ANA KWA ANA NA MILOVAN, ASEMA SASA HAKUNA KULALA NA MAPIGANO KWA KWENDA MBELE

Profesa Milovan Cirkovick

BAADA ya Simba kutoa sare ya pili mfululizo jana katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, BIN ZUBEIRY leo amefanya mahojiano na kocha wa Wekundu hao wa Msimbazi, Profesa Milovan Cirkovick, raia wa Serbia kuhusu masuala mbalimbali juu ya timu yake. Endelea.
  
BIN ZUBEIRY: Habari za leo kocha
PROF MILOVAN: Nzuri, sema

BIN ZUBEIRY: Nina maswali machache nataka kukuuliza kuhusu timu
PROF MILOVAN: Uliza

BIN ZUBEIRY: Hatumuoni Abdallah Juma hata benchi, ana tatizo gani?
PROF MILOVAN: Abdallah alikuwa nje ya timu (alisafiri) kwa zaidi ya wiki moja hakufanya mazoezi na timu, ila amerudi na ameanza mazoezi, akiwa vizuri atapangwa

BIN ZUBEIRY: Na katika mechi mbili zilizopita, Edward Christopher hakucheza, wakati amekuwa akicheza vizuri siku za karibuni
PROF MILOVAN: Kweli, nilimpumzisha ili nitumie na wachezaji wengine pia na kama jana kulikuwa kuna Okwi na Ngassa, unadhani ningemuacha nani kati yao nikampanga yeye

BIN ZUBEIRY: Hata kuingia akitokea benchi ilishindikana?
PROF MILOVAN: Ungekuwa wewe ungemtoa nani ukamuingiza Edward kati ya Okwi na Ngassa

BIN ZUBEIRY: Nadhani Okwi jana hakuwa vizuri sana
PROF MILOVAN: Okwi ni mtu ambaye wakati wowote huwa natarajia kitu kutoka kwake, wakati wowote anaweza akabadilisha matokeo ya mchezo

BIN ZUBEIRY: Na siku za karibuni, Amri Kiemba humtumii kama kiungo mkabaji tofauti na mwanzoni mwa msimu
PROF MILOVAN: Unataka kuingilia kazi yangu sasa, wewe ni kocha?

BIN ZUBEIRY: Na jana pia hatukumuona kijana Shomary Kapombe pale nyuma, si kawaida, vipi?
PROF MILOVAN: Kapombe anasumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu ndiyo maana hukumuona hata benchi jana

BIN ZUBEIRY: Na unayazungumziaje matokeo ya jana kwa ujumla, ukiwa umetoa sare ya pili mfululizo
PROF MILOVAN: Ndiyo mpira, mimi na wachezaji wangu tumejifunza kitu na hatutarajii kurudia makosa

BIN ZUBEIRY: Umewasogeza karibu sana Azam, na Yanga sasa hawako mbali na wewe
PROF MILOVAN: Azam kweli wapo karibu na sisi, lakini tutaongeza juhudi sasa, wachezaji wangu na mimi sasa hivi tunaona umuhimu wa kujitolea zaidi

BIN ZUBEIRY: Mechi ijayo unarudi Tanga Jumapili kwenye Uwanja mbaya, unasemaje
PROF MILOVAN: Kweli, ni hali halisi, tutakwenda kupigana kwa vyovyote tushinde, hatutaki matokeo kama haya tena

BIN ZUBEIRY: Mwanzoni, kila baada ya mechi ulikuwa unasema kama kawaida, maana yake ushindi, lakini sasa unaizungumziaje ligi
PROF MILOVAN: Ni nzuri, ngumu na ina changamoto ya kutosha

BIN ZUBEIRY: Timu ipi unaihofia zaidi
PROF MILOVAN: Kila timu inawania ubingwa, kila timu ni mpinzani

BIN ZUBEIRY: Kuna ambayo ni mpinzani zaidi, ipi?
PROF MILOVAN: Wazi ni Azam na Yanga

BIN ZUBEIRY: Asante kocha, nakutakia siku njema na kazi njema
PROF MILOVAN: Asante, na wewe pia.

Post a Comment

Previous Post Next Post