MISAADA inayotolewa na kada wa CCM na mfanyabiashara maarufu
hapa nchini, Mustafa Sabodo, kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), sasa inaonekana kuwagawa makada wa chama hicho tawala.
Baadhi ya makada wamekuwa wakitaka Sabodo atimuliwe kwenye chama hicho
kwa madai ni msaliti na mwenye lengo la kuiimarisha CHADEMA
inayoonekana kutishia utawala wa CCM.
Miongoni mwa makada wa CCM ambao kwa wakati tofauti walitaka Sabodo
atimuliwe ndani ya chama hicho ni pamoja na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa
Morogoro, Stephen Mashishanga na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa
Shinyanga, Khamis Mgeja.
Harakati za makada hao kutaka Sabodo atimuliwe jana ziligonga mwamba
baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape
Nnauye, kuunga mkono hatua za Sabodo kukisaidia CHADEMA.
Nape aliwataka Watanzania wengine waige mfano huo, kwakuwa itikadi za kisiasa haziwezi kuwakwamisha wananchi wasishirikiane.
Katika taarifa yake iliyowekwa katika mtandao wa kijamii wa Daily
Nkoromo, Nape alisema kuwa haoni tatizo kwa Sabodo kukisaidia CHADEMA
hasa katika suala la upatikanaji wa visima kwa kile alichoeleza
watakaonufaika na visima hivyo ni Watanzania wote pasipo kujali vyama
vyao.
Kauli hiyo ya Nape ambaye ndiye msemaji wa CCM, inapingana na kauli za
makada wengine ndani ya chama hicho juu ya mtazamo wa kuendelea
kumkumbatia Sabodo anayejipambanua na wafanyabiashara wengine katika
kuhakikisha mageuzi ya kweli yanapatikana nchini.
Nape alisema uamuzi wa kutoa ufafanuzi huo ni kutokana na maswali
mbalimbali yanayoelekezwa kwake na watu tofauti juu ya hatima ya
michango inayotolewa na Mustapha Sabodo kwa CHADEMA, pamoja na matamshi
yake dhidi ya CCM.
“Kuna watu wengi wanauliza nini maoni yangu juu ya uamuzi wa mzee Sabodo kusaidia vyama vya upinzani na hasa CHADEMA.
Kimsingi sioni tatizo katika hili, la muhimu ni yeye kuendelea kuwa
mwanachama muaminifu wa CCM,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Nape.
Alisema kama kuna mwanachama wa CCM atakayekuwa na shaka juu ya
uungwana huo wa mzee Sabodo itampasa arejee maamuzi ya serikali ya
kuruhusu mfumo wa vyama vingi na aangalie utaratibu wa kuvipatia vyama
ruzuku, kwa kile alichoeleza kuwa ulikuwa na lengo la kudumisha umoja
kwa kuviwezesha kufanya kazi ya kuikosoa serikali na kuhimiza maendeleo.
Aliongeza kuwa wenye fikra ya kuona mzee Sabodo anakisaliti Chama Cha
Mapinduzi watakuwa si wanasiasa wa kweli na Wana CCM waaminifu
wanaoitakia mema Tanzania.
“Hivi kwanini tunataka kuwafikisha Watanzania mahali wasisaidiane
kisa siasa!....wapo wanaohoji kwanini mzee Sabodo ametoa visima kwa
CHADEMA? Sasa najiuliza visima vitakapoanza kufanya kazi watumiaji
wataulizwa itikadi zao au kila mwananchi ana uhuru wa kutumia? Tatizo
hapa ni nini? Narudia sioni tatizo kwa mzee Sabodo kusaidia vyama vya
upinzani ili mradi pesa hizo ni zake!" alisema Nape.
Mzee Sabodo licha ya kuwa ni kada wa CCM mara nyingi amekuwa
akijitokeza wazi wazi kuisaidia CHADEMA katika masuala mbalimbali ya
kifedha.
Miongoni mwa misaada yake ni pamoja na kuahidi kuchimba visima katika
majimbo yote yanayoongozwa na CHADEMA, ikiwa ni pamoja na kuahidi
kuwapatia jengo lenye ofisi za kisasa zitakazoendana na hadhi ya chama
hicho.
Mbali na ahadi hiyo, mzee Sabodo aliwahi kukaririwa akisema anatamani
CCM ishindwe katika uchaguzi wa mwaka 2015 na kwamba yupo tayari
kumchangia mgombea urais kupitia CHADEMA.

Post a Comment