
UTATA bado umegubika mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow aliyepoteza maisha kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi usiku wa Oktoba 12 mwaka huu, Uwazi limejuzwa.
Taarifa kutoka chanzo chetu cha kuaminika zinaeleza kuwa tayari polisi wameingia kazini kuchunguza sababu hasa za mauaji hayo na waliohusika huku simu alizopigiwa na alizopokea kamanda huyo wiki moja kabla ya mauaji zikifuatiliwa kwa kina.

“Polisi wameingia mpaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na katika mitandao mbalimbali ya simu ili kuchunguza mawasiliano ya Kamanda Barlow na watu wengine.

Mwili wa Marehemu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,
Liberatus Barlow ukiagwa katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Kamanda Barlow aliyekuwa akiendesha gari lake binafsi aina ya Toyota Hilux- Double Cabin baada ya kuuawa habari zinasema wauaji walichukua simu zake mbili, ambazo sasa polisi wanazifanyia kazi kwenye mitandao ya simu.
Habari za ndani za kipolisi zinasema kuwa mwalimu Doroth ambaye anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mwanza kwa mahojiano zaidi tayari simu yake ipo mikononi mwa jeshi hilo kwa lengo lilelile la kuifanyia uchunguzi.
Bado wananchi wengi wa Mwanza wanaamini kwamba mtandao wa ujambazi ndiyo unahusika na kifo cha Kamanda Barlow kwa kuwa alikomaa nao kuhakikisha wahalifu hao hawafurukuti.

Mbali na mtandao wa ujambazi kutajwa, vibaka nao jijini humo wamekuwa na wasiwasi mkubwa, wanaishi kwa tahadhari wakiamini msako wa polisi wa safari hii utawaingiza selo wengi wao.
Kufuatia mauaji hayo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI Robert Manumba ameweka kambi jijini Mwanza kuongeza nguvu ya uchunguzi wa tukio hilo.
Manumba alipotafutwa na mwandishi wetu juzi Jumapili na kuulizwa walichokipata kuhusiana na sakata hilo, alisema kwa kifupi kwamba waachwe wafanye upelelezi wao na watatoa taarifa kwa wana habari wakati muafaka ukifika.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliozungumzia mauaji hayo walielezea kushangazwa kwao na hatua ya Barlow kutembea usiku bila mlinzi wake (bodyguard) ambaye kwa kiwango kikubwa angeweza kusaidia kumuepushia kifo hicho.

Wanafamilia
wa marehemu, Kamanda Liberatus Barlow wakiwa na majonzi makubwa sana
katika uwanja wa Nyamagana wakati wa kuuaga mwili wa mpendwa wao.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, alipoongea na wana habari mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema mauaji hayo yalifanyika kati ya saa 7 na saa 8 usiku, wakati Barlow akimsindikiza mwalimu Doroth.
Inasemekana wote wawili walikuwa wametoka kuhudhuria kikao cha maandalizi ya harusi ya mtoto wa dada wa Barlow, kilichofanyika kwenye Hoteli ya Florida jijini Mwanza.
Marehemu Lebaratus Barlow anakuwa kamanda wa polisi wa kwanza nchini kuuawa. Miaka ya sabini, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Iringa, Dk. Wilbert Kleruu naye aliuawa lakini mauaji yake yalitekelezwa na mkulima aliyeitwa Said Mwamwindi kufuatia madai ya kutofautiana ‘lugha’.
GPL
Post a Comment