WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameendeleza moto
ndani ya wizara hiyo ambapo jana alitengua uamuzi uliofanywa na Waziri
aliyepita, Omary Nundu, wa kuwasimamisha kazi maofisa saba wa Tazara.
Dk. Mwakyembe ambaye wiki moja iliyopita aliwatimua vigogo wa Shirika
la Ndege la Taifa (ATCL), alisema ameamua kutengua uamuzi wa waziri
mwenzake aliyepita kwa madai kuwa utaratibu wa kuwasimamisha kazi
haukuwa sahihi.
Nundu, aliwasimamisha kazi viongozi saba wa menejimenti ya Shirika la
Reli la Tanzania na Zambia (Tazara), akidai kabla ya kufikia uamuzi huo
alifanya uchunguzi na kujiridhisha kuwa wanapaswa kuwaweka pembeni kama
hatua za kiutawala zinavyotaka na kusubiri zile za kisheria kuchukua
mkondo wake.
Jana katika kikao cha ghafla alichohitisha ofisini kwake, Waziri
Mwakyembe alisema mbele ya waandishi wa habari kuwa utaratibu wa
kusimamishwa kazi wafanyakazi hao haukuwa sahihi.
“Katika kikao tulichoketi Juni 11 jijini Dar es Salaam pamoja na
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, Waziri wa
Usafirishaji, Kazi na Mawasiliano wa Zambia Yamfwa Mukanga, Naibu Waziri
wa Fedha na Mipango wa Zambia, Miles Sampa na Naibu Waziri wa Biashara
na Viwanda wa Zambia, Keith Mukata, tumeafikiana mambo mbalimbali
ikiwemo kuimarisha nguvu ya bodi ya wakurugenzi wa Tazara,” alisema.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mwakyembe, wameitaka bodi kukaa kupitia upya uamuzi huo.
Pia bodi iliyoteuliwa itakuwa na wajibu wa kupitia vifungu na taratibu zilizochokuliwa katika kuwasimamisha maofisa hao.
Viongozi waliosimamishwa ni wale waliokuwa wakikaimu, akiwamo
mwendesha mitambo mkuu, meneja masoko, meneja mwongozaji wa treni,
meneja wa fedha na mkuu wa IT.
Miongoni mwa tuhuma zinazowakabili watu hao ni pamoja na kusababisha
hasara katika shirika hilo, kupungua kwa uzito wa tani za shaba
zinazosafirishwa kila wakati, kutokupeleka makato ya wafanyakazi NSSF,
pamoja na kufanya kazi kirafiki kulikosababisha baadhi ya wateja wa
shirika hilo kukwepa kusafirisha mizigo yao.
Post a Comment