Ajali ya mv Skagit, urais 2015 vyaitesa
UPEPO wa mabadiliko ya kisiasa uliozikumba nchi nyingi duniani,
unaelekea kukiathiri Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho sasa kinahaha
kujinusuru kung’oka madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Chama tawala hivi sasa kina msuguano mkubwa wa kiuongozi ambapo baadhi
ya viongozi wake wamekuwa wakimshutumu Katibu Mkuu, Willison Mukama,
kwa kukwamisha mikakati ya kujiimarisha na kurejesha matumiani
yaliyofifia miongoni mwa wanachama wake.
Licha ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, wiki hii kukanusha
kutokuwa na msuguano na Mukama, makada wa chama hicho wamelidokeza
Tanzania Daima Jumapili, kuwa vita ya makundi ya kuwania uongozi na ile
ya ufisadi inakitesa chama hicho.
Mnyukano wa kisiasa unaonekana wazi hivi sasa ni baina ya Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, dhidi ya kundi
linalomuunga mkono aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, anayetajwa
kutaka kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Wakati hali ya mambo ikionekana kutokuwa nzuri ndani ya chama hicho,
nguvu kubwa sasa imehamishiwa kwenye Bunge kwa lengo la kuwadhibiti
wabunge wa CHADEMA ambao wanaelezwa kutishia uhai wa chama hicho.
Makada wa CCM wamedokeza kuwa wamebaini wabunge wa CHADEMA mwaka
2005-2010 walilitumia vizuri Bunge kujenga hoja za msingi ambazo
ziliwasaidia kujijenga na hatimaye kupata wabunge 22 wa majimbo kutoka
watano.
Waliongeza kuwa kutokana na kubaini jambo hilo, chama hicho kimeamua
‘kuzishughulikia’ hoja zinazotolewa na CHADEMA bila kujali kama zina
masilahi kwa taifa au la.
Inadaiwa kuwa viongozi wa Bunge nao wamepewa maelekezo ya kukisaidia
chama chao hasa wanapoona kuna hoja zinazoelekea kuwapatia umaarufu
wabunge wa CHADEMA.
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa pamoja na maelekezo hayo
baadhi ya viongozi wa Bunge wameonekana kushindwa kukisaidia chama
tawala kwa sababu ya kutozijua ipasavyo kanuni, hivyo kutumia ubavu
kukataa jambo linalotolewa na wapinzani, hivyo kuwaongezea umaarufu.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, anatuhumiwa kutoa fursa zaidi kwa
wabunge wa CCM kurudia maneno ya dharau na lugha ya kuudhi dhidi ya
wapinzani.
Kiongozi huyo pia juzi alionesha ‘ukada’ wake pale alipojifanya
kukosea jina la Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Kamili, kwa kumuita Rose
Kamili Slaa, ilhali akijua mbunge huyo alishatarikiana na Dk. Slaa.
Hata hivyo CCM hivi sasa pia kinakabiliana na wakati mgumu wa
kushutumiwa kushindwa kuwachukulia hatua watendaji wake wanaobainika
kufanya uzembe katika shughuli zao za kila siku.
Ajali ya mv Spice Islanders iliyotokea mwaka jana na mv Skagit
iliyotokea wiki iliyopita inadaiwa ilichangiwa na uzembe wa wataalamu
kwa kushindwa kukagua ubora wake.
Serikali ya CCM pia inalaumiwa kwa kushindwa kuwa na vifaa vya kisasa
vya uokoaji licha ya kila mara kukumbwa na matukio ya ajali za baharini
na ziwani.
Katika ajali hizo mbili za majini zilizopoteza maisha ya Watanzania
zaidi ya 400, serikali ya CCM inalaumiwa kwa kushindwa kusimamia sheria
za usafiri wa majini na kuficha taarifa ya uchunguzi wa ajali ya awali.
Mmoja wa wabunge wa CCM ambaye jina lake limehifadhiwa, aliilaumu
serikali kwa kuunda tume kuchunguza ajali ya mv Bukoba na Spice
Islanders, lakini haikutoa matokeo ya uchunguzi huo.
“Serikali iliunda tume kuchunguza ajali ya awali ya mv Spice Islanders
na mv Bukoba lakini ikaficha matokeo ya uchunguzi wake. Leo imetokea
ajali nyingine na binafsi naamini kama matokeo ya uchunguzi wa awali
yangetolewa, bila shaka ajali ya juzi ingeepukika,” alisema kada huyo.
Kufichwa kwa matokeo ya uchunguzi wa ajali za awali za majini,
kumeelezwa kuwa ndiyo sababu ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuzima
hoja za wabunge wa kambi ya upinzani walioungana na wabunge wote wa
Zanzibar kutaka kujadili ajali ya mv Skagit iliyosababisha vifo vya
zaidi ya watu 150
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz
Post a Comment