Rushwa bungeni moto
• Mbatia sasa atishia kuwataja wakati wowote
SAKATA la wabunge kuhongwa kwa nia ya kuyatetea makampuni ya mafuta
na menejimenti ya Shirika la Ugavi wa Umeme Nchini (TANESCO) linazidi
kuchukua sura mpya kadiri siku zinavyosonga mbele.
Siku moja baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo, kuvurumisha makombora dhidi ya wabunge hao pasipo kuwataja kwa
majina, Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia, ameibuka na jipya kuhusu
sekeseke hilo.
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi
amesema wakati wowote kuanzia sasa atawataja kwa majina wabunge wote
waliopokea rushwa kwa lengo la kuwalinda viongozi wakuu wa TANESCO
wanaokabiliwa na tuhuma za kulihujumu shirika hilo.
Mbali ya hilo, Mbatia amemshutumu Spika wa Bunge, Anne Makinda, kwa
kuwalinda wabunge hao aliodai wamehongwa na mafisadi hao wa TANESCO.
Kauli hiyo aliitoa jana mkoani hapa alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari kuhusu uamuzi wa Spika Makinda kuridhia kuivunja Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na kuiagiza Kamati ya Maadili, Haki
na Madaraka ya Bunge kuwachunguza watuhumiwa.
Mbatia alisema Spika anao ushahidi wa kutosha wa majina ya wabunge
waliohongwa kwani Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,
aliliambia Bunge kuwa wana ushahidi wote.
Alibainisha kuwa ushahidi huo ndiyo uliomfanya Spika Makinda akaridhia
kuivunja kamati husika na kuipa kazi Kamati ya Maadili, Haki na
Madaraka ya Bunge kuwachunguza watuhumiwa.
Kiongozi huyo pia alisema hawana imani na kamati iliyopewa jukumu la
kuwachunguza wabunge watuhumiwa wa rushwa kwa sababu inaundwa na baadhi
ya watuhumiwa.
“Tunamtaka Spika ajitakase kwanza kwa kuwaengua wajumbe ambao ni
watuhumiwa, kinyume na hapo hatuna imani na kamati hiyo,” alisema.
Alisema Bunge ni chombo kitukufu na ili utukufu huo uonekane ni lazima
maamuzi yanayofanywa huko yaheshimiwe, hivyo akapendekeza kuwa mbali na
Bunge kutumia kanuni zake kuwahukumu wabunge watuhumiwa au linaweza
kuiga maamuzi ya baadhi ya mabunge ya Jumuiya ya Madola.
Alitolea mfano mabunge ya Uingereza na India, ambapo Bunge la
Uingereza limewahi kuwatimua na kuwavua ubunge wabunge 57 na India
imefanya hivyo kwa wabunge 11 kutokana na kujihusisha na vitendo vya
rushwa.
“Hivyo basi tunatoa wito kuwa mbunge yeyote wa chama chochote
anayeamini kwa dhamira yake kwamba ni mjumbe wa Kamati ya Nishati na
Madini na anafanya biashara na TANESCO kwa njia ya maslahi binafsi
halafu anatumia rushwa kuwashawishi wabunge wengine au amepokea rushwa
kutetea uovu ni bora akajiondoa mwenyewe kwenye ubunge kabla ya
kuabishwa na Bunge,” alisema.
Mbatia aliongeza kuwa wanamtaka Spika awe amewataja kwa majina wabunge
waliopokea rushwa si zaidi ya wiki moja ili Bunge liwachukulie hatua,
huku akiwaomba wabunge wenzake bila kujali itikadi za vyama vyao wafanye
azimio la Bunge ili wahusika mbali na kuvuliwa ubunge wafungwe jela
miaka mitano.
“Kwa mujibu wa sheria namba 3 kifungu cha 32 ya Haki, Kinga na
Madaraka ya Bunge ya mwaka 1988, mbunge anakatazwa kuzungumza, kuhoji,
kupiga kura au kutetea jambo lolote bungeni ambalo litakuwa na ushawishi
wa maslahi yake binafsi kutoka nje na kwamba adhabu yake ni kifungo
kisichopungua miaka mitano jela,” alisema Mbatia.
Mwenyekiti huyo ambaye alifuatana na mbunge mwingine wa chama hicho wa
Kasulu Mjini, Moses Machali, alimtaka Spika kuzitaja kamati nyingine
ambazo wajumbe wake wanatuhumiwa kwa rushwa.
Mbali na Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa, kamati nyingine
zinazodaiwa baadhi ya wabunge wake kujihusisha na vitendo vya rushwa ni
ile ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) chini ya Zitto Kabwe na Hesabu
za Serikali za Mitaa (LAAC) inayoongozwa na Augustine Mrema.
Nyingine ni ya Miundombinu chini ya Peter Serukamba, Viwanda na
Biashara ya Mahmoud Mgimwa na Ardhi, Maliasili na Mazingira chini ya
James Lembeli.
“Tatizo la nchi yetu ni kuchelewa kufanya maamuzi wakati muafaka.
Tukilitakasa Bunge kwa kuwashughulikia wabunge waliokula rushwa ni wazi
hata serikali itaanza kuwachukulia hatua wale ambao tumekuwa
tukiwalalamikia kujihusisha na rushwa,”
Mbatia aliwatahadharisha wabunge wa chama chake kuwa kama kuna yeyote aliyechukua rushwa katika sakata hilo, ajiengue mapema.
Mbatia pia alitumia mwanya huo kuwatia matumaini wabunge waadilifu
wenye misimamo mikali ya kuikosoa serikali kuwa wasiogopeshwe na sakata
hilo ambalo alidai serikali italitumia kuwanyamazisha wabunge kwa vile
walikuwa wakiikosoa.
Ingawa Mbatia hakuwataja kwa majina wabunge hao, habari ambazo Tanzania Daima inazo zinaeleza kuwa wabunge
zaidi ya sita wanatajwa kuwa katika kundi la wale wanaotuhumiwa kuwatetea mafisadi wa TANESCO.
Inadaiwa wabunge hao walipewa fedha na kampuni za mafuta ili
washinikize kung’olewa kwa Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo Eliakim Maswi wanaodaiwa kuipa zabuni ya kusambaza
mafuta kwa TANESCO kampuni ya Puma Energy.
Habari zinaeleza kuwa, wabunge hao wako katika Kamati ya Hesabu za
Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Kamati ya
Miundombinu, Kamati ya Viwanda na Biashara na Ardhi, Maliasili na
Mazingira.
Gazeti hili limedokezwa kwamba wabunge takriban wote isipokuwa mmoja
tu, walioko katika orodha hiyo wanatokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Chanzo:- Tanzania daima
Post a Comment