Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
ametaka wananchi wa Kenya wapewe nafasi ya kuamua ni viongozi gani
wanawataka katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Machi mwakani.
Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa wananchi wa Kenya wanayo haki ya msingi
kabisa kuamua hatma ya taifa lao katika Uchaguzi Mkuu huo.
Mheshimiwa
Rais aliyasema hayo leo Oktoba 21, 2012 alipokutana na kufanya
mazungumzo na ujumbe wa wabunge wa vyama mbalimbali vya siasa vya nchini
Kenya uliomtembelea Ikulu jijini Dar es salaam.
Ujumbe
huo uliongozwa na Naibu Waziri Mkuu wa Kenya na Waziri wa Fedha Mhe.
Uhuru Kenyatta ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha TNA na Waziri wa
Sheria wa Kenya Mhe Eugene Wamalwa wa chama cha New Ford Kenya. Wote
wawili ni wagombea wa nafasi ya Urais katika uchaguzi ujao.
Wengine
katika msafara huo walikuwa ni Naibu Waziri wa Afya na mbunge wa
Mombasa Mhe. Kambi Kazungu, Mbunge wa kuteuliwa wa chama cha TNA Bi
Rachel Shebesh, na Mbunge wa Kajiado kwa tiketi ya TNA Moses ole Sakuda
na mbunge wa zamani Mhe Abdullahi Alli.
Rais
Kikwete aliwapongeza kwa kuamua kufanya kazi kwa pamoja licha ya kuwa
watakuwa washindani katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu huo.
Mheshimiwa
Rais ameitakia heri nchi ya Kenya katika uchaguzi huo ujao, na
kusisitiza kwamba nchi hiyo ya jirani ina umuhimu katika mustakabali wa
kiuchumi kwa nchi za Afrika Mashariki.
Rais
Kikwete wakati huo akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) alikuwa
miongoni mwa viongozi walioshughulika sana kutafuta ufumbuzi wa ghasia
na vurugu zilizozuka kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 nchini Kenya.
Rais
Kikwete alikaa siku tatu nchini Kenya akitafuta usuluhishi wa vurugu
hiyo ya kisiasa nchini humo, ambayo katika mazungumzo yake leo ameyataja
kama ajali iliyolipata Taifa la Kenya, na ambayo majirani wake
hawaitarajii kutokea katika uchaguzi ujao.
Imetolewa na:
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS
DAR ES SALAAM,
21 Oktoba, 2012
Post a Comment