Baada ya habari kutolewa jana na leo juu ya uamuzi wa Spika kuhusu tuhuma kwamba
baadhi wa wabunge na wajumbe wa kamati ya Nishati na Madini walijihusisha na vitendo
vya rushwa katika kutekeleza kazi zao za kibunge, nimeulizwa na baadhi ya wanahabari
na wananchi kwa simu na kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii sababu za kusimama
bungeni tarehe 9 Novemba 2012 mara baada ya Spika kutoa uamuzi huo na kutaka kuomba
muongozo.
Nalazimika kutoa ufafanuzi huu nje ya bunge baada ya mkutano wa bunge kuahirishwa
bila Spika kunipa fursa ya kusema jambo hili bungeni kwamba nilitaka muongozo wake
kwa mujibu wa Kanuni ya 5(1) na 5 (2) kuwa nakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi
wake kutokana na kuwa na maudhui kadhaa yasiyozingatia katiba ya nchi, sheria
mbalimbali za nchi, kanuni za kudumu za bunge, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge
pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana
na utaratibu wa bunge letu.
Hata hivyo kwa kuzingatia kuwa rufaa huchukua muda kusikilizwa nilitaka niombe
muongozo wake kabla ya Mkutano wa Bunge kuahirishwa kwa kuwa katika uamuzi wake
hakueleza hatma ya Kamati ya Nishati na Madini ilivyovunjwa, hivyo Spika anapaswa
bado kueleza kwa umma iwapo kamati hiyo inarejeshwa au inaundwa kamati nyingine au
kuelekeza kamati nyingine ya kudumu ya Bunge inayopaswa kuisimamia Serikali wakati
huu ambapo nchi inakabiliwa na matatizo mengi kwenye sekta za nishati na madini
yenye athari kwa maisha ya wananchi.
Kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nasisitiza kwamba Spika
anapaswa kurejea barua yangu ya toka mapema Oktoba wake ambayo mpaka sasa
haijapatiwa majibu, hoja niliyoiwasilisha bungeni na kuungwa mkono ya jambo
lililohusu haki za bunge na miongozo niliyoomba bungeni kuhusu masuala ya nishati
kwa nyakati mbalimbali katika mkutano wa Bunge uliomalizika na kutoa kauli kwa
umma.
Kwa kuwa katika uamuzi wake Spika wa Bunge ameeleza kwamba Waziri wa Nishati na
Madini Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake Eliackim Maswi wametoa maelezo
yasiyokuwa kweli kwa nyakati mbalimbali uwepo wa kamati ya bunge kwa ajili ya
kuisimamia Wizara hiyo kwa niaba ya bunge ni suala linalohitaji uamuzi wa haraka.
Aidha, katika uamuzi wake Spika zaidi ya kutoa onyo kali kwa Katibu Mkuu na Wabunge
hakutoa onyo kwa Waziri wa Nishati na Madini wala hakueleza chochote iwapo alipokea
ushauri kutoka kwa Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu
ukiukwaji wa kanuni uliofanywa Spika bungeni wakati wa kadhia nzima.
Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Spika anaweza kutoa taarifa bungeni wakati wowote na
taarifa yake haijadiliwi hivyo sehemu kubwa ya taarifa ya tarehe 9 Novemba 2012
ilikuwa ni maelezo kuanzia sehemu ya kwanza mpaka sehemu ya pili.
Uamuzi wa Spika unapatikana sehemu ya tatu ya maelekezo hususan kifungu cha 6.12 ya
kwamba “tuhuma husika hazikuweza kuthibitishwa” na baadaye kufuatiwa na uamuzi wa
Spika kuhusu watoa tuhuma katika vipengele (a), (b), (c) na (d).
Nakusudia kukata rufaa ili taarifa kamili ya Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge iweze kuwasilishwa kwa ukamilifu wake kwenye kamati husika ya
kudumu ya Bunge na hatimaye taarifa kamili kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni ili
‘mbivu na mbovu’ zijulikane na masuala yanayohitaji kufanyiwa uchunguzi wa ziada na
vyombo vingine vya nje ya Bunge yaendelee kwa hatua zaidi badala ya uamuzi huu wa
‘funika kombe’.
Yapo masuala ya ziada ambayo binafsi niliyaeleza mbele ya kamati ndogo chini ya
kiapo ambayo sitakiwi kuyaeleza nje ya bunge kwa mujibu wa kanuni na sheria husika ,
hata hivyo taarifa kamili ikiingia bungeni kutakuwa na uhuru wa majadiliano kwa
mujibu Kwa Ibara ya 100 ya Katiba ya Nchi.
Aidha, nitaka rufaa kwa kuwa kiwango cha ‘adhabu’ kilichotolewa kwenye uamuzi wa
Spika hakilingani na ‘makosa’ ambayo yameelezwa kuwa na uzito wenye kuathiri “kwa
kiasi kikubwa hadhi ya Bunge kama taasisi na heshima ya wabunge waliohusishwa”.
Spika amefanya uamuzi wake chini ya Kanuni ya 5(1) na 72 (1) lakini hakuzingatia
kuwa kanuni ya 72 (3) inaeleza kuwa iwapo mbunge ameshindwa kuthibitisha ukweli
Spika amepewa fursa ya kumsimamisha mbunge huyo kuhudhuria vikao vya Bunge
visivyozidi vitano.
Aidha nitaka rufaa kwa kuwa waliodaiwa kutoa kutoa tuhuma bila ushahidi walipaswa
kujieleza kwa tuhuma hizo kabla ya kuhukumiwa kwa misingi ya kanuni za haki ya asili
zilizopo pia katika katiba ya Nchi na kwa kuzingatia matakwa ya kanuni za kudumu za
Bunge; hata hivyo Spika amefikia uamuzi wa moja kwa moja wa kutoa adhabu ya ‘onyo
kali’ kinyume na masharti ya kanuni ya 5 (1).
Ikumbukwe kwamba Spika katika maelezo yake amesisitiza kuwa Kamati Ndogo ilipewa
hadidu rejea moja tu, “Kuchunguza na kumshauri Spika iwapo tuhuma kwa baadhi ya
wabunge na wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini kujihusisha na vitendo vya rushwa
ni za kweli au hapana”, baada ya kuchunguza kwa mujibu wa hadidu rejea hiyo na
kuwasilisha ripoti yake Spika alipaswa kama kuna ukiukwaji mpya wa kanuni
uliobainika kutokana na uchunguzi huo kuanzisha mchakato wa adhabu.
Binafsi niliitwa kwa maandishi kuisaidia kamati ndogo katika uchunguzi wake kutokana
na maoni niliyowasilisha bungeni kwa niaba ya kambi rasmi ya upinzani, sijawahi
kuandikiwa au kuitwa popote kutakiwa kujieleza kwa ‘kuisemea tuhuma bungeni bila ya
kufanya utafiti kupata ukweli’ na maelezo yangu niliyoyatoa bungeni hayakukiuka
kanuni yoyote ya bunge kama ambavyo nitathibitisha wakati nitakapokata rufaa.
Kwa upande mwingine nitaka rufaa kwa kuwa adhabu aliyopewa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini Eliakim Maswi hailingani na ukubwa wa makosa anayodaiwa kuyafanya,
ikiwa ni kweli amevunja haki za bunge kwa kuzusha tuhuma za uongo dhidi ya wabunge
kwa ajili ya kujihami dhidi ya baadhi ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya Nishati na
Madini waliokuwa wanahoji kuhusu utendaji wa Wizara yake.
Kwa kosa hilo ikiwa maelezo ya Spika kuhusu matokeo ya uchunguzi wa Kamati ni sahihi
anapaswa kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za
Bunge na kupewa adhabu ya zaidi ya onyo ikiwemo hata faini au kifungo au walau
kutakiwa kuwajibika.
Kadhalika kwa Spika ameeleza kuwa mbinu aliyotumia ni pamoja na kutaka kuwalipa
fedha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini shilingi milioni mbili kwa
kila mjumbe madai haya ni ya jaribio la kufanya ufisadi wa fedha na matumizi mabaya
ya madaraka kama ilivyokuwa kwenye kashfa ya Katibu Mkuu aliyemtangulia David Jairo
hivyo Spika alipaswa kupendekeza kwa mamlaka ya uteuzi wake kuchukua hatua za
kinidhamu na kisheria.
Uamuzi wa Spika ‘kufunika kombe’ hauna tofauti na maamuzi yaliyotangulia ambayo
yamesababisha mpaka sasa Serikali haijawasilisha bungeni ripoti ya utekelezaji wa
maazimio ya Bunge kufuatia uchunguzi uliofanywa na kamati teule ya Bunge.
Ni vizuri ikakumbukwa kwamba katika hotuba yangu bungeni kwa niaba ya Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni tarehe 27 Julai 2012 nilisisitiza kwamba “ili ukweli wa kina uweze
kujulikana Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa bunge liazimie kuunda Kamati
Teule ya Bunge kuchunguza masuala yote ya ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya
madaraka na tuhuma za ufisadi katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na
ununuzi wa mafuta wa ajili ya mitambo ya umeme.
Uchunguzi huo uhusishe pia mkaguzi mkuu kufanya ukaguzi wa kiuchunguzi (Forensic
Audit) kwa malipo yaliyofanywa na makampuni ya BP (Sasa PUMA Energy), Oryx na Camel
Oil ili kubaini iwapo kuna vigogo zaidi wa serikali waliojinufaisha kwa kisingizio
cha dharura ya umeme. Izingatiwe kwamba masharti ya ibara ya 27(2) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamtaka kila mtu “… kutunza vizuri mali ya Mamlaka
ya Nchi na ya pamoja (na) kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu….”.
Mchakato huu ungewezesha kupata ukweli wa ziada kibunge kuliko utaratibu uliotumiwa
na Kamati Ndogo na Spika. Kesho tarehe 11 Novemba 2012 nitaeleza masuala ya ziada
nitakayoyakatia rufaa na kauli yangu kuhusu maelezo na uamuzi wa Spika juu ya Waziri
na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini.
John Mnyika (Mb)
10/11/2012
Post a Comment