TAARIFA RASMI YA SERIKALI KUHUSU KUSUDIO LA WALIMU KUGOMA
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Peniel
Lyimo (mrefu) akibadilishana mawazo na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi
Ombeni Sefue
--

SERIKALI kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi leo, Ijumaa, Julai
27, 2012 majira ya saa tisa alasiri, imepokea notisi ya saa arobaini na
nane (48) ya kusudio la walimu wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania
(CWT) kugoma kuanzia Jumatatu tarehe 30 Julai 2012 saa moja na nusu
asubuhi.
Kabla ya notisi hii kutolewa, Serikali imekuwa
ikifanya jitihada nyingi za kujadiliana na viongozi wa CWT kuhusu jinsi
ya kuboresha maslahi ya walimu kwa nia ya kumaliza suala hili kwa
maelewano kwa kutumia vyombo na ngazi mbali mbali za kisheria.
Kwa sasa, shauri hili liko Mahakama Kuu Divisheni ya
Kazi na leo hii siku ya Ijumaa tarehe 27 Julai, 2012 majira ya saa sita
mchana pande zote mbili zilifika Mahakamani, na Mahakama ikaamuru
kwamba pande zote zikamilishe maelezo yao ifikapo siku ya Jumanne tarehe
31 Julai, 2012 saa sita mchana, ili kuiwezesha Mahakama kuendelea
kusikiliza shauri hilo na hatimaye kutoa uamuzi.
Kwa hiyo, Mgomo huu siyo halali kwa sababu shauri hili bado liko Mahakamani.
Kwa
msingi huo hatua ya CWT kutoa notisi ya kuanza kwa mgomo kabla ya
kukamilika kwa shauri hili ni kukiuka taratibu halali za Kimahakama
ambazo kila mmoja anawajibika kuziheshimu.
Serikali inapenda kuwafahamisha walimu wote kuwa
kujihusisha na mgomo huu ni kwenda kinyume cha Sheria, Kanuni na
Taratibu za kazi. Hivyo, walimu wanapaswa kupima madhara ya mgomo huu
usiokuwa halali na Serikali inawataka walimu kupuuza mgomo huo na
kutokujihusisha nao. Walimu wote wanatakiwa waendelee na kazi kama
kawaida.
Peniel M. Lyimo
KAIMU KATIBU MKUU KIONGOZI
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
27 Julai, 2012
Post a Comment