REFA KUTOKA KUCHEZESHA PAMBANO LA WATANI JUMATANO HII.

Felix Sunzu wa Simba akiwa chini ya ulinzi wa mabeki wa Yanga, Nadoir Haroub 'Cannavaro' aliye karibu na msaada wa Oscar Joshua nyuma yake


REFA Mathew Akrama kutoka Mwanza ndiye atakayechezesha mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baina ya wapinzani wa jadi nchini, Yanga na Simba itakayochezwa keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura amesema kwamba katika mechi hiyo namba 80 ya Ligi Kuu itakayoanza saa 1:00 usiku na kurushwa moja kwa moja na Televisheni ya Super Sport ya Afrika Kusini, Akrama atasaidiwa na Samuel Mpenzu kutoka Arusha na Ephrony Ndissa wa Dar es Salaam wakati refa wa mezani atakuwa Oden Mbaga pia wa Dar es Salaam.
Amesema tiketi kwa ajili ya mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baina ya wapinzani wa jadi nchini, Yanga na Simba itakayochezwa keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, zitaanza kuuzwa kesho kwenye vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Alivitaja vituo vitakavyotumika kuuza tiketi hizo kuanzia saa 4 asubuhi ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Uwanja wa Taifa, Kituo cha Mafuta OilCom Ubungo, Mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Ohio/Samora, Dar Live Mbagala na Kituo cha Mafuta Buguruni.
Alikumbushia viingilio, cha chini kwenye mechi hiyo ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani ambavyo ni 19,648 kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000. Watazamaji watakaoketi kwenye viti vya rangi ya bluu ambavyo ni 17,045 watalipa sh. 7,000 kwa tiketi moja.
Sh. 10,000 ni kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 wakati VIP C inayochukua watazamaji 4,060 itakuwa sh. 15,000. Kwa upande wa VIP B tiketi ni sh. 20,000 na VIP A yenye watazamaji 748 tu kiingilio kitakuwa sh. 30,000.

Post a Comment

Previous Post Next Post