WAKATI kampeni za wagombea uongozi katika uchaguzi mdogo wa klabu ya
Yanga zikihitimishwa jioni ya jana, Yusuf Manji anayewania nafasi ya
uenyekiti amesema ni
heri ya kufa kuliko Yanga kufungwa mabao 5-0 na Simba chini ya uongozi
wake.
Manji aliyewahi kuwa mfadhili na mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, alisema
kipigo cha kiwango hicho ni matokeo ya kushindwa kazi kuanzia viongozi,
wachezaji hadi benchi
la ufundi, hivyo kuondoa maana, hadhi na thamani ya viongozi.
Alisema kwa kulitambua hilo, ikitokea Yanga chini ya uongozi wake kufungwa tena
5-0 na Simba, ataomba heri afe kuliko kujionea hasira na huzuni za wanachama,
wapenzi na mashabiki kwani uongozi utakuwa hauna maana ya kuwepo.
“Nikipewa kura, kwa kushirikiana na wenzangu tutajenga kikosi bora,
sitakubali kuona Yanga ikifungwa tena na Simba 5-0, ni heri nife kuliko
uongozi kupata aibu ya kiwango hicho,” alisema Manji katika mahojiano
maalumu na Tanzania Daima hivi karibuni.
Alisema ingawa kufungwa ni sehemu ya mchezo, njia pekee ya kuzuia kipigo cha aibu,
ni kusajili nyota bora, kuwapa masilahi ya kutosha pia wakiwa chini ya makocha bora
hadi wakose kisingizio cha kufungwa vibaya kama ilivyotokea Mei 6, 2012.
Manji alisema, kipigo hicho kwa kiasi kikubwa kilitokana na wachezaji
kujikatia tamaa kutokana na mazingira magumu yaliyokuwa yakiwazunguka,
hivyo hatakubali hilo
litokee kwenye uongozi wake kama atashinda katika uchaguzi wa leo.
Alisema, kama timu itaundwa na nyota mahiri, kulipwa maslahi bora tena chini
ya makocha mahiri, pia umoja na mshikamano ukitamalaki kwa wanachama
hadi kwenye uongozi, vipigo vya aibu kwa Yanga itabaki kuwa historia.
Wakati Manji akisema hayo, mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Edgar
Chibura, ameahidi kuijenga klabu hiyo kiuchumi iondokane na aibu ya
utegemezi licha ya ukongwe wake wa zaidi ya miaka 70 tangu kuasisiwa
kwake 1935.
Alisema kama atashinda, atajitahidi kushirikiana na viongozi wenzake
na wanachama kwa ujumla akiamini hakuna kisichowezekana chini ya misingi
imara ya kujitegemea kupitia vyanzo vya uhakika vya mapato.
Chibura alisema hilo likifanyika pamoja na uwazi katika mapato na
matumizi ya klabu, Yanga itapiga hatua kubwa kiuchumi hivyo kuwavutia
wadhamini zaidi wa kushirikiana na Kampuni ya Bia Tanzania TBL, kupitia
bia ya Kilimanjaro. Zaidi ya hilo, Chibura ambaye ni mwalimu kitaaluma,
aliongeza atajitahidi kusimamia mabadiliko ya katiba ya klabu hiyo
kupitia viongozi wa matawi
yote nchini ambao watakuwa wakiwasilisha mapendekezo ya wanachama.
Aidha, ataboresha kitengo cha habari kwa kuongeza maofisa, kuanzishwa
kituo cha televisheni cha Yanga, kuanzishwa kituo cha redio, pia kituo
cha utalii kitakachohusisha masuala ya klabu hiyo tu tangu kuasisiwa
1935.
Naye John Jembele anayewania nafasi hiyo ya uenyekiti, anaamini hakuna
wa kuikomboa Yanga kiuchumi, isipokuwa mwanachama wa klabu hiyo mwenye uchungu wa kweli, hivyo amewataka kutofanya makosa
katika uchaguzi wa leo.
Alisema, umasikini wa klabu hiyo kiuchumi, ni matokeo ya kutotumiwa
vizuri mtaji wa wanachama, wakitumiwa ipasavyo wataweza kuijenga
klabu hiyo kiuchumi, hivyo muhimu ni kuoneshwa njia ya kupita.
Alisema, atapigania pia suala la uwazi wa mapato na matumizi ya klabu
hiyo kwani jambo hilo limekuwa chanzo cha mivutano mingi, hivyo
atahakikisha suala hilo linakuwa wazi kuepuka majungu ambayo huzaa
makundi.
Kila mgombea wa nafasi hii, amejinadi hivyo kazi ya wanachama kufanya
maamuzi ya nani anafaa kuchaguliwa kwenye nafasi ya uenyekiti kuziba
nafasi ya Lloyd Nchunga, aliyejiuzulu kwa shinikizo la wanachama.
Atakayeshinda kwenye nafasi hii ya juu, atakuwa mwenyekiti wa 18 tangu
mwaka 1935; akitanguliwa na Athumani Mwinyichande, Omari Mussa,
Kondo Kipwata, Mohamed Maboski, Saidia Msafiri, Salum Assanawi, Daud
Aziz na Bille Bandawe.
Wengine ni Juma Shamte, William Bocco, Jabir Katundu, Rashid Ngozoma
Matunda, Tarimba Gullam Abbas, Francis Kifukwe, Imani Mahugila Madega na
Lloyd Nchunga.
Wagombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti, ni Clement Sanga, Stanley Kevela
Yono na Ayoub Nyenzi ambao kila mmoja ameeleza nini atafanya kama
atachaguliwa kurithi nafasi iliyoachwa na Davis Mosha.
Aidha, kuna wagombea 14 ambao watachuana kuwania nafasi nne za Ujumbe
wa Kamati ya Utendaji iliyoachwa wazi na Ally Mayay, Mzee Yusuph,
Charles Mgondo waliojiuzulu na Theonest Rutashoborwa aliyefariki dunia.
Wagombea wa nafasi hiyo ni Abdallah Bin Kleb, Ramadhani Said, Mussa
Katabalo, George Manyama, Peter Haule, Justine Baruti, Abdalla Mbamba,
Abdallah Sharia, Aaron Nyanda, Omary Ndula, Beda Simba, Edger Fongo,
Jumanne Mwammwenywa na Lameck Nyambaya.
Akizungumzia uchaguzi huo, Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga,
Francis Kaswahili alisema hakuna mabadiliko kwani taratibu zimekwenda
vizuri, uhakiki wa kadi utafanyika kati ya saa moja asubuhi hadi saa
sita mchana.
Uchaguzi huu unafanyika kuziba nafasi sita katika uongozi ulioingia
madarakani Julai 18, 2010, baada ya watano kujiuzulu na mmoja
kufariki dunia mapema mwaka huu
Post a Comment