HILI NDIO TAMKO LA CHADEMA KUKANUSHA SHUTUMA ZA CUF KUFANYIWA VURUGU NA CHADEMA


Ndugu
wananchi na wanahabari,
Siku ya terehe 27 Alhamisi Septemba 2012 chama cha wananchi CUF walitoa
taarifa ya malalamiko kwa vyombo vya habari na mitandao kuwa wanachama
wa CHADEMA wamewafanyia vurugu kwa kuwapiga mawe na kuwa jambo hilo
limehamasishwa na viongozi wa chama katika mkoa wa Arusha pamoja na Mhe
Godbless Lema.
Wote tunafahamu kuwa siku hiyo hiyo katika viwanja vya soko la Kilombero
wafanyabiashara ndogo ndogo walikuwa wamevamia na walikuwa wakijigawia
maeneo, baada ya eneo la awali walilopewa la viwanja vya NMC kushindwa
kuwachukua wafanyabiashara wote na halmashauri kushindwa kutoa majibu
kwa wafanyabiashara hawa ambao waliwaambia wote waende NMC.
Kwanza tunapenda kutoa pole kwa viongozi wa CUF kwa jambo hili
lililowapata.

Wao
kama watu na Watanzania wenzetu tunawapa pole sana.
Pili, CHADEMA inakanusha kuhusika na jambo hili. Hii si tabia ya CHADEMA
na kamwe haiwezi kuwa tabia ya CHADEMA kufanya siasa chafu za namna
hiyo. CHADEMA tunajali sana amani na upendo, na hii ndiyo tabia na
makuzi yetu Watanzania.
Katika mazingira haya, CHADEMA tunachukua fursa hii kuvikaribisha vyama
vyote mathalani CUF, Arusha ni yetu sote na tutumie demokrasia vizuri
kufanya kazi nzuri ya siasa kwa ajili ya kusababisha na kuleta matumaini
kwa Watanzania hawa ambao serikali ya chama cha mapinduzi imeshindwa
kuwaletea.



CHADEMA
hatuna shida na ushindani wa kisiasa katika mazingira ya kidemokrasia
kwa maana ndio wakati pia wa wananchi kupima na kujua nani mkweli na ama
nani anafanya kwa dhati ya kweli. Hivyo tunawakaribisha CUF karibuni
Arusha na wala wasitafute kisingizio cha kuegemea ili CUF ianze kutajwa
tajwa kwa kutumia mgongo wetu.
Sambamba na hili, CHADEMA mkoa wa Arusha tumesikitishwa sana na tamko la
CUF lilitolewa na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na haki za
BInadamu Mhe Abdul Kambaya, tamko lenye matisho na lugha isiyofaa. Moja
na maneno ya tamko hilo wamesema, nukuu “Uwezo wa kuwafanya tutakavyo
tunao na kwa sababu wameanza tunaweza kumaliza”.



Wakazi
wa Arusha na Watanzania wapime na waone, haya si maneno yanayoweza
kutoka kwenye kichwa cha mtu anayefikiri vizuri, mtu anayeipenda nchi
yake na kuheshimu utawala wa sheria. Zaidi ya hapo tamko hilo limesema
pia, “Ile ngangari kwa polisi tunaweza kuwahamishia wao wakose pa
kukaa”.
Katika yote haya, niwaombe wakazi wa Arusha, Wanachadema na hata
wanachama wa vyama vingine tuwapende na tuwakaribishe CUF Arusha na sote
tufanye kazi ya siasa kwa nguvu za hoja.



CUF
wanaweza kufanya hicho wanachotaka kufanya lakini CHADEMA kamwe hatupo
tayari kwa vurugu ya aina yoyote, aidha tunawakaribisha kwa moyo mmoja
na kama wapo tayari basi tufanye siasa zenye tija na manufaa kwa wakazi
wa Arusha.
Aidha nitoe onyo kali sana kwa mamluki ambao wamekuwa wakijifanya kondoo
kumbe ndani ni mbwa mwitu. Mara kadhaa watu hawa wamekuwa wakisababisha
fujo ili kukifanya CHADEMA kionekane kuwa ni chama cha vurugu.



MAMLUKI
ni sumu, tukimgundua na kumthibitisha mtu wa aina hiyo katikati yetu
tutamtangaza mbele ya jamii kuwa yeye ni sumu na kuomba wananchi
wamtenge maana anapingana kwa kuleta hila na unafiki kwenye kazi ya
kuwakomboa Watanzania.



Niwatangazie
mamluki hamtatuweza na tutawagundua tu.
Mwisho, tunapoelekea kwenye marudio ya uchaguzi mdogo kwenye kata za
Daraja II kwa Arusha mjini na Bangata kwa wilaya ya Arumeru Magharibi,
nirudie kusema maneno ya Mhe Lema kuwa iwapo viongozi na watumishi wa
umma watajihusisha na kushiriki kwa kufanya kampeni za kisiasa wakiwa
wanatumia magari na vifaa vingine vya serikali watu hawa tutawakamata na
tutawapeleka huko wanakostahili kupelekwa wezi na vibaka wengine. Hii
ni tahadhari tunamaanisha kweli na wananchi wote wawe makini “wakamate
mwizi” lengo likiwa ni kuweka adabu kwa watumishi na viongozi umma
wanaovunja sheria ya utumishi wao kwa umma na matumizi ya rasilimali kwa
namna isivyotakiwa kisheria.




 CHADEMA tutashiriki chaguzi hizi na tunawaomba wakazi wote wa maeneo haya tushiriki kwa utulivu na amani.

WANACHADEMA wote tuendelee kuwa majasiri, tusiwe waoga na tusimamie kweli na haki. 

“Hakuna kulala Mpaka Kieleweke” 


Amani Sam Golugwa 
KATIBU WA CHADEMA 
MKOA WA ARUSHA

Post a Comment

Previous Post Next Post