Wapinzani wa Yanga Kagame kutajwa leo

Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati, Cecafa, Nicholaus Musonye
Dynamo, TP Mazembe zajitoa, Superspot kuonyesha 'live'
Mwandishi Wetu na Mashirika
WAPINZANI wa Yanga, mabingwa watetezi Kombe la Kagame watajulikana leo wakati ratiba ya michuano hiyo itakapowekwa hadharani tayari kwa michuano hiyo itakayoanza Julai 14 hadi 28 kwenye Uwanja wa taifa, Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati, Cecafa, Nicholaus Musonye alisema jana kuwa ratiba hiyo itakuwa hadharani baada ya timu zote kuthibitisha kushiriki michuano hiyo.

Yanga inayotetea ubingwa wake, huenda ikafungua dimba la michuano hiyo. Itasindikizwa na timu za Simba (bingwa Bara) na Azam iliyoshika nafasi ya pili.

Musonye alisema kuwa michuano itafanyika kama ilivyopangwa jijini Dar es Salaam na ule wa Azam wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 7,000.
 
Timu zitakazoshiriki ni APR (Rwanda), Yanga, Simba, Azam (Tanzania), Tusker (Kenya), Wau Salam (Sudan ya Kusini) na Atletico ya Burundi.

Timu nyingine ni Mafunzo (Zanzibar) Mamlaka ya Mapato (Uganda), Elman (Somalia), Ports (Djibouti), Red Sea (Eritrea) na Coffee ya Ethiopia.
 
Naye Rais wa Cecafa, Leodegar Tenga wamemshukuru Rais Paul Kagame kwa jitihada zake za kuinua soka katika ukanda huo. Rais Kagame amekuwa akidhamini michuano ya Cecafa tangu 1999.
 
Musonye aliwataka wadhamini wengine kujitokeza kusaidia kufanikisha michuano ya 2012 kama ilivyofanya Supersport ambayo imeahidi kuonyesha 'live' mechi za michuano hiyo.

Wakati huo huo, Dynamos ya Zimbabwe imetupilia mbali mwaliko wa Cecafa kushiriki michuano yake kwa kuwa inajiandaa na mechi za Kombe la Caf dhidi ya Inter-club ya Angola.
 
Dynamos itacheza mechi yake kati ya Julai 14 na 16 siku ambayo michuano itaanza. Mbali na mechi hiyo, pia inakabiliwa na mechi ya ligi dhidi ya Hwange na Highlanders pamoja na michuano ya Banc ABC Super Eight inayoanza Julai 21.
 
Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Ray Kazembe alisema kuwa hawataweza kwenda Tanzania kutokana na majukumu hayo.
 
Mbali na timu hiyo, Musonye alisema pia kuwa wanatarajia Vita Club ya DRC pamoja na   Bloemfontein Celtics, Platinum FC na Silver Stars za Afrika Kusini kushiriki michuano hiyo.
 
Awali ilielezwa kuwa Orlando Pirates ilialikwa lakini huenda isije kutokana na majukumu ya ligi wakati TP Mazembe iliyoalikwa, imechomoa kwa kuwa inabanwa na mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.
 
"Kwa sasa tuko katika mchakato kuhakikisha tunapata timu tatu kutoka nje ya ukanda wa Cecafa. nafasi ya timu kuja ni kubwa, na tunapigana kupata timu moja kutoka DR Congo," Musonye alisema.
 
"Madhumuni ya Cecafa kualika timu hizi ni kuipa sura michuano hii kwa kuwa ni mikubwa katika ukanda huu."

Post a Comment

Previous Post Next Post