Uamsho: Tutapambana hadi tuhakikishe Zanzibar inakuwa huru

KUFUATIA vurugu zilizotokea Mei 26 mwaka huu mjini Zanzibar zikiihusisha Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki) au maarufu kama Uamsho, wengi wamekuwa wakijiuliza undani wa kikundi hicho.
Akizungumza na mwandishi wetu ELIAS MSUYA mjini Zanzibar hivi karibuni, msemaji wa kundi hilo Sheikh Farid Hadi Ahmad anaeleza mikakati ya kikundi hicho katika kupinga muungano.
Swali: Kwanza naomba kujua historia yako ya uanaharakati katika dini na siasa na lini mlianzisha kundi hili la uamsho?
Jibu: Kama ni mambo ya Uamsho, yana viongozi wake ungewauliza wao, mimi ni Amiri mkuu wa Maimamu wa Zanzibar.  Lakini kwa ufupi hizi harakati zimeanza wakati wa mchakato wa katiba ambapo kwa mara ya kwanza muswada wa Katiba ulipoletwa na kujadiliwa katika hoteli ya Bwawani hata maafisa wa serikali waliikataa. Sisi Jumuiya za mihadhara ya kiislamu pia tuliikataa.
Ilitakiwa baada ya kurudishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa ili kurekebishwa, wailete tena ili tuujadili. Lakini waliileta ikiwa tayari ni sheria yenye utata huo huo.
Upungufu mkubwa tunaoulalamikia upo katika kifungu cha tisa ambacho kinabainisha mambo matakatifu yasiyotakiwa kuguswa ukiwemo muungano. Hata Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akiizindua Tume ya atiba alisisitiza kuwa uwepo wa muungano usiguswe.
Sisi Wazanzibari tunajua uwepo wetu kwenye atiba ya muungano ni ni muungano wenyewe, siyo rasilimali za bara, siyo madini aau korosho au kilimo. Sasa kwa nini muungano usijadiliwe kwanza kabla ya hiyo katiba?
Kuhusu kundi la Uamsho, mimi nimekuwa mzungumzaji tu katika kipindi hiki cha kujadili mabadiliko ya Katiba.
Jumuiya hii ya Mihadhara ya Kiislamu inaundwa na jumuiya zaidi ya 30 za kiislamu za Unguja na Pemba.Ilianzishwa kwaajili ya shughuli za kidini. Wakati huu wa kujadili katiba tulipopata taarifa, tuliona kuna haja ya kujadili nafasi ya Zanzibar katika muungano.
Kwa hiyo tulikwenda kuwaelimisha wenzetu kule Pemba na baadaye tukaenda Dar es Salaam kushauriana na wataalamu wa sheria.
Baada ya hapo tulinda kamati ya watu 15 kutoka katika ma sheikh, taasisi za kiislamu na wanasheria. Vilevile tuliteuliwa watu watatu ambao tutakuwa tukiangalia mambo muhimu katika mchakato wa Katiba na muungano.
Watu hao ni pamoja na Mwenyekiti Sheikh Mselem bin Ali, makamu mwenyekiti ni mimi na Katibu ni Sheikh Nassor bin Omari.
Ndiyo maana mimi nimekuwa msemaji mkuu wa Jumuiya hii ya Uamsho.
Swali: Katika historia ya maisha yako, unadaiwa kuishi Oman na uliwahi kushiriki jesi la nchi hiyo?
Jibu: Siyo kweli, huo ni uzushi wa kipuuzi.
Swali: Vilevile kundi lenu linahusishwa na juhudi za wenyeji wa kisiwa cha Pemba waliotaka kujitenga na kuanzisha nchi yao. Unasemaje?
Jibu: Huo nao ni uzushi. Ni kweli, kati yetu wapo wenyeji wa Pemba lakini pia tupo wa Unguja.
Swali: Hebu tueleze tukio la Mei 29 mwaka huu, uilikuwaje mkafanya vurugu?
Jibu: Mei 26, tulitoa taarifa polisi kwamba tutafanya mhadhara na maandamano. Kimsingi yale hayakuwa maandamano, yalikuwa ni matembezi tu. Watu tumefanya mghadhara pale Lumumba kisha tukajisikia kutembea tu. Mimi nilijisikia tu kutembea na watu wengi wakanifuata, yalikuwa matembezi mazuri tu. Naamini hatukufanya kosa kwani hata Katiba ya Zanzibar ibara ya 16 inatoa uhuru wa wananchi kutoa maoni yao.
Tulifanya maandamano kwa amani, hakuna hata jani lililokatika hadi yalipoisha. Lakini Jeshi la Polisi liliona kilichofanyika siyo halali. Nashangaa Rais Ali Mohamed Shein kulisifia jeshi hilo.
Polisi walikwenda kumkamata Sheikh Mussa Juma akiwa msikitini. Nashangaa kwa sababu Uamsho tuna ofisi na wanazijua, wana namba zetu za simu. Kwa nini wasitupigie au kuja ofisini kutujulisha kuwa wanatuhitaji waje watukamate kama wezi? Hapo unategemea nini? Vijana hawakukubali kuona sheikh wao amekamatwa, wakaingia mitaani kumtetea. Ndiyo vurugu zikaanza.  Mabomu yakapigwa michenzani kote ikawa moshi mtupu.
Swali: Kwa hiyo ndiyo mkaamua kuchoma makanisa na bar?
Jibu: Kwanza nashangaa kusikia Wakristo wakilalamika kunyanyaswa na tunawachomea makanisa. Sisi tunalaani watu hao na tunayo majina tuliyofanyia uchunguzi tutawakabidhi polisi. Uislamu haulazimishi mtu dini.
Wanasema makanisa 25 yamechomwa, wakati ni makanisa mawili tu. Hata ninyi waandishi wa habari mtende haki, maana siku hizi mnaonyesha tu makanisa wakati hata sisi Waislamu tunaonewa.
Mimi niliwahi kukamatwa na polisi mwaka 2004 na kufungwa kitambaa cheusi usoni na kupelekwa porini na kuteswa kama jambazi, bila kosa lolote.
Kuna wakati hapa polisi walimpiga risasi sheikh akiwa anatoka msikitini. Katika tukio hili la juzi, kuna msikiti umevunjwa, hayo mbona hamsemi? Polisi wamevamia nyumba ya Sheikh Mselem na kuvunja milango, mbona hamsemi?
Dini yetu inatufundisha kuishi na watu wa dini nyingine. Hata wakati wa Mtume Muhammad, waliowaokoa waislamu ni wakristo. Wakati waislamu kutoka Makka kwenda Habasha walikuwa wakristo. Mfalme wa habasha alikuwa mkristo.
Ila pia dini yetu inatufundisha kutokubali kuonewa. Sisi ni watulivu, lakini ukituchokoza hatutakaa kimya. Wewe mtu akikupiga kibao shavuni, utamwangalia tu?
Swali: Sasa kama vurugu zilianzia kwenu, unadhani nani amechoma hayo makanisa na bar?
Jibu: Hao ni Wazanzibari tu wenye hasira. Siyo kazi yetu kufanya upelelezi, polisi ndiyo wanajua watu waliofanya fujo, kawaulize.
Swali: Kikundi cha uamsho kilisajiliwa kwa malengo ya kuhubiri dini, vipi leo mmejiingiza kwenye siasa na sasa mahubiri yenu yanawachochea wananchi kufanya vurugu.
Jibu: Katiba ya Zanzibar inatoa haki kwa kila mwananchi kushiriki uongozi wa nchi. Uongozi wan chi ni suala pana ndiyo maana na sisi tunashiriki katika siasa. Mbona hata kina Dk wilbrod Slaa ni padre na hata Nyerere alikuwa hivyo hivyo lakini wanashiriki siasa?
Swali: Lakini Dk Slaa hayuko tena kwenye dini, amejiunga na chama cha siasa ndiyo maana yuko kwenye majukwaa ya siasa tofauti na ninyi mnaotumia majukwaa ya dini kuhubiri siasa?
Jibu: Ukristo unasema ya Mungu mpe Mungu nay a Kaisari mpe Kaisari, lakini kwetu Waislamu hiyo haipo. Uislamu ni mfumo mzima wa maisha. Neno siasa ni neno la kiarabu na lina maanisha uongozi.
Hata Mtume Muhammad alikuwa rais katika eneo lake na vilevile alikuwa kiongozi wa dini, kwa hiyo na sisi hatuna makosa kushiriki siasa hata kama ni viongozi wa dini.
Mahubiri yetu hayachochei vurugu ila ndiyo njia ya kuwaelimisha Wazanzibari kudai nchi yao. Sisi hatuna vurugu, ila tukichokozwa hatutakaa kimya.
Swali: Kwa kuwa madai yenu ya msingi ni kujitenga na muungano, unadhani nini kifanyike?
Jibu: Mimi naamini kabisa, kura ya maoni ndiyo itamaliza yote haya. Sisi lengo letu ni kukwamisha kabisa mchakato wa Katiba hapa Zanzibar ili kura ya maoni ipigwe Wazanzibari waamue. Siamini kama kuna Mzanzibari mzalendo atakayeklubali muungano.
Tunasisitiza kwamba hatuna nia ya kuwa viongozi wa Serikali, rais Shein na viongozi wenzake waendelee kushika nafasi zao tu. Shida yetu sisi ni kuwa nchi huru.
Kwa kuna shida gani sisi kujitenga? Mbona ncghi za Kenya na Uganda hatujajiunga nazo lakini tuna uhusiano mzuri tu? Nchi nyingi tu zimeshajitanga na wanaishi vizuri. Sudan kusini hata haikuwa nchi lakini ikaenda kwenye kura ya maoni na sasa ni nchi kamili, sembuse sisi tuliokuwa nchi tangu awali?
Swali: Mmewahi kupeleka madai haya kwenye ngazi ya serikali?
Jibu: Ndiyo, tumewahi kuwashirikisha Baraza la Wawakilishi, Makamu wa kwanza wa Rais Seif Sharif Hamad, tulikwenda hadi kwa Rais lakini akatuambia tuonane na waziri wa Sheria na Katiba na tukamwona.
Hata wakati wa kura za maoni kwaajili ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Serikali ilitushirikisha katika hatua zote.
Swali: Sasa kwa kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeshaundwa na vyama vya CCM kinachoongozwa na Serikali mbili huku CUF kikiiamini Serikali tatu, hamwoni kwamba mkianzisha mambo ya kujitenga na muungano mtaivuruga Serikali hiyo na umoja wa Wazanzibari?
Jibu: Tunachozungumzia sisi ni Zanzibari yetu siyo vyama. Kama ni vyama basi tutaviunganisha hata kama vinatofautiana katika sera za serikali. Tutawaunganisha wananchi bila kujali vyama.
Kwanza ukifuatilia hata hizo sera za Serikali moja, mbili au tatu, zimeshapitwa na wakati. Sera za vyama siyo Qur’an au Biblia, zinabadilika.
Swali: nini hatima ya harakati zenu?
Jibu: Sisi tutapambana hadi kieleweke na tunaamini tutashinda. Maopambano yetu yatakamilika pale tutakapoona Zanzibar imekuwa huru.

Post a Comment

Previous Post Next Post