HATIMAYE USAFIRI WA DALADALA ZA TRENI JIJINI DAR WAANZA RASMI LEO... WANANCHI KIBAO WAMEFURAHIA HUDUMA YA USAFIRI HUO USIO NA KERO YA FOLENI LEO ASUBUHI KUANZIA UBUNGO MAZIWA HADI POSTA - STESHENI, MWAKYEMBE AZINDUA PIA USAFIRI MWINGINE WA TRENI KUTOKA TAZARA HADI MWAKANGA...!

Wanacheeeeeeeeka...! Abiria wakifurahia usafiri wa treni. (Picha: Kwa hisani ya issamichuzi.blogspot.com)

Ndani ya daladala la treni ni hakuna vurugu wala longolongo... ni raha eeenh! Hivi ndivyo ilivyo ndani ya chombo. 
Chombo kikikatiza mitaa.
Mchuma wa Tazara utakaotumika kama daladala kutoka eneo la Tazara hadi Mwakanga.
Hatimaye ile ahadi ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kuhusiana na kuanzishwa kwa usafiri wa daladala za treni jijini Dar es Salaam imeanza kutekelezwa leo asubuhi na wananchi mbalimbali wakanufaika na huduma hiyo kwa usafiri kati ya Ubungo Maziwa na posta, eneo la Stesheni.

Usafiri mwingine wa treni ulio mbioni kuanza rasmi jijini Dar es Salaam baada ya kuzinduliwa leo kupitia reli ya Tazara ni wa kutoka Tazara hadi Mwakanga.

Akizungumza wakati wa kuzindua rasmi safari hizo leo, Dk. Waziri Mwakyembe aliwataka wananchi watakaokuwa wakitumia usafiri huo kuvumilia kasoro mbalimbali zitakazojitokeza katika siku za mwanzo na kuahidi kwamba serikali itaendelea kuboresha huduma hizo kila uchao.

Dk. Mwakyembe aliwataka wakazi wa Dar es Salaam, hasa kwenye maeneo yaliyo karibu na reli kutunza miundombinu ya usafiri huo, ikiwa ni pamoja na kukomesha tabia ya baadhi ya watu kugeuza maeneo ya njia za reli kuwa majalala ya kutupia uchafu.

Akawataka viongozi wa serikali za mitaa ambako reli zinapita waongoze uangalifu ili usafiri huo uendelee vyema na kuwapunguzia adha ya usafiri na foleni wakazi.

"Inasikitisha kuona kuwa katika baadhi ya maeneo, reli zimegeuzwa kuwa dampo na kujaa uchafu... nawaomba tujitahidi kutunza maeneo haya ya miundombinu ya reli," akasema Dk. Mwakyembe.

Katika hatua nyingine, Waziri Mwakyembe aliwapongeza mafundi wa TRL na Tazara kwa kufufua mabehewa 14 yaliyokuwa yamekufa kabisa na kuokoa Sh. bilioni 2.1.

Alisema vilevile kuwa vichwa vya treni vilivyofufuliwa na mafundi wa mashirika hayo na miundombinu mingine imeokoa jumla ya Sh. bilioni 18.

"Hivi vichwa peke yake, kama vingekodishwa vingetugharimu kati ya Sh. bilioni 9 au 10 hivi," alisema Dk. Mwakyembe.

Post a Comment

Previous Post Next Post