Takriban wakimbizi tisini waliokuwa wamekwama
katikati ya bahari ya Mediterranea kwa siku nne, hatimaye wameokolewa,
kwa mujibu wa shirika la habari la Italia pamoja na jamaa za wale
waliokuwa wamekwama.
Mmoja wa wale waliokuwa kwenye boti hiyo
aliwasiliana na idhaa ya kisomali ya BBC kusema kuwa boti yao ilikwama
baada ya injini kuisha mafuta na vile vile walikuwa wameishiwa na maji
ya kunywa.
Aliongeza kuwa walikuwa wameondoka mji mkuu wa Libya Tripoli, kuelekea pwani ya Italia.
Wahamiaji hao waliokolewa katika mpango wa pamoja kati ya maafisa wa Italia na Libya.
Mapema mwezi huu watu 54 walifariki kutokana na
kiu baada ya kuishiwa na maji wakiwa njiani kutoka Libya kuelekea Italia
vile vile kwa Boti.
Wahamiaji waliookolewa wamerejeshwa nchini Libya kulingana na taarifa za shirika la habari la Ansa nchini Italia.
Jamaa za wale waliokuwa kwenye boti hiyo walithibitishia BBC kuwa walipatikana.
Wahamiaji wengi kutoka Libya hufariki kila mwaka
katika safari zao hatari kuelekea katika kisiwa cha pwani ya Italia cha
Lampedusa.
Mmoja wa wahamiaji hao, walisema kuwa walijaribu
kuwasiliana na walinzi wa baharini lakini wakapewa nambari nyingine ya
simu kupiga ingawa hawakufanikiwa kupata jibu lolote.
Zaidi ya wasomali milioni moja wametoroka nchi
yao tangu mwaka 1991, wakati Siad Barre alipompindua rais aliyekuwa
mamlakani, na tangu hapo vita havijawahi kuisha nchini Somalia
Chanzo:- BBC Swahili
Post a Comment