OCHIENG KUPATA ITC YAKE LEO

OCHIENG KUPATA ITC YAKE  LEO

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe kushoto akimkabidhi jezi Paschal Ochieng baada ya kusaini mkataba na klabu hiyo. Katikati ni Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange 'Kaburu'

SIMBA SC imemaliza utata wa usajili wa beki wake wa kimataifa wa Kenya, Paschal Ochieng kutoka AFC Leopard ya Kenya na sasa hakuna shaka atachezea Wekundu hao wa Msimbazi msimu mpya.
Habari za ndani kutoka Simba SC, zimesema kwamba, Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, chini ya Mwenyekiti wake, Zacharia Hans Poppe ilikutana na klabu hiyo bingwa ya zamani ya Kenya na kumaliza tofauti zao.
Leopard ilikuwa inadai Simba imemsajili Ochieng kinyume na utaratibu, kwani bado ana mkataba na klabu yake hiyo wa miezi sita.
Kwa sababu hiyo, Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ya beki huyo wa zamani wa Yanga, inatarajiwa kuwasili nchini kuanzia leo.
Ochieng ni miongoni mwa wachezaji watano wa kigeni watakaokuwamo kwenye kikosi cha Simba cha msimu ujao, wengine wakiwa ni kiungo Mussa Mudde, ambaye hata hivyo inaelezwa anaweza kukatwa akasajiliwa Keita wa Mali, washambuliaji Felix Sunzu kutoka Zambia, Emmanuel Okwi kutoka Uganda na Daniel Akuffo kutoka Ghana.

Post a Comment

Previous Post Next Post