Bahanuzi, Chuji waenda Taifa Stars

Bahanuzi, Chuji waenda Taifa Stars

Athuman Iddi 'Chuji'


MSHAMBULIAJI wa Yanga, Said Bahanuzi, ameanza kufaidi matunda ya mafanikio ya Kombe la Kagame baada ya kujumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.

Mchezaji huyo amekuwa gumzo sasa katika medani ya soka nchini baada ya kuibuka mfungaji bora kwenye mashindano ya Kagame yaliyomalizika wikiendi iliyopita ambapo Yanga ilitwaa taji hilo kwa mara ya pili mfululizo.

Habari kutoka ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zinasema pamoja na Bahanuzi ambaye alifunga mabao sita kwenye michuano hiyo, pia kiungo Athuman Iddi 'Chuji' ameitwa Stars itakayocheza mechi ya kirafiki hivi karibuni.
TFF imepeleka maombi kwenye nchi nne kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki Agosti 8.

Kocha wa Stars, Kim Poulsen, amemrudisha Chuji kundini baada ya kupotea kikosini humo msimu uliopita kiasi cha wengi kumfikiria kuwa zama zake za kucheza soka zimefikia ukingoni.

Mara ya mwisho Chuji kuitwa Stars ilikuwa mwaka 2010 wakati alipoteuliwa na kocha wa zamani wa timu hiyo, Jan Poulsen.

Habari ambazo Mwanaspoti imezipata zilisema kuwa Kim ameshaandika majina ya Chuji na Bahanuzi katika daftari lake akimaanisha wachezaji hao watakuwemo katika kikosi chake kijacho ambacho kitacheza mechi za kufuzu Kombe la Dunia.

Bahanuzi alifanya makubwa na Yanga licha ya ukweli kuwa alikuwa anacheza kwa mara ya kwanza katika mashindano ya kimataifa.

Akizungumza na Mwanaspoti, mchezahi huyo aliyesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar ametoboa siri ya mafanikio ya kuibuka mfungaji bora kwenye Kombe la Kagame kuwa ni kumtanguliza Mungu mbele kwa kila jambo analolifanya.

Bahanuzi aliyepachika mabao sita kwenye mashindano hayo, aliliambia Mwanaspoti jana Jumatatu kuwa kila jambo analolifanya anamtanguliza Mungu.

"Mungu ndiyo siri yangu ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya Kagame," alisema Bahanuzi anayevaa kiatu namba 10.

"Nimezaliwa na kulelewa katika mazingira ya dini, ninamwamini zaidi mwenyezi Mungu kuliko chochote."

Staa huyo aliyeichezea pia Ocean View ya Zanzibar kabla ya kutua Mtibwa, haamini kama kuna uchawi kwenye soka.
"Nafikiri ni imani potofu za watu wachache, nimejipanga kufanya vizuri zaidi na si kuishia hapa," alisema.

Katika hatua nyingine, alisema anaamini kocha wa Stars, Kim Poulsen, ameona uwezo wake na kumjuisha kwenye kikosi chake.

"Tuna tatizo la ufungaji kwenye timu ya Taifa, naamini nitakapopewa nafasi kwenye kikosi nitaendeleza haya niliyofanya Kagame," alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post