SIRI YA KUWAKAMATA SIMBA ZAFICHULIWA - KIBADENI

Kibadeni

KOCHA wa Kagera Sugar, Abdallah Athumani Seif ‘Kibadeni’ amesema kwamba alijua ataifunga Simba jana, lakini bahati mbaya ikawa sare na ameridhika na matokeo hayo pia kwa ilikuwa mechi ya ugenini.
Kibadeni alisema kwamba katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kilichompa matumaini ya kuifunga Simba ni kwa sababu anamjua vizuri kocha wa timu hiyo, Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick kwa kuwa alifanya naye kazi.
“Mimi nilijua tu nitawapa tabu Simba, kwa sababu Milovan ninamjua, nimefanya naye kazi mimi Simba, ufundishaji wake naujua,”alisema Kibadeni.    
Kagera jana ilitoka nyuma kwa mabao 2-0 na kupata sare ya 2-2 na Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hiyo ikiwa sare ya pili mfululizo kwa Wekundu hao wa Msimbazi, baada ya Jumamosi pia kulazimishwa sare ya bila kufungana na Coastal Union mjini Tanga.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 18 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, kutokana na Azam FC kulazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Hadi mapumziko, Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr. dakika ya nane, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’ kutoka wingi ya kulia.
Kwa ujumla kipindi cha kwanza timu zote zilishambuliana kwa zamu, ingawa ni Simba walioonekana kufanya mashambulizi ‘yenye akili’ zaidi.
Kipindi cha pili Simba ilirudi na moto tena na katika dakika ya 51, Mrisho Khalfan Ngassa aliifungia timu hiyo bao la pili kwa shuti kali lililowababatiza mabeki wa timu hiyo na kutinga nyavuni.
Hilo lilikuwa bao la tatu kwa Ngassa tangu ajiunge na Simba katika mechi tisa alizoichezea timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi.
Baada ya hapo, Kagera walizinduka na kuanza kulishambulia lango la Simba kupitia pembeni na katika dakika ya 64 Themi Felix aliunganisha kwa kichwa krosi ya George Kavilla na kuifungia Kagera bao la kwanza.
Bao liliwazindua Kagera, ambao waliongeza kasi ya kulishambulia lango la Simba na katika dakika ya 66, Juma Nyosso alimkwatua kwenye eneo la hatari Paul Ngwai na Salum Kanoni akaenda kumtungua Juma Kaseja, akiisawazishia Kagera.
Baada ya hapo timu zilianza kushambuliana kwa zamu na mpira ulinoga zaidi kutokana na mashambulizi ya pande zote mbili.
Katika mechi nyingine, Mgambo imeshinda mechi ya tatu mfululizo, baada ya kuifunga Toto African 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. JKT Ruvu imezinduka baada ya kuifunga Polisi Morogoro 2-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na JKT Oljoro imetoka 0-0 na African Lyon.
Simba SC; Juma Kaseja (Nahodha), Nassor Masoud ‘Chollo’/Uhuru Suleiman, Amir Maftah, Paschal Ochieng, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto/Edward Christopher, Amri Kiemba, Haruna Moshi/Jonas Mkude, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa.
Kagera Sugar; Andrew Ntala, Salum Kanoni, Martin Muganyizi, Amandus Nesta (Nahodha), Benjamin Effe/Themi Felix, Malegesi Mwangwa, Daudi Jumanne/Kamana Salum, George Kavilla, Shijja Mkinna, Enyinna Darlington na Wilfred Ammeh/Paul Nwai.
Katika mchezo wa awali, Simba B iliifunga Moro United mabao 3-0 katika mchezo wa utangulizi kabla ya mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Simba na Kagera Sugar, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.   
Mabao ya Simba B inayofundishwa na Suleiman Matola, akisaidiwa na Amri Said ‘Stam’ yalipatikana yote kipindi cha pili, wafungaji Ramadhan Salum dakika ya 65 na 70 na Miraj Athumani dakika ya 85.  Moro United inajiandaa na Ligi Daraja la Kwanza, inayotarajiwa kuanza Oktoba 24, mwaka huu.

Post a Comment

Previous Post Next Post