Msanii mkongwe katika tasnia ya sanaa ya maigizo na vichekesho nchini
maarufu kama Mzee Small ameongea na bongo5 exclusively na kusema kwa
sasa anaendelea vizuri kiasi japokuwa hali yake bado haijatengemaa kwa
asilimia kubwa.
Tukimnukuu anasema “mimi bado naumwa na ugonjwa wa “kiharusi”
ambapo tangu tarehe 20 mwezi 5 mwaka huu mpaka leo hii kidogo nimekuwa
napatiwa matibabu kwa matabibu wa tiba asilia. Ugonjwa huu niliupata
wakati natokea Mwanza ambapo nilikuwa nimechukuliwa na mtangazaji mmoja,
jina silikumbuki na kuwaburudisha kabla ya kusafiri kwenda nje ya nchi.
Ugonjwa huu ulinipata asubuhi ya tarehe hiyo tano baada ya kurudi
kutoka Mwanza ambapo baada ya kulala nilipoamka nikajikuta mwili unagoma
kufanya matendo ya kawaida yaliyozoeleka kama kushindwa kuamka na kukaa
kwenye kiti mwenyewe bila msaada wa mtu mwingine.
Kuona hivyo mke wangu akanipeleka kwenye moja ya hospitali ya maeneo
ya hapa Tabata Kimanga, ndipo walipogundua nina Kiharusi na daktari
akanieleza nimepooza upande wote wa kushoto kwangu.”
Mzee Small anaendelea kusema baada ya matibabu ya awali wauguzi na
madaktari walimhamishia hospitali ya taifa Muhimbili ingawaje kwa sasa
anadai anamtegemea zaidi tabibu wa tiba asilia kutoka Kigoma ambaye
ndiye anafanya kazi ya kumitibu kwa kumchua, kumnyoosha na kumfanyisha
mazoezi ya viungo.
Mzee Small alichukua fursa hiyo ya kuongea na bongo5 kuwashukuru
wadau wote wakiwemo wasanii ,vyombo vya habari, ndugu jamaa na marafiki
kwa kuweza kumchangia kwa namna moja na nyingine pamoja na kupigiwa
simu na watu wengi wa kumtakia kheri.
Alimalizia kwa kuwashukuru wananchi wote kwa kumjali katika kipindi hiki kiugumu kwake.
Chanzo:- bongo5
Post a Comment