BALOZI SEIF IDD ACHARUKA AKUSUDIA KUITAKA WIZARA YA ARDHI ZANZIBAR KUWAJIBIKA.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akionyeshwa ramani ya eneo la chuo cha sayansi ya Afya Mbweni na msimamizi wa ujenzi wa chuo hicho Bw. Waziri Juma ambalo limeshapimwa kwa ajili ya ujenzi wa makazi.
Jengo la Bw. Abdulla Ali Khamis ambalo limo ndani ya eneo la chuo cha Sayansi ya Afya Kilichopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Polisi wa Nchi wanachama wa Mataifa ya Kusini, Mashariki na Kati mwa Afrika SADC nje ya Ofisi yake baada ya kufanya nao mazungumzo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimpongeza mwanachama mpya aliyejiunga katika Jumuiya ya wachangiaji damu kwa Hiari Zanzibar Bibi Maryam Mohd akichangia damu kwa mara ya kwanza katika kituo cha damu salama Kiliopo Sebleni Mjini Zanzibar.
Jengo jipya la Bohari Kuu ya Wizara ya Afya linaloendelea kujengwa ndani ya eneo la kiliokuwa kiwanda cha Sigara Maruhubi Mtoni.(Picha na Saleh Masoud Mahmoud – OMPR- ZNZ).
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anakusudia kumuandikia Barua Waziri anayesimamia masuala ya Ardhi Zanzibar kumtaka kufuta mara moja hati ya umiliki wa Viwanja vya nyumba ambavyo vimo ndani ya eneo la Chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni.
Balozi Seif ametoa kauli hiyo wakati akiangalia eneo la Chuo hicho ambalo limevamiwa kwa ujenzi, wakati wa ziara yake katika Taasisi zilizomo ndani ya Sekta ya Afya ikiwa ni mwanzo wa ziara zake kuangalia utendaji wa Wizara za Serikali pamoja na changamoto zinazozikabili Wizara hizo.
Balozi Seif akionyeshwa kukasirishwa kwake na tabia ya baadhi ya watu kukaidi maamuzi ya Serikali pamoja na Maagizo ya Mahakama ya kuhodhi ardhi amesema Taifa halitakuwa na Maendeleo kama Jamii ikijali zaidi Ubinafsi.
Ameagiza kusitishwa mara moja maendeleo ya ujenzi wa nyumba moja  ambayo tayari ina mgogoro ulioko mahakamani pamoja na kuzuiwa kwa ujenzi wowote kwa wale waliomilikishwa viwanja saba ndani ya eneo hilo la chuo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amefahamisha kwamba Serikali haikusudii kufanya ubabe kwa raia wake lakini kamwe haitasita kumchukulia hatua za kisheria Raia atakayeonyesha dharau au jeuri dhidi ya Serikali.
Ameoupongeza Uongozi wa Wizara ya Afya kupitia Chuo hicho kwa juhudi zake za kuendeleza Majengo yatakayokidhi mahitaji ya wanafunzi kwa siku za baadae.
Mapema Msimamizi wa Ujenzi wa Chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni Ndugu Waziri Juma alimueleza Balozi Seif kwamba Eneo hilo lilikuwa  likimilikiwa kihalali na Chuo cha Ufundi cha Mbweni tokea mwaka 1962.
Ndugu Waziri  alisema Chuo cha Sayansi kililazimika kisheria kuomba eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa chuo chake ambapo baadaye uongozi wa chuo hicho ukaamua kujenga ukuta baada ya kuanza dalili za uvamizi wa eneo hilo.

Post a Comment

Previous Post Next Post