuu Mizengo Pinda alimsimamisha kazi Katibu Mkuu na
Mganga Mkuu. Baadaye Rais Kikwete alimtema Waziri wa Afya na Naibu wake.
Madai mengine hayajatekelezwa hadi sasa,” kilisema chanzo chetu cha
habari.
Hata hivyo serikali haikuweka muda wa ukomo wa utekelezaji wa maazimio hayo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Rais wa MAT, Dk. Namala Mkopi,
alisema chama hicho kinakutana na wanachama wake kesho kueleza
utekelezaji wa ahadi za serikali.
“Siwezi kukuambia zaidi ila kweli tuna mkutano Jumamosi kutoa taarifa
ya utekelezaji wa madai yetu. Nikikuambia zaidi nitakuwa naingilia kile
tunachotaka kwenda kujadili, jambo ambalo sio zuri sana,” alisema Dk.
Mkopi.
Februari mwaka huu, Waziri Mkuu, Pinda, alimsimamisha kazi Katibu Mkuu
Nyoni na Mganga Mkuu, Dk. Mtasiwa, kutokana na tuhuma za kuingiza
nchini robo tatu ya vifaa bandia vya vipimo vya ukimwi kutoka Korea
Kusini.
Alitaja sababu zingine kuwa ni tuhuma za kuanzisha kampuni ya
kusambaza nguo kwa madaktari na kuiingiza kinyemela kampuni ya kufanya
usafi ndani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbil. Pinda alisema tuhuma hizo
ni nzito zinazoidhalilisha serikali na kamwe haitakuwa busara
kuzifumbia macho huku serikali ikiendelea kudhalilika.
Alisema malalamiko ya madaktari ni makubwa na kwamba yana msingi wa
kusikilizwa na kusihi kamati iliyoundwa kuorodhesha kila kitu ili
serikali iweze kuyafanyia kazi.
Madaktari hao walirejea kazini Machi 7 mwaka huu baada ya mazungumzo yao na Rais Kikwete Ikulu.
Katika mgomo huo wa siku 20, madaktari walitaka utekelezaji wa maslahi
yao mbalimbali ikiwemo kuongezewa mishahara, kupatiwa nyumba, kuongezwa
posho na pia kuwajibishwa kwa watendaji wa wizara ambao walikuwa ni
Katibu Mkuu, Blandina Nyoni, Mganga Mkuu, Dk. Deo Mtasiwa na mawaziri
wao.
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz
Post a Comment