SUSAN MASHIBE
Ni mwanamke jasiri, mpiganaji mwenye utaalam wa masuala ya anga
aliyethibitishwa na Mamlaka ya Anga Marekani (FAA). Anamiliki Kampuni
ya TanJet inayojihusisha na utoaji wa ushauri wa masuala ya anga ndani
na nje ya nchi.
Mwaka jana, alinukiwa Tuzo ya Kiongozi Kijana Ulimwenguni (Global Young
Leader), aliyopewa na Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF). Kampuni yake
imekuwa ikipata tenda mbalimbali barani Afrika, Ulaya, Marekani na
kadhalika. Jopo la wajumbe wa Baraza la Congress nchini Marekani,
lilipotembelea Tanzania mwaka 2009, Mashibe ndiye aliyeratibu masuala
ya anga kuhusu ujio wao.
FLAVIANA MATATA
Mwaka 2007 alipokwenda kushiriki mashindano ya dunia ya Miss
Universe na kushika nafasi ya sita, wengi walidhani huo ndiyo mwisho
wake. Ilionekana hivyo kwa sababu warembo wengi wameshiriki mashindano
ya dunia na baada ya kurudi nchini, hawakusikika tena.
Kwa Flaviana, huo ulikuwa ni mwanzo wa kupiga hatua zaidi kusaka
mafanikio yake. Hivi sasa, mrembo huyo ni mwanamitindo wa kimataifa,
anayefanya kazi na makampuni makubwa ulimwenguni.
HAPPINESS MAGESSE
Miss Tanzania aliyechukua taji hilo mwaka 2001, Happiness
Magesse ndiye aliyefanikiwa zaidi kimataifa kuliko wote, japo wapo
wengine wanaojitahidi. Hivi sasa Happiness ‘Millen’ ni mwanamitindo wa
kimataifa.
EMELDA MWAMANGA
Ni mwanzilishi aliye pia Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Relim
Entertainment inayomiliki jarida maarufu la Kiingereza, Bang. Jinsi
alivyoweza kulisimamisha jarida hilo na kulifanya kuwa maarufu zaidi
nchini, inatosha kumpongeza kwamba ameonesha njia.
LADY JAYDEE
Jina lake asilia ni Judith Wambura. Ni mwanamuziki wa kike
mwenye mafanikio zaidi ambayo chanzo chake ni muziki. Anamiliki bendi
na mgahawa wa kisasa ambao ulimgharimu zaidi ya shilingi milioni 100
kuuanzisha. Bila shaka Jaydee ameonesha njia kwa wanamuziki wengine wa
kike hapa nchini.
MADAM RITA
Kuanzisha kitu wakati mwingine inaweza kuwa jambo rahisi lakini
uimara wa mtu ni pale anapoweza kulisimamia na kufanikiwa. Rita Paulsen
anastahili pongezi kwa namna alivyoweza kuanzisha Shindano la Bongo
Star Search na kulifikisha hapa lilipo. Huyu ni mwanamke kijana
aliyeonesha njia ya kweli ya mafanikio.
RAHMA AL-KHAROOS
Anamiliki Kampuni ya RBP Oil & Industrial Technology. Uwezo
wake uliweza kuwashtua wengi pale alipoweza kujitolea mamilioni ya
fedha kuiwezesha Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars. Mwanamke huyu
ni mfano tosha kwamba inawezekana kama tu utaamua kupambana.
SHEAR NASSA
Anamiliki maduka ya Shear Illusions, vilevile ana jarida
linaloitwa Shear Hair & Beauty. Ukubwa wa maduka yake, heshima na
umaarufu wake kwa uuzaji wa vitu vya urembo ni kielelezo cha
kumthibitisha Shear kwamba ni mwanamke kijana aliyefanikiwa, kwa hiyo
ameonesha njia.
KHADIJA MWANAMBOKA
Mbunifu wa mavazi wa kike mwenye umaarufu kuliko wanawake wote
nchini. Ameanza harakati zake akiwa na umri mdogo na kwa alipofikia
hivi sasa, ameshaonesha njia kwa wanawake wengine nchini. Jambo muhimu
ni kusimamia fani yako mpaka kuifikisha kwenye kiwango bora. Khadija
alipofikia kwa ubunifu wa mavazi, anastahili pongezi.
FINA MANGO
Alipata umaarufu mkubwa kwenye fani ya utangazaji wa redio
lakini alipoamua kuanzisha kampuni yake ya One Plus, ameweza kupata
mafanikio makubwa. Tenda ya kuratibu na kusimamia Tuzo za Muziki
Tanzania (Tuzo za Kili) kwa miaka mitatu mfululizo imedhihirisha ubora
wa kampuni yake.
***************************************************
UPO msemo uliotawala vichwa vya watu tangu dahari kwamba
wanawake ni tabaka la kukaa nyumbani na kufanya kazi za ndani. Wao
jukumu lao ni kumfurahisha mume na lingine ni kuwaandaa watoto kwa ajili
ya kwenda shule na kufuatilia nyenendo zao darasani.
Ilivyozoeleka ni kwamba wanawake ni goigoi. Utaona bungeni kuna
wabunge wa viti maalum ambavyo wengi hutafsiri kuwa ni vya upendeleo.
Kwa maana kwamba uwezo wao kushindana kwenye majimbo na kushinda ni
mdogo ndiyo maana wanapewa hivyo maalum kwao.
Katika mitihani, kuna unafuu wa alama za ufaulu kwa wanafunzi wa
kike. Yaani wanaonekana hawana uwezo wa kushindana na wavulana.
Vijijini, wanawake wamekuwa wakitumika kama nyenzo ya kilimo, yaani mama
akalime ndiyo alishe familia, baba akacheze bao au kunywa pombe.
Miaka inakwenda, wapo wanawake wengi ambao wameweza kudhihirisha
kwamba inawezekana kwa jinsi ya kike kuanzisha kazi na kufanikiwa.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro ni
mfano wenye nguvu kwa wanawake kufanikiwa.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mchungaji Getrude Rwakatare na
wengineo, ni kichocheo kinachotoa uthibitisho kuwa wanawake wanaweza. Ni
suala la kuwaamini na kuwapa nafasi, kwa hakika wanaweza kufanya mambo
makubwa mno.
Ukiachana na hao, ipo orodha ya wanawake vijana 10 ambao
wanastahili pongezi. Wamepambana katika maeneo yao kiasi cha kupata
mafanikio ambayo yameonesha njia. Inabidi tuwatambue na kuthamini
jitihada zao kwa maana wameendelea kuthibitisha ndivyo sivyo kwa wale
waliokuwa wanaamini kuwa wanawake si lolote kwenye utafutaji
Post a Comment