Na Salma Said, Zanzibar
VIGOGO watano wa Uamsho wanashikiliwa na polisi na wanatarajiwa
kufikishwa mahakamani leo huku Jumuiya hiyo ikitoa waraka wa kuwataka
Waislamu wadumishe amani.
Viongozi hao wako mikononi mwa polisi tangu juzi wakihojiwa mambo kadhaa
likiwemo la kutoweka mmoja wao, Farid Had Ahmed ambaye ilidaiwa kuwa
alikamatwa na polisi kwa siku nne.
Mbali na Farid vigogo wengine wa uamsho ambao wanahojiwa na polisi ni
Amiri wa Uamsho, Sheikh Mselem Ali Mselem, Naibu wake, Azzan Khalid
Hamdan, Mussa Juma na Hassan Bakar.
Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema jana kwamba
wanawahoji msheikh hao na watawafikisha mahakamani leo iwapo wataona
kuna mashitaka ya kujibu.
Katika hatua nyingine, Uamsho imetoa waraka kwenye misikiti ya Zanzibar
wakiwataka Waislamu wawe watulivu na kuhudhuria kwa wingi mahakamani leo
wakiwa na vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.
Waraka huo uliosambazwa unasema hivi: “Kama hali ilivyo na mnavyosikia
mnaombwa muwe watulivu na mufanye subra na leo (jana) hapo Msikiti wa
Mbuyuni hapatakuwa na muhadhara si Adhuhuri wala Alasiri. Mnachoombwa na
viongozi wenu muwe wavumilivu na watulivu hadi kesho (leo) mufike
mahakamani bila ya fujo na muchukue kopi za vitabulisho vyenu vya
Mzanzibari.
“Jingine ni kuwa msikae vikundi na mkawapa askari sababu, tunasisitiza
amani na utulivu na Waislamu ni wenye kutii amri za viongozi wao.
Tunasisitiza mani na utulivu pia subra na dua kwa wingi . Ukipata
taarifa hii mjulishe na mwenzio toa kopi na uwape wengine. Wabillah
taufq.”
Waraka huo ambao ulikuwa unasambazwa katika misikiti jana haukutiwa saini na mtu yeyote wala haukutaja umetolewa na nani.
Wakili wa Uamsho, Salim Tawfik alisema jana kuwa wateja wake
watafikishwa mahakamani leo lakini akalaumu kwamba Polisi wamewahoji
bila ya yeye kuwepo.
“Mimi nilikwenda polisi nikakuta Mselem anahojiwa nikataka kuingia
wakanizuia, wakasema wataniita lakini hawakufanya hivyo,” alidai wakili
huyo.
Hali ya Zanzibar imetulia lakini ulinzi wa polisi na askari wa vikosi
vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wameimarisha ulinzi katika maeneo
mbalimbali ya mji huu wakiwa wanazunguka na silaha mikononi.
Kwa siku tatu mji wa Zanzibar ulikumbwa na ghasia kubwa kwa askari
kupambana na wananchi ambao walikuwa wakiamdamana wakitaka Sheikh Farid
aachiwe.
Post a Comment