Siko seli huua asilimia 50 ya watoto wanaozaliwa

ASILIMIA 50 ya watoto kati ya 8,000 na 11,000 wanaozaliwa na ugonjwa wa sikoseli nchini kila mwaka hufariki kwa ugonjwa huo.
Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Huduma za Ugonjwa wa sikoseli katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Dk. Deogratias Soka alipokuwa akielezea mkutano wa mtandao wa utafiti wa ugonjwa huo Afrika Mashariki na Kati ambao unatarajiwa kufanyika leo.
Alisema wengi wa watoto hao hufariki ndani ya miaka miwili tangu wazaliwe na kuongeza kuwa hali hiyo inachangiwa na jamii kutokuwa na ufahamu juu ya ugonjwa huo.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya watoto katika hospitali hiyo Dk. Edward Kija, alisema kuwa ugonjwa huo unarithiwa kutoka kwenye vinasaba vya ugonjwa huo kwa wazazi wake na kusema kuwa hapa nchini asilimia 13 ya watu wote wanaishi na vinasaba vya ugonjwa huo.
Alisema watoto wanaougua ugonjwa huo wanakabiliwa na tatizo la upungufu wa damu, maambukizi katika mfumo wa damu na kupata maumivu ya viungo na mifupa.
Alisema wamefanya utafiti mbalimbali kuhusu ugonjwa huo na kwamba lengo ni kuboresha huduma hizo ambazo mpaka sasa kwa hapa nchini zinapatikana katika Hospitali ya Muhimbili pekee.
Aidha alisema kutokana na jamii kutokuwa na uelewa juu ya ugonjwa huo, kesho katika viwanja vya michezo hospitalini hapo kutafanyika Siku ya Siko Seli ambapo wananchi watapatiwa elimu na hatimaye kuondokana na imani potofu kwamba mtoto mwenye ugonjwa huo haishi zaidi ya miaka 18.
Naye Dk. Leon Tshilolo kutoka Hospitali ya Kinshasa, nchini Kongo, alisema katika bara la Afrika nchi inayoongoza kwa ugonjwa huo ni Kongo, ikifuatiwa na Garbon na Tanzania.

Post a Comment

Previous Post Next Post