SIKU
chache baada ya Jeshi la Polisi kutoa taarifa yake ya uchunguzi kuhusu
kifo cha aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow,
umeibuka utata wa mali alizokuwa akimiliki, huku akidaiwa kumiliki
utajiri wa kutisha likiwamo jengo la ghorofa.
Habari za kiuchunguzi
zilizopatikana zinaeleza kuwa mbali ya jengo hilo, Kamanda Barlow
anadaiwa pia kumiliki magari zaidi ya saba yakiwamo malori mawili aina
ya Fuso, malori mawili ya mchanga, gari dogo aina ya Toyota Cresta
pamoja na Toyota Hilux Double Cabin.
Magari hayo yanadaiwa kuhifadhiwa eneo la Nyakato mjini Mwanza, yakisimamiwa na mfanyabiashara mmoja kwa niaba yake.
Mbali na magari hayo
kamanda hyo anatajwa kumiliki nyumba ya kifahari mkoani Mara, ambayo
aliijenga alipokuwa RPC mkoani humo, huku nyumba nyingine ikiwa maeneo
ya Capri-Point jirani na Ikulu ndogo mkoani Mwanza, inayoelezwa kuwa
aliinunua baada ya Serikali kutangaza uuzaji wa nyumba zake kwa
watumishi wake.
Umiliki wa mali hizo
umeibua maswali mengi, wengi wakitaka kujua iwapo zinalingana na kipato
cha Kamanda Barlow, licha ya kuwa na cheo cha Kamanda wa Polisi wa mkoa.
Jengo la ghorofa
Moja ya mali za Kamanda
huyo ambazo zimeanza kuwa gumzo mjini Mwanza ni jengo la ghorofa ambalo
ujenzi wale ulikuwa ukiendelea katika kiwanja Namba 173 Block G, eneo
la Nyakato Mahina kwa kibali Na. 6400 (Building Permit), kilichotolewa
na ofisi ya Mhandisi Jiji la Mwanza kikiruhusu kujenga jengo la ghorofa
tatu.
Mhandisi wa Jiji
Mhandisi wa Jiji la
Mwanza, Boniface Nyambele alikiri Kamanda Barlow kuomba kibali cha
kujenga jengo la ghorofa katika kiwanja hicho na kwamba, hata ujenzi
wake walikuwa wakiufuatilia kwa karibu.
“Kibali kilichotolewa
hapa kilikuwa ni kwa ajili ya kujenga jengo la ghorofa tatu, alipoanza
ujenzi alieleza kuwa anataka kujenga ghorofa tano, lakini baada ya
kukagua jengo hili tulikuta foundation yake ikiwa na uwezo wa kuhimili
ghorofa tatu tu, tulimzuia,” alisema Nyambele.
Hata hivyo, mmoja wa
wasimamizi wa ujenzi wa jengo hilo, ambaye hakutaka kutajwa jina lake
alisema kuwa marehemu Kamanda Barlow, aliwasisitiza kujenga ghorofa
tano.
Alisema kwamba kila
mara kamanda huyo alikuwa akiwaeleza kuwa masuala ya vibali kutoka Jiji
wanapaswa kumwachia yeye licha ya wakaguzi kumkatalia.
“Baada ya kuwa
tumejenga hapa ,mwezi mmoja kabla ya kufariki alituita na kumweleza
fundi wetu mkuu kuwa alikuwa amebadili mawazo ya kujenga jengo la
ghorofa tatu na kwamba, mpango wake sasa ulikuwa ni kuongeza ghorofa
nyingine mbili juu,” alisema mmoja wa wasimamizi wake wa ujenzi na
kuongeza:
“Alipoelezwa kama kisheria haikubaliki, alidai hayo hayamuhusu atasimamia yeye huko kwenye sheria.”
Mwandishi wa habari
hizi alifika eneo linapojengwa ghorofa hilo na kushuhudia ubao
unaoonyesha kuwa kibali cha ujenzi wa jengo hilo kimetolewa kwa
Liberatus Barlow.
Wizi ulikwamisha ujenzi
Hata hivyo, majuma
machache kabla ya kifo chake, eneo hilo la ujenzi kulitokea wizi wa
nondo za ujenzi, ambapo baada ya tukio hilo mwangalizi wa jengo hilo na
baadhi ya mafundi wake walikamatwa na kuwaweka mahabusu kwa siku nne
katika Kituo cha Polisi Nyakato Mwatex huku ikielezwa kuwa kamanda huyo
aliwatoa baada ya kukubaliana nao kumlipa nondo zilizopotea.
“Siku ya wizi huo
ujenzi ulisimama na tulikamatwa na kulazimishwa kulipa nondo 10 alizodai
zimeibwa, lakini msimamizi wetu nakumbuka aliamua kulipa yeye badala
yetu na kesi iliishi baada ya kuwekwa ndani siku nne. Alilipa nondo 60
badala ya 10 na huo ulikuwa mwisho wake wa kuendelea na kazi pamoja
nasi, ” alisema kijana huyo aliyewahi kufanya kazi ya kibarua katika
jengo hilo.
Umiliki wa magari na utata
Mali nyingine
zinazodaiwa kumilikiwa na Kamanda Barlow ni pamoja na magari, ambapo
katika idadi ya magari hayo, gari moja aina ya Toyota Hilux ambalo ndilo
alipata nalo ajali limeonekana kuwa na utata katika umiliki wake
kutokana na namba hiyo ya usajili kubainika kuwa siyo yake kwa vile
ilisajiliwa kwa gari aina ya Nisan Premier inayomilikiwa na wamiliki
wawili.
Ingawa umiliki wa
magari mengine unadaiwa kusajiliwa kwa majina ya mfanyabiashara maarufu
jijini Mwanza, lakini umiliki wa gari ambalo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,
Evarist Ndikilo, alipotangaza kifo cha kamanda huyo, alilitangaza pia
kuwa ni mali ya marehemu, imebainika kuwa alilipata wiki moja kabla ya
kifo chake.
Katika uchunguzi wa
Mwananchi Jumapili, imebainika kuwa hata bima ya gari hilo iliyoonyesha
imekatwa kutoka Kampuni ya Bima ya Zanzibar, ilikuwa haitambuliki.
Kamanda Barlow
alilichukua gari hilo kwa mmoja wa wafanyabiashara jijini Mwanza, ambaye
bado jeshi hilo la polisi linamsaka kutokana na utata wa umiliki wake,
kuonyesha namba hiyo siyo halisi ya gari hilo.
Meneja wa Kampuni ya Bima
Meneja wa Tawi la
Kampuni ya Bima Zanzibar Mkoa wa Mwanza, Suzan Masele alipotakiwa kutoa
ufafanuzi wa suala hilo, alisema kuwa stika ya bima ya gari hilo
alilokuwa nalo Kamanda Barlow, wamefuatilia kwenye mfumo wao wa malipo
wakabaini kuwa haipo.
"Tumeangalia katika system (mfumo) yetu hakuna bima ya malipo hayo, kwa hiyo ni feki," alisema.
Aidha, utata wa umiliki
wa gari hilo pamoja na bima yake ulithibitishwa na Mkuu wa Jeshi la
Polisi nchini (IGP), Said Mwema, ambaye alisema jijini Mwanza kuwa jeshi
lake lilikuwa likiendelea na uchunguzi wa umiliki wa gari hilo, pamoja
na bima yake kujua ukweli na jinsi lilivyoingia mikononi kwa marehemu
siku kadhaa kabla ya kifo chake.
“Suala la gari
alilokuwa akilitumia marehemu mpaka siku mauti yanamkuta, pamoja na bima
yake, hatuwezi kulieleza hapa, kwa sasa bado tunachunguza,” alisema
IGP, alipoulizwa na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumaliza
kutoa taarifa za awali za uchunguzi wa kifo Kamanda Barlow.
Habari na Frederick Katulanda, Mwanza
Chanzo - Mwananchi
Post a Comment