MICHUANO ya Kombe la Kagame imemalizika wikiendi iliyopita kwa Yanga kutwaa ubingwa baada ya kuifunga Azam mabao 2-0.
Hapa ni wachezaji 11 wanaounda kikosi cha kwanza cha michuano ya Kagame yaani 'First Eleven'.
Vigezo vilivyotumika kuwateua wachezaji hao ni pamoja na mchango binafsi kwenye timu zao. Hii ni kwa mujibu wa Mwanaspoti.
Said Ndikumana, Atletico
NI kipa bora wa mashinadno ya Kombe la Kagame. Amefungwa mabao manne sawa na Yaw Berko wa Yanga aliyeumia robo fainali. Licha ya kufungwa mabao hayo, ameonyesha uwezo mkubwa na kufikisha timu yake robo fainali.
Shomari Kapombe, Simba
NI tegemeo kwenye kikosi cha Simba kwa sasa. Kiraka huyo anazimudu nafasi zote za ulinzi tena kwa kiwango cha juu. Amefunga bao moja na kutoa pasi iliyozaa bao lililozamishwa na Abdallah Juma dhidi Ports ya Djibout.
Erasto Nyoni, Azam
BEKI aliyepewa majukumu mazito na kuyafanyia kazi ipasavyo. Alitakiwa kulinda lango na pia kupandisha mashambulizi kusaka bao. Alitoa pasi moja ya bao lililofungwa na John Boko dhidi ya Simba.
Mbuyu Twite, APR ya Rwanda
NI vigumu kumtoa kasoro kiuchezaji. Amekamilika. Ufupi wake haumzui kuruka na kucheza mipira ya juu. Anaweza akawa beki bora wa mashindano ya Kagame.
Kelvin Yondan, Yanga
KUTUA kwake Yanga kumeifanya safu ya ulinzi kuimarika tofauti na misimu iliyopita. Beki ambaye ameonyesha uwezo wa kukaba na kuanzisha mashambulizi. Alitoa pasi ya bao lililozamishwa na Said Bahanuzi mechi ya fainali.
Athuman Idd, Yanga
AMERUDI kwenye fomu na kuacha maswali mengi kwa mashabiki wa soka. Alikuwa na majukumu mawili mazito. Kutibua na kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza. Amefanya kazi hiyo kwa mafanikio makubwa.
Salum Abubakar, Azam FC
YOSSO huyo ameonyesha uwezo mkubwa wa kuchezesha timu. Ni tegemeo kwa siku zijazo katika kikosi cha Taifa Stars. Alipiga pasi 71 kwenye mechi ya fainali dhidi ya Yanga. Pasi 55 zilifika kwa walengwa huku 16 zilienda fyongo.
Haruna Niyonzima, Yanga
KIUNGO ambaye kila timu inataka kuwa naye. Kutokana na ubora wake wa kupiga pasi za mwisho. Alitoa pasi tatu za mabao yaliyozamishwa na Bahanuzi mawili na jingine na Kiiza. Mchango wake aliwafanya Kiiza na Bahanuzi kung'ara.
Said Bahanuzi, Yanga
MFUNGAJI bora wa mashindano ya Kombe la Kagame. Amepachika mabao sita na kutoa pasi ya bao lililofungwa na Hamis Kiiza.
John Boko, Azam FC
BOKO alifunga mabao matano yaliyoifikisha Azam fainali ikishiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Kagame. Mfungaji Bora huyu wa Ligi Kuu Bara amethibitisha kuwa hakubahatisha na makali hayo kuyahamishia mashindano ya Kagame.
Hamis Kiiza, Yanga
KIIZA amefunga mabao matano sawa na Boko. Pia ametoa pasi nne za mabao yaliyofungwa na Said Bahanuzi matatu na Nizar Khalfan.
KOCHA BORA; Tom Saintfiet
Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet ndiye kocha bora wa mashindano ya Kagame. Ametetea taji na kulibakiza Tanzania kwa mara ya pili mfululizo. Amepoteza mechi moja kati ya sita na kutoa wachezaji watano kuunda kikosi bora cha michuano hiyo.
Chanzo:- Mwanasports
Post a Comment